VIONGOZI wakuu wa kisiasa wanaomezea mate urais mwaka wa 2027 wanatumia mamia ya mamilioni ya pesa kutafuta ushawishi na msaada kutoka Amerika, ili kuimarisha nafasi zao katika uchaguzi huo, kwa mujibu wa stakabadhi ambazo Taifa Leo imepata.
Kampuni za ushawishi wa kisiasa zinazoendeshwa na watu wa karibu wa Rais wa Amerika Donald Trump, zimekuwa maarufu miongoni mwa Rais William Ruto na viongozi wa upinzani, ambao wanaamini kuwa uhusiano wa karibu na Amerika unaweza kuwa na athari kubwa katika matokeo ya uchaguzi wa 2027.
Huku Rais Ruto akijaribu kurekebisha uhusiano unaotishia kuvunjika na serikali ya Trump, wapinzani wake wanatumia mbinu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kutumia fedha nyingi, ili kujihakikishia uungwaji mkono kutoka Amerika kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027.
Kihistoria, Amerika na mataifa mengine ya Ulaya yamekuwa yakijihusisha na siasa za Kenya kwa kutoa ufadhili kwa wagombea na vyama vya kisiasa.
Serikali ya Rais Ruto, mfanyabiashara Jimi Wanjigi, na aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i ni miongoni mwa wale ambao wameingia mikataba rasmi na kampuni za ushawishi wa kisiasa za Amerika ili kuimarisha uhusiano wao na serikali ya Trump.
Watu hao wameingia mikataba hiyo kwa mujibu wa sheria ya Amerika inayojulikana kama Foreign Agents Registration Act (FARA), ambayo inahitaji mawakala wa kigeni kuripoti shughuli zao kwa serikali ya Amerika ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kinyang’anyiro cha urais 2027.
Serikali ya Rais wa zamani Uhuru Kenyatta pia iliwahi kushirikiana na kampuni kama hizo mara tatu, ikiwemo wakati wa kampeni za uchaguzi wa marudio mwaka 2017.
Viongozi wa upinzani kama Raila Odinga pia waliwahi kuajiri kampuni za Amerika ili kuboresha taswira zao kisiasa na kusaidia shughuli za kuchangisha fedha za kampeni.
Msukumo huu wa kisiasa wa kutafuta uungwaji mkono kutoka Amerika unachochewa na mvutano wa kisiasa ulimwenguni kati ya Amerika na China katika enzi mpya ya ushindani wa mataifa yenye ushawishi mkubwa duniani.
Amerika, ambayo inajaribu kudhibiti upanuzi wa ushawishi wa China barani Afrika, inawatafuta viongozi wa Afrika wanaotaka kuimarisha ushirikiano wa karibu ili kuendeleza ushawishi wake ulimwenguni na kulinda mfumo wa dunia unaoipendelea.
Awamu ya kwanza ya utawala wa Trump imepelekea kuongezeka kwa harakati za ushawishi kutoka kwa nchi na viongozi mbalimbali wanaojaribu kuelewa misimamo ya kisiasa ya Amerika ambayo mara nyingi imekuwa ikibadilika.
Mfanyabiashara Jimi Wanjigi alifanya mkataba na kampuni ya Arsenal Government and Public Affairs Group, inayoongozwa na mshauri wa kisiasa Christopher John Neiweem, katika juhudi za kufikia Rais Trump kupitia makubaliano yaliyofanyika mnamo Januari 17, 2025.
Kampuni hiyo pia imewahi kuajiriwa na wanasiasa wa upinzani nchini Sudan Kusini katika jitihada za kuvutia msaada wa utawala wa Trump.
Kwa mujibu wa stakabadhi, kampuni hiyo huhusika na kampeni za ushawishi zinazolenga marais kwa ada ya Sh135.6 milioni kila baada ya miezi sita.
Ada hiyo inaweza kubadilishwa kwa makubaliano ya pande zote.
"Bw Wanjigi ni mwanasiasa wa zamani nchini Kenya na ana nia ya kuwania urais mwaka wa 2027. Jukumu langu ni kuwasilisha misimamo yake ya sera kwa watunga sera wa Amerika ili kupata uungwaji mkono kwa azma yake, pamoja na kujadili jinsi sera za Kenya zinaweza kuunga mkono maslahi ya serikali ya Amerika,” mkataba huo unaeleza.
Dkt Matiang’i naye ameajiri kampuni ya Dickens & Madson Canada Inc, ambayo imepokea malipo ya awali ya Sh8.4 milioni, huku kiasi cha Sh32.3 milioni kikitarajiwa kulipwa baadaye.
Kwa mujibu wa mkataba huo wa Julai 2024, kampuni hiyo italenga kushawishi serikali ya Amerika kumuunga mkono Matiang’i kuwania urais kwa kutumia mikakati ya kisiasa, mahusiano ya umma na ushawishi wa sera.
Mwaka wa 2017, utawala wa Rais Uhuru Kenyatta uliingia mikataba miwili tofauti na kampuni ya Amerika ya Sonoran Policy Group, ukilipa zaidi ya Sh77 milioni kwa kazi ya kushawishi serikali ya Amerika kuboresha ushirikiano wa kibiashara, uwekezaji na utalii kupitia ubalozi wa Kenya.
Mwaka wa 2019, serikali hiyo iliongeza mkataba mwingine na kampuni hiyo hiyo kwa Sh155 milioni kwa mwaka ili kusaidia kupanga mikutano ya maafisa wa Kenya na viongozi wa Amerika.
Katika uchaguzi wa 2017, kiongozi wa ODM Raila Odinga alishirikiana na mashirika mawili: Vanguard Africa – Shirika la kidemokrasia ambalo lilimsaidia kuandaa mikutano Washington DC na viongozi wa Amerika na mashirika yasiyo kuwa ya kiserikali kuhimiza uchaguzi huru na wa haki nchini Kenya na Aristotle International lilihusika na shughuli za kuchangisha fedha kwa muungano wa NASA, ikiwemo kushawishi maafisa wa Amerika kuunga mkono mchakato wa uchaguzi wa haki.
from Taifa Leo https://ift.tt/jrTUsCk
via IFTTT