
HATUA ya aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko kuwasilisha malalamishi katika makao makuu ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) baada ya Kenya kubanduliwa kwenye Kombe la Afrika kwa Wachezaji wanaoshiriki Ligi za Nyumbani (CHAN 2024) haikuwa na mashiko yoyote wala haikuwa na uwezo wa kufanikishwa kivyovyote. Kenya ilibanduliwa Ijumaa iliyopita na Kisiwa cha Madagascar 4-3 kupitia mikwaju ya penalti kwenye robo fainali ya CHAN. Hii ni baada ya timu hizo kuagana sare ya 1-1 kwenye muda wa kawaida. Hata hivyo, maswali yameibuka kwa nini bao lililofungwa na mshambulizi Ryan Ogam lilifutiliwa mbali ilhali ukiangalia mfumo wa teknolojia mpya ya VAR lilikuwa halali. Itabidi Sonko na mashabiki wa soka nchini waendelee kumeza mate machungu kwa sababu sheria ya soka inasema mwaamuzi ndiye ana usemi wa mwisho uwanjani. “Hakuna mwanya au uwezekano wowote kuwa rufaa ya Sonko itafaulu au ingefaulu. Unaweza kukata rufaa kuhusu uamuzi wa refa iwapo unahusiana na marufuku ya mechi lakini si goli,” akasema Wakili wa kimataifa wa michezo Raphael Omalla. “Kwa mfano mchezaji anaweza kulishwa kadi nyekundi kwa kumvyoga mwenzake lakini kwa ufasiri wako uone kadi hiyo nyekundu haikufaa. Hapo unaruhusiwa kukata rufaa,” akaongeza. Kwenye malalamishi, Sonko alidai kuwa bao la Ogam kukataliwa na beki mpya wa Gor Mahia Lewis Bandi kunawa mpira ndani ya kijisanduku kisha Madagascar kupewa penalti ni matukio ambayo hayakufaa kabisa. Sonko alitaka matokeo ya mechi hiyo ifutwe kisha iamrishe irudiwe ingawa hiyo haiwezekani kwa sababu Madagascar Jumanne ilivaana na Sudan kwenye nusu fainali uwanjani Benjamin Mkapa Dar es Salaam. Kuelekea bao la Ogam fowadi wa Gor Mahia Ben Stanley aliadhibiwa kwa kumsukuma beki wa Madagascar kabla ya kuwahi mpira kwa kichwa na ukafikia Ogam. Tukio la Bandi japo halijaibua mjadala lakini Sonko alikuwa akisema jinsi alivyozuia mpira huo, hakuunawa akikusudia. Sheria za CHAN zinasema kuwa ni afisa wa Shirikisho la Soka Nchini (FKF) ama mwanachama wa Baraza Kuu (NEC) ndiye anaweza kuwasilisha rufaa kwa CAF. Sonko si mwanachama wa FKF wala si NEC na rufaa yake haiwezi kusikizwa kuhusiana na matokeo hayo. “Ni FKF ndiyo iliwasilisha kikosi cha Stars kwenye CHAN wala si Sonko. Kwa hivyo kama ni malalamishi basi yanastahili kutoka kwa shirikisho,” akasema Omalla akisisitiza kwamba Sonko angeishinikiza FKF kukata rufaa. Aliongeza kuwa matokeo kwenye mashindano yanayoendelea kama CHAN hayawezi kukatiwa rufaa au kubatilishwa. CAF ikiangazia mechi zilizochezwa hutegemea ripoti ya refa na iwapo atapatikana ana hatia, basi huadhibiwa kama mtu binafsi badala ya matokeo kubatilishwa. Kati ya adhabu hizo ni kutojumuishwa kwenye mashindano yanayofuata, kupokonywa leseni za Fifa au kusimamishwa kabisa kusimamia mechi jinsi alivyofanyiwa refa wa Zambia Janny Sikazwe mnamo 2018. “Kile ambacho Kenya inaweza kufanya ni refa kuwasilisha malalamishi CAF refa aadhibiwe iwapo kutakuwa na ushahidi hakuwajibikia kazi yake ipasavyo. Awali kuna matukio ambapo watu wamewahi kulalamikia mienendo ya refa na malalamishi hayo hayakufika popote,” akasema Omalla. Jagina wa Argentina marehemu Diego Maradona aliwahi kufunga kwa kutumia mkono kwenye robo fainali kati ya Argentina na England katika Kombe la Dunia mnamo 1986. Alifunga bao la pili, bao kali ambalo lilisaidia Argentina kufuzu nusu fainali 2-1 na hatimaye kushinda kombe hilo la dunia.
-IMETAFSIRWA NA CECIL ODONGO
from Taifa Leo https://ift.tt/YGBa8sF
via
IFTTT