Mrengo wa upinzani unaongozwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua unapanga kufanya kikao maalum ili kushughulikia mvutano unaoibuka kuhusu mgombea urais huku shinikizo zikiongezeka utaje mgombea urais wa pamoja katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Taifa Leo pia imebaini kuwa kikao hicho kitawezesha viongozi wa upinzani kuchagua jina la muungano wao, kulingana na mapendekezo yaliyowasilishwa na kamati ya kiufundi.
Majina yaliyopendekezwa kwa muungano huo ni: Muungano wa Ukombozi, Komboa Kenya Alliance, Liberation Alliance Movement, na Mageuzi Coalition.
“Kamati iliwashauri viongozi waidhinishe jina la muungano na pia viongozi rasmi, ili shughuli za muungano zianze rasmi,” chanzo kutoka kamati hiyo kilisema.
Pia, ilibainika kuwa timu ya kiufundi ilihitaji mwelekeo wa pamoja kuhusu uchaguzi mdogo ujao, jambo ambalo limefanya kambi hiyo kupanga kikao hicho cha dharura.
Hatua ya Bw Gachagua kutangaza ghafla azma yake ya kuwania urais 2027 imeibua msisimko mkubwa katika ulingo wa siasa, huku wandani wake wakisema ni mbinu ya kuimarisha uungwaji mkono kabla ya uchaguzi mkuu.
Hata hivyo, hatua hiyo imezua wasiwasi kuwa huenda viongozi wa upinzani wakagawanyika kila mmoja akilenga maslahi yake binafsi, hali sawa na iliyikumba muungano wa FORD mwaka 1992, ambapo tamaa ya madaraka ilizima uwezekano wa kumshinda Rais Daniel arap Moi.
Ingawa upinzani unajitambulisha kama “muungano wa pamoja” dhidi ya Rais Ruto, vyanzo vya ndani vinaashiria kuwepo kwa kushukiana, tamaa ya uongozi na ushindani wa ndani, hali inayodhoofisha umoja wao. Hili ndilo suala ambalo kikao kinatarajiwa kusaidia kushughulikia.
Viongozi wanaotarajiwa kuhudhuria kikao hicho ni pamoja na Bw Gachagua, kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka, aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i, kiongozi wa DAP-K Eugene Wamalwa, kiongozi wa chama cha Democratic Party Justin Muturi, na kiongozi wa People’s Liberation Party (PLP), Martha Karua.
Jana, Bw Wamalwa alikanusha madai ya mgawanyiko lakini alithibitisha kuwa kikao hicho “kitafanyika hivi karibuni.”
“Kikao hicho kinahitajika ili tujadiliane kuhusu masuala ya muungano wetu. Tutakutana hivi karibuni,” alisema Bw Wamalwa.
Hili linajiri huku Rais Ruto, anayeshirikiana na kiongozi wa ODM Raila Odinga, wakiongeza mashambulizi ya kisiasa, hali inayoongeza presha kwa kambi ya upinzani kuweka mambo yao sawa la sivyo wapoteze umaarufu kuelekea 2027.
Ingawa kuna sura ya umoja hadharani, mapambano ya ndani kwa ndani tayari yameanza miongoni mwa viongozi wakuu wa muungano huo.
Tofauti kubwa ni kati ya Bw Uhuru Kenyatta (Jubilee) na Bw Gachagua (DCP) kuhusu nani anayefaa kupeperusha bendera ya urais ya upinzani.
Ingawa wote wawili wanazungumzia umoja na nia ya kuondoa utawala wa Ruto, vyanzo vya ndani vinaeleza kuwepo kwa mfarakano mkubwa kuhusu mgombea wa urais.
Kiini cha mzozo huu ni ushindani mkali kati ya Fred Matiang’i na Kalonzo Musyoka, huku Bw Gachagua naye akitoa matamshi makali kuhusu nia yake ya kuwania.
Inadaiwa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta anamuunga mkono Matiang’i, na huenda mkutano ujao wa wajumbe wa chama cha Jubilee ukamkabidhi uongozi wa chama hicho.
Mgogoro huo ulidhihirika hadharani pale Wakili Ndegwa Njiru, mshirika wa karibu wa Gachagua, alipodai kuwa “Matiang’i ni mradi wa serikali na amesukumwa na NIS.”
Dkt Matiang’i amepuuzilia mbali madai kuwa mradi wa mtu yeyote.
“Kwa nini hamsemi mimi ni mradi wa Benki ya Dunia ilhali nimetoka huko tu?” alihoji katika mahojiano ya runinga.
Mbunge wa Gatanga Edward Muriu, mshirika wa Gachagua, alisema tangazo la Gachagua kuhusu urais halimaanishi mgawanyiko, bali ni mbinu ya kisiasa kuimarisha uungwaji mkono Mlima Kenya.
“Watu hawawezi kukuunga mkono kama hujawaambia ndoto zako. Lazima aseme anawania urais ili kuvutia ngome yake,” alisema Bw Muriu.
Naibu Gavana wa Machakos Francis Mwangangi alisema mkakati wa upinzani ni kujenga nguvu za wakuu wa kanda kabla ya kuchagua mgombea mmoja wa kitaifa.
Seneta wa Kitui Enock Wambua alionya kuwa upinzani lazima uungane:
“Hii si kuhusu jeuri au tamaa ya madaraka, bali ni mapambano ya mamilioni ya Wakenya waliokata tamaa na utawala wa Ruto. Hatutakubali mtu yeyote kuharibu fursa hii kwa sababu ya maslahi ya binafsi,” alisema.
“Ni sawa kwa Gachagua au yeyote kutangaza nia ya kuwania urais, lakini wakati ukifika (na ni hivi karibuni), uamuzi wa pamoja utafanyika kuchagua anayefaa zaidi,” alisema.
from Taifa Leo https://ift.tt/sGz5WYK
via IFTTT