Seneta wa zamani aandika barua ndefu akieleza anaacha kazi ya Ruto aliyodumu miezi minane

SENETA wa zamani wa Murang’a Kembi Gitura amejiuzulu wadhifa wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wasimamizi wa Hospitali ya Mafunzo, Rufaa na Utafiti wa Chuo Kikuu cha Kenyatta (KUTRRH) akisema hakubaliani na sera za serikali ya Rais William Ruto.

Kwenye barua ndefu aliyomwandikia Rais, Bw Gitura ambaye pia aliwahi kuwa Naibu wa Spika wa Seneti, hata hivyo alisema utendakazi wa hospitali hiyo uliimarika chini ya uongozi wake wa miezi minane.

“Sijajiuzulu wadhifa wa mwenyekiti wa Bodi ya KUTRRH kwa sababu sina imani kwa taasisi hii ya kitaifa. La hasha. Wakati huu hospitali hii inafanya nzuri ikihudumia sio tu Kenya bali eneo hili. Nimejiuzulu kwa sababu sitaki nionekane au kuhusishwa na serikali ya UDA ambayo siamini sera zake,” akaeleza kwenye hiyo barua ndefu.

Bw Gitura alifichua kuwa alipoteuliwa na Rais Ruto kwa wadhifa huo Desemba 19, 2024, marafiki zake walimsumbua na maswali wakitaka kujua sababu zilizomfanya kukubali uteuzi huo ilhali hakuwa mwanachama wa chama cha United Democratic Alliance (UDA).

“Ni kweli niliwania kiti cha useneta wa Murang’a kwa tiketi ya Jubilee. Lakini niliwaeleza marafiki zangu na wafuasi wangu wa kisiasa kwamba nilikubali uteuzi huo kwa sababu KUTRRH ni taasisi ya kitaifa wala sio ya kisiasa,” akasema huku akisisitiza kuwa aliendesha kampeni kali ya kupinga UDA kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Bw Gitura alibwagwa katika uchaguzi huo na Seneta wa sasa Joe Nyutu aliyewania kiti hicho kwa tiketi ya chama tawala cha UDA.

Hata hivyo, Bw Nyutu sasa amekiasi chama hicho na anaunga mkono sera za chama kipya cha Demcracy for the Citizens’ Party (DCP) kinachoongozwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Bw Gitura, ambaye pia amewahi kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Usambazaji wa Dawa Nchini (KEMSA) amejiuzulu wakati ambapo sekta ya afya inakumbwa na sakata ambapo baadhi ya hospitali zimekuwa zikiwasilisha madai bandia ya malipo kwa Mamlaka ya Afya ya Kijamii (SHA).



from Taifa Leo https://ift.tt/5jRQ6Lr
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post