Kudumisha usalama Kaunti ya Kilifi ni sawa na polisi kukimbiza kivuli katika nyika. Mbuga kubwa zenye msitu, kutoka Chakama hadi mipaka ya Hifadhi ya Taifa ya Tsavo Mashariki, zinatoa makazi kwa mitandao ya uhalifu, wawindaji haramu, na vikundi vya mafunzo hatari ya kidini.
Katika hali ngumu hii, viongozi wa makundi potofu kama Paul Mackenzie na hivi karibuni Sharlyne Anindo Temba wamefanikiwa kwa kutumia ukubwa wa eneo hilo na umasikimi wa watu wanaoamini kuwa serikali imewatelekeza.
Kugunduliwa kwa makaburi ya pamoja Shakahola mwaka 2023 na kufukuliwa kwa miili Kwa Bi Nzaro mwaka huu kunaibua tena swali: kwa nini maafa Kilifi yanarudiarudia licha ya hasira kitaifa na ukaguzi mkali wa serikali? Majibu yanayoibuka ni mchanganyiko kuhusu eneo, umaskini, udhibiti dhaifu, na imani ndogo kati ya wananchi na maafisa wa usalama.
Chakama Ranch pekee ina ekari 52,000 za msitu mkubwa. Ni eneo lililojaa njia za ndovu, na nyayo za wanyama hatari kuingia ndani ya Tsavo Mashariki. Maafisa wa usalama wanasema ni vigumu kupiga doria eneo hili. Bila barabara nzuri, uangalizi kutoka angani, au vituo vya walinzi wa misitu, makundi yanaweza kufanya shughuli kwa miezi bila kugunduliwa.
“Ardhi hii ni kubwa, ni ngumu kuikagua vizuri. Suluhucbora ni kuwezesha wakazi, watu waweze kulima, kuishi, kutumia ardhi. Jamii inayofanya kazi itatoa usimamizi wa mali asili, msitu uliouachwa hauwezi kufanya hivyo,” alisema Gavana Gideon Mung’aro. Aliongeza kuwa bila mipango wazi, “kila janga hapa litakuwa ni nakala ya lile la awali, lakini mbaya zaidi.”
Lakini hadi maono hayo yatimie, msitu unabaki mahali pazuri pa kujificha. Hata Shakahola, polisi walipata makaburi baada ya watu kutoa taarifa za siri. Kabla ya serikali kuingilia kati, wengi walikuwa wameangamia
Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha Kilifi ni mojawapo ya kaunti maskini sana Kenya, kwa kiwango cha umaskini cha asilimia 61 kulingana na Ripoti ya Umaskini 2024. Hali hii inasaidia kuelewa jinsi makundi ya dini yasiyo rasmi yanavyopata nguvu na kwa nini ni vigumu kuingilia kati.
Ukosefu wa huduma msingi kama barabara, maji safi, umeme ni kawaida kila siku kwa vijiji vingi. Kwa watu wa Kwa Bi Nzaro, serikali kutowajali ni jambo la kawaida.
“Tunataka hati za mashamba, maji, barabara na umeme. Badala yake, tunajulikana kwa makundi ya kidini na watu kupotea,” alisema David Karisa, mkazi wa eneo hilo.
Viongozi wa makundi hayo wanavutia familia zinazohitaji. Wanatoa ahadi ya uponyaji, chakula, hata wokovu. Kwa watu wasio na matumaini, Imani potofu wanayoangukia inakuwa njia ya kuwaangamiza
Serikali imeshindwa kudhibiti kabisa makundi haya hatari ya kidini. Baada ya Shakahola serikali iliahidi udhibiti mkali, lakini Kwa Bi Nzaro inaashiria kwamba mengi hayajabadilika.
Sharlyne Anindo Temba, anayechukuliwa kuwa mfuasi wa Mackenzie, alianzisha makazi yake Chakama Ranch kimya kimya na kukusanya wafuasi.
Huenda kikwazo kikubwa ni kutokuwepo kwa Imani na maafisa wa usalama. Kwa Bi Nzaro, watu watatu Gona Charo, Karisa Gona, na mzee Safari Kenga—walitoa siri ya kundi hilo lakini badala ya kutambuliwa, walikamatwa na kulaumiwa.
“Ukikamata waliofichua maovu , wengine wataogopa kusema chochote,” alisema Gavana Mung’aro.
from Taifa Leo https://ift.tt/ZBbjFHT
via IFTTT