Sheria mpya ilivyofungulia wakulima wa chai mabilioni yaliyokwama benki

Serikali ilitumia kanuni mpya za Bima ya Amana kwa Akaunti za Wadhamini kuruhusu Sh2.65 bilioni kulipwa wakulima wa chai walio chini ya Shirika la Maendeleo ya Chai Nchini (KTDA), fedha ambazo zilikuwa zimekwama kwa zaidi ya miaka tisa katika benki mbili zilizoporomoka — Chase Bank na Imperial Bank.

Malipo hayo yalitangazwa na Rais William Ruto mnamo Septemba 11, 2025, katika Ikulu ya Nairobi, kufuatia juhudi za ndani ya serikali, ikiwemo maamuzi ya kisera kutoka Ikulu na ushauri wa kisheria kutoka kwa Mwanasheria Mkuu. Serikali ilitumia Kanuni za Bima ya Amana kwa Akaunti za Wadhamini (2025), zilizopitishwa mwezi Julai, kuidhinisha malipo hayo.

KTDA ilikuwa imeweka Sh1.9 bilioni katika Chase Bank na Sh2.9 bilioni katika Imperial Bank kabla ya taasisi hizo za kifedha kufungwa kwa tuhuma za usimamizi mbaya na ubadhirifu. Katika miaka ya awali, KTDA ilifanikiwa kurejesha Sh1.7 bilioni kupitia hatua za ufilisi, lakini kiasi kilichosalia kilikuwa kimekwama kwa kukosa msingi wa kisheria wa kuwalipa wakulima chini ya akaunti ya shirika.

Shirika la Bima ya Amana Kenya (KDIC) hulipa fidia kwa akaunti za wadhamini pale tu ambapo taasisi ya kifedha imewekwa chini ya ufilisi na Benki Kuu ya Kenya (CBK). Malipo hayo hufuata kiwango cha juu kilichowekwa cha Sh500,000 kwa kila mdai, si kwa kila akaunti ya wadhamini.

KDIC imethibitisha kuwa malipo kwa wakulima wa chai wa KTDA yalifanyika chini ya Kanuni za Bima ya Amana kwa Akaunti za Wadhamini za Kenya (2025) zilizopitishwa Julai mwaka huu.

“Tuna kile kinachoitwa akaunti ya wadhamini. Mtu anapofungua akaunti kama mdhamini, anapaswa kuonyesha kwenye rekodi za benki kuwa fedha hizo si zake binafsi bali anazishikilia kwa niaba ya watu wengine. Benki hufungua akaunti hiyo kwa kutambua kuwa si mdai mmoja tu aliyehusika,” alisema Afisa Mkuu Mtendaji wa KDIC, Bi Hellen Chepkwony, katika mahojiano.

Alifafanua kuwa Shirika la Maendeleo ya Chai Nchini (KTDA) ni la wakulima na lilikuwa linashikilia fedha hizo kwa niaba yao.

“KTDA ni wakala. Wanashikilia fedha kwa niaba ya wakulima. Kwenye akaunti ya KTDA kulikuwa na takriban wakulima 591,923 waliokuwa na fedha humo. Tuna orodha yao na kiasi cha fedha walichokuwa nacho. Kwa hivyo tulichokifanya ni kutambua kila mmoja wao kama mnufaika halisi wa fedha hizo,” aliongeza.

Bi Chepkwony alisema kuwa malipo ya KTDA hayakuwa ya kipekee, kwani wadai wengine waliokuwa na salio la hadi Sh500,000 tayari walikuwa wamelipwa kikamilifu, na kufanikisha jumla ya fidia ya hadi asilimia 90 ya madai yote kutoka benki zilizofilisika.

Kwa mujibu wa kanuni mpya, akaunti za wadhamini zinapaswa kutambuliwa kama hazimilikiwi na mtu mmoja bali na watu au mashirika kwa niaba ya wengine. Hii inaruhusu KDIC kulipa fidia ya hadi Sh500,000 kwa kila mdau anayetambuliwa katika akaunti hiyo.

Bi Chepkwony alifafanua kuwa hadi sasa, asilimia 90 ya walioathirika na kufungwa kwa benki hizo wamelipwa fidia kikamilifu. KTDA ilikuwa miongoni mwa wa mwisho kulipwa, kutokana na ukubwa wa madai na hitaji la uthibitisho wa kisheria kuwa ilikuwa mdhamini halali.

“Tulichambua rekodi zao, tukathibitisha walikuwa wadhamini. Hilo ndilo lilifungua mlango wa malipo haya baada ya miaka tisa ya kusubiri,” aliongeza.

Bi Chepkwony alisema KDIC inalinda masilahi ya wawekaji pesa na imejitolea kuhakikisha hakuna mdai anapoteza fedha kiholela endapo benki itafilisika.



from Taifa Leo https://ift.tt/AGaSksC
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post