Kazi ya Ruto ni kubomoa, asema Uhuru

Rais mstaafu Uhuru Kenyatta jana alivunja kimya chake kisiasa cha miaka mitatu kwa kumlaumu vikali Rais William Ruto na serikali yake, akitangaza mbele ya mkutano wa wajumbe wa chama cha Jubilee kuwa Wakenya wamethibitishwa kuhusu onyo alilowapa kuhusu aliyekuwa naibu wake. Bw Kenyatta, ambaye alijiondoa kutoka  siasa baada ya kumkabidhi madaraka Rais Ruto mwaka 2022, alitumia mkutano huo kuwakumbusha Wakenya kuwa aliwaonya wasimpe urais mtu aliyekuwa ameonyesha dalili za kuwagawanya na kusaka maslahi ya  kibinafsi. Alitaja kusahaulika kwa kampeni ya hasla muda mfupi baada ya uchaguzi, changamoto za kiuchumi zilizochochea maandamano nchini kote, na kile alichoita usaliti wa kanuni za kidemokrasia kama ushahidi  kwamba onyo lake halikuwa kwa sababu ya mgogoro  wakibinafsi, bali utabiri wa mtu aliyefanya kazi na Ruto. Ilikuwa mara ya kwanza tangu alipoondoka madarakani kumkabili moja kwa moja. Alilinganisha mpango wake wa kitaifa wa Linda Mama wa huduma za uzazi na mpango wa sasa wa serikali wa Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA), akitaja SHA kama mradi ulioanzishwa haraka bila kuhakikisha kinga za usalama. “Tulihakikisha mama wajawazito wanazaa kwa heshima bila mzigo wa gharama za hospitali,” alisema, akirejelea mpango wa serikali yake wa kueneza huduma za uzazi. “Leo tunasikia kuhusu mifumo mipya, isiyothibitishwa na isiyopangwa, inayowaadhibu wananchi ambao wanadaiwa kulindwa.” Hatua yake ya kukosoa  SHA ilikuwa ni pigo kubwa kwa ajenda ya mabadiliko ya huduma za afya ya Rais Ruto, ambayo imekumbwa na changamoto za kisheria na mkanganyiko katika utekelezaji wake. Bw Kenyatta alizidi kuwakumbusha Wakenya kuwa aliwaonya dhidi ya kuchagua Ruto kwa sababu ya hadithi yake hasla kuhusu maisha yake binafsi. “Niliwaambia kuwa uongozi sio kuhusu mtu alizaliwa wapi, wala mama yake alikuwa nani. Uongozi ni kuhusu uadilifu, maono, na huduma kwa watu,” alisema, akimlenga Rais Ruto na kauli zake maarufu zilizomfanya aingie Ikulu. Alikosoa pia ajenda ya elimu ya Rais Ruto, akilinganisha upanuzi wa elimu ya bure na kurejeshwa kwa heshima ya mitihani chini ya Jubilee na kile alichokiita kuondoa ahadi za kikatiba. “Tulilinda elimu ya msingi bila malipo, kuwa na shule za upili za bure za mchana, na kupunguza mzigo kwa wazazi,” alisema Kenyatta. Maneno yake yalijiri wakati serikali imekubali kukosa fedha za kufadhili elimu ya msingi bila malipo kikamilifu, vyuo vikuu vikikumbwa na changamoto za mfumo mpya wa ufadhili, shule zikikosa pesa kwa miezi, na taasisi za elimu ya juu zikikabiliwa na mgogoro wa kifedha unaoacha wahadhiri na wafanyakazi bila mshahara. Katika sehemu kubwa ya hotuba yake, Bw Kenyatta aliendelea kusema alitarajia mrithi wake kuimarisha badala ya kubomoa mipango ya Jubilee, akimlaumu Ruto kwa kubomoa misingi aliyoiweka. “Baada ya kumkabidhi mamlaka ya nchi kwa utulivu na kwa mpangilio, nilitarajia vivyo hivyo kwa nchi yetu,” alisema. “Kwa bahati mbaya, haikufanyika hivyo. Badala ya kujenga na kuboresha tulichokipata, kila kitu tulichokiwekea msingi kimeharibiwa.” Malalamishi yake dhidi ya serikali ya sasa hayakuwa tu kuhusu sera, bali pia kuhusu urithi. Alidai serikali ya Ruto haijashindwa kutoa huduma bali pia kwa makusudi inafuta mafanikio ya muongo mmoja, na kuacha Wakenya kubeba mzigo wa mageuzi yaliyokwama na taasisi zilizoanguka

from Taifa Leo https://ift.tt/A0Nl3aT
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post