KWA miongo kadhaa baada ya uhuru mwaka wa 1963, siasa za Kenya ziligeuka kuwa muundo wa madaraka yaliyojikita katika urais.
Marais wa zamani Mzee Jomo Kenyatta na Daniel arap Moi walikuwa na mamlaka yaliyopita kiwango cha kawaida cha utendaji wa serikali, waliweza kuajiri na kufuta kazi maafisa wa umma, kuvunja bunge, kudhibiti utawala wa mikoa, na hata kutumia maaafisa wa usalama kuwaangamiza wapinzani wao.
“Urais wa kifalme,” kama ulivyotambuliwa, ulikuwa nembo ya utawala wa Kenya.
Kuanzia miaka ya 1990, vuguvugu la kutaka mabadiliko ya kisiasa lilishika kasi. Mashirika ya kijamii, makanisa, wanasiasa wa upinzani na wananchi wa kawaida walitaka kuwe na mipaka ya madaraka ya rais.
Ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007/08, ambapo zaidi ya watu 1,000 waliuawa na zaidi ya 600,000 wakafurushwa makwao, zilifichua hatari ya mfumo wa kisiasa wa “mshindi kutwaa kila kitu.”
Kufuatia hilo, Kenya ilianza safari ya mageuzi ya kihistoria iliyozaa Katiba ya 2010, inayotambulika kama mojawapo ya katiba za kisasa na bora barani Afrika.
Kiini cha katiba hiyo kilikuwa juhudi ya makusudi ya kudhibiti madaraka ya rais.
Hata hivyo, makamu wa rais wa zamani Kalonzo Musyoka anaonya kwamba Kenya inarudi kwenye utawala wa kiimla, licha ya kinga zilizowekwa na Katiba ya 2010. Anasema, miaka 15 tangu katiba hiyo izinduliwe, urais wa kifalme bado haujadhibitiwa.
Akizungumza kwenye kongamano la kila mwaka la Chama cha Mawakili Kenya (LSK) mnamo Agosti 15, Bw Kalonzo—ambaye pia ni Wakili Mkuu na mwanasiasa wa upinzani—alisema kuwa ahadi ya Katiba ya kulinda utawala wa sheria iko hatarini kutokana na ukandamizaji wa serikali, utekaji nyara, na ukiukaji wa haki za binadamu.
“Miaka ya 2024–2025 imekuwa mfano halisi wa ukandamizaji unaotekelezwa na serikali ambao haujawahi kushuhudiwa katika historia ya miaka 62 ya uhuru wa Kenya,” alisema Kalonzo, akitaja visa vya utekaji nyara, kupigwa kwa waandamanaji wa amani, na vikundi vya uhalifu vinavyofanya kazi chini ya ulinzi wa polisi.
Kwa mujibu wake, vijana wanaotekeleza haki yao ya kuandamana wanatekwa nyara, kuteswa na kushtakiwa chini ya Sheria ya Kuzuia Ugaidi. Licha ya mateso hayo, bado wanabaki na imani kuwa Katiba ndiyo kinga dhidi ya utawala wa kiimla.
Kituo cha Sheria kinasisitiza kwamba nguvu halisi ya Katiba ya 2010 katika kudhibiti urais wa kifalme inapatikana kwenye Sura ya Haki za Binadamu.
“Kwa msingi wa Ibara ya 19 na 20, Sura ya Haki za Binadamu ndiyo moyo wa demokrasia ya kikatiba ya Kenya. Haki hizi si zawadi kutoka kwa serikali, bali ni haki za kuzaliwa za kila Mkenya,” inasema taarifa kutoka kwa shirika hilo.
“Inalenga kulinda utu wa mwanadamu, kukuza haki za kijamii, na kumpa mtu uwezo wa kutimiza uwezo wake. Kwa kuzifunga taasisi zote za serikali, sheria zote na hata watu binafsi, Katiba inaweka mipaka bayana kuhusu jinsi mamlaka ya serikali — ikiwa ni pamoja na urais — yanavyopaswa kutekelezwa.”
Wakili na mwanasiasa Willis Otieno anasema urais kwa sasa “umekuwa tishio kubwa kwa Katiba.”
“Unadhoofisha na kudhihaki taasisi zilizoundwa na Katiba. Angalia juhudi za hivi karibuni za kuingilia mamlaka ya Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), au uteuzi wa washauri wa rais ilhali baraza la mawaziri ndilo lenye mamlaka hayo.”
Profesa Gitile Naituli wa Chuo Kikuu cha Multimedia anasema Katiba ya 2010 iliundwa mahsusi kuvunja mfumo wa urais uliokuwa juu ya kila kitu, kwa kusambaza mamlaka kwa taasisi imara zaidi.
“Kwa kuanzisha tume huru, Bunge lenye mabaraza mawili, ugatuzi, na kuweka mipaka maalum kwa mamlaka ya rais, waandishi wa Katiba walijaribu kusahihisha miongo ya utawala wa kiimla.”
Kwa mujibu wa Prof Naituli, mabadiliko hayo yamefanikiwa kwa kiwango kikubwa.
“Tofauti na enzi zilizopita, marais wa sasa hawana mamlaka ya juu kabisa kama waliokuwa nayo waliowatangulia. Mahakama huru, miundo ya ugatuzi, na Bunge lililo huru kiasi vimeleta vituo mbadala vya mamlaka.”
Hata hivyo, anaonya kwamba faida hizo si kamilifu:
“Ingawa Katiba ilipunguza nguvu za urais kwa maandishi, utekelezaji wake haujaendana na dhamira. Taasisi za kusawazisha mamlaka bado zinaweza kutekwa kisiasa, huku mitandao ya ufisadi ikifufua tena urais kuwa na nguvu zaidi ya makusudio ya Katiba.”
from Taifa Leo https://ift.tt/Jn7F4aW
via IFTTT