
Watu wanaodanganya kuhusu mali wanayomiliki wakati wa kuwasilisha taarifa za mali zao bungeni wakiteuliwa kwa nyadhifa za umma wataweza kufungwa hadi miaka mitano gerezani au kutozwa faini ya Sh5 milioni ikiwa mswada mpya utapitisha kuwa Sheria. Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Utumishi wa Umma (Idhini ya Bunge) wa mwaka 2025 unalenga kuimarisha ukaguzi wa wanaowania nyadhifa za umma ili kuzuia udanganyifu wa mali unaofanywa na watu wakati wa kuwasilisha taarifa zao bungeni. Kwa mujibu wa uswada huo, anayetoa taarifa za uongo kuhusu mapato, mali au madeni atatozwa faini isiyozidi Sh5 milioni au kifungo cha hadi miaka mitano gerezani au zote mbili. Mswada unaeleza kwamba wanaotaka nyadhifa za umma watatakiwa kuwasilisha taarifa sahihi za mapato yao, mali na madeni, ikiwa ni pamoja na ripoti za mthamini na vyeti vya mhasibu kuthibitisha taarifa hizo. Hii ni hatua muhimu inayolenga kuziba mapengo ya sheria zilizopo ambazo hazihitaji mtu kutoa taarifa sahihi, na hivyo kuwezesha baadhi yao kujaribu kuonekana wenye mali zaidi au chini ya hali halisi. Mbunge wa Funyula, Dkt Wilberforce Oundo, alitaka serikali na wabunge kuhakikisha mswada huu unapitishwa haraka ili kukomesha tabia ya kudanganya wakati wa kupigwa msasa bungeni. “Watu wanaendelea kudanganya wakihojiwa na Bunge, wanazidi kutoa taarifa za uongo ili kuweka mazingira ya kuiba mali ya umma wanapoingia madarakani,” alisema Dkt Oundo. Mswada huu pia unasisitiza kuwa wahasibu na wathamini watakaobainika kutoa vyeti vya udanganyifu watakabiliwa na adhabu kali kisheria, ikiwemo kufunguliwa mashtaka ya hujuma na rushwa. Kwa sasa, ni Katibu wa Bunge anayeomba taarifa kutoka taasisi mbalimbali kuhusu wanaoteuliwa kwa nyadhifa tofauti za umma, na kamati husika ya Bunge hutumia taarifa hizo kuchunguza maadili na masuala mengine ya wateule. Hata hivyo, tatizo kuu limekuwa ukosefu wa ushahidi wa kutosha unaothibitisha mali halisi ya wanaoteuliwa, jambo linaloruhusu baadhi yao kujionyesha kuwa matajiri wakubwa bila kuonyesha nyaraka za kuthibitisha. Mswada huu unalenga kudhibiti hali hii kwa kuwahimiza wanaoteuliwa kuwasilisha stakabadhi rasmi za wathamini wa mali yao pamoja na vyeti vya mhasibu, ili kuwa nauwazi kamili kuhusu hali zao za kifedha. Kwa mujibu wa mswada huo, wanaoteuliwa pia watahitajika kutoa taarifa kuhusu mapato yanayotarajiwa katika siku zijazo, mikataba isiyokamilika, na hata ahadi za kimikataba ambazo zinaweza kuathiri hali yao ya kifedha. Kwa upande mwingine, mswada unataka wanaoteuliwa kufichua mikataba na shughuli wanazojihusisha nazo nje ya majukumu yao ya kazi, ili kuepuka migongano ya maslahi na kuwajibika kikamilifu. Dkt Oundo aliongeza kwamba kuboreshwa kwa sheria hii kutasaidia pia kupunguza visa vya ufisadi na wizi wa mali za umma, jambo ambalo limekuwa likiwakumba viongozi wa serikali kwa muda mrefu. “Ukweli ni kwamba, bila uwazi na uwajibikaji, inakuwa rahisi kwa baadhi ya viongozi kuingiza mikono katika rasilmali za umma kwa lengo la kujihakikishia faida binafsi,” alisema. Kwa sasa, sheria ya Utumishi wa Umma (Idhini ya Bunge) ya mwaka 2011 ndiyo inatumika katika kuendesha mchakato wa kupiga msasa wanaoteuliwa kuhudumu serikalini, lakini sehemu nyingi za sheria hiyo zimeonyesha upungufu mkubwa hasa katika ukaguzi wa mali na maadili. Hivi sasa, kipindi cha ukaguzi kimeongezwa kutoka siku 14 hadi siku 28, lakini juhudi za kuleta mabadiliko ya kina zinaendelea katika Bunge. Hii ni kwa lengo la kuhakikisha wanaoteuliwa wanafuata vigezo vyote vya kisheria na kimaadili kabla ya kuidhinishwa kushikilia nyadhifa mbalimbali za umma.
from Taifa Leo https://ift.tt/M6hR85e
via
IFTTT