Maiti za watu ni mlo wa mbwa nchini Haiti

Katika nchi ya Haiti ambapo polisi wa Kenya wametumwa kukabili magenge raia wamezoea miili ya watu kutafunwa na mbwa katika mitaa wanayoishi.

Katika mtaa mmoja wa jiji la Port-au-Prince, Haiti, mwili wa mtu aliyekufa ulikuwa umetupwa barabarani. Haukuwa umefunikwa na hakuna aliyeshughulika kuuondoa. Mbwa walikuwa wanaumega vipande vipande, huku wakazi wakipita bila kushtuka – hali ambayo, kwa wageni, ni ya kutisha, lakini kwa wenyeji, ni kawaida.

Hii si hadithi ya sinema ya kutisha. Ni ukweli mchungu wa maisha katika taifa ambalo limekumbwa na uhalifu wa magenge. Na mwili huo, kwa mujibu wa walinzi wa amani walioko nchini humo, haukuachwa hapo kwa bahati mbaya. Ulikuwa umeachwa kwa makusudi – kwa maagizo ya magenge ya wahalifu – kama ujumbe wa hofu na mamlaka kwa wakazi wa maeneo hayo.

“Hakuna anayegusa mwili hadi viongozi wa magenge waruhusu,” alieleza afisa mmoja wa kikosi chakinachoongozwa na Kenya. “Kama wamesema usiondolewe, unabaki pale, hata kama unaoza na kuliwa na mbwa.”

Katika mitaa kama Delmas na Carrefour Feuilles, ambapo kiongozi hatari wa genge, Jimmy Cherizier almaarufu Barbecue, anajulikana sana, hali ni mbaya. Ingawa maafisa kikosi kinachoongozwa na Kenya vimefanikiwa kutwaa maeneo kadhaa, bado baadhi ya sehemu zimesalia kuwa chini ya utawala wa magenge.

Hivi ndivyo Haiti ilivyo: taifa ambalo serikali yake haidhibiti kila kipande cha ardhi yake, ambapo raia wamesalia kuwa waathiriwa wa mashambulishi ya kila siku, kuanzia ubakaji, mauaji, wizi wa mabavu hadi kutekwa.

Taarifa zinaonyesha kuwa zaidi ya watu milioni moja wamelazimika kukimbia makazi yao kutokana na ukatili wa magenge. Maiti nyingi haziokotwi na haziwekwi katika mochari yoyote. Zinatumiwa kama silaha ya kisaikolojia ujumbe wa magenge kwa jamii: 'Hatuogopi, tunatawala, na hakuna wa kutugusa.'

Katika safari ya waandishi wa Taifa Jumapili walioungana na vikosi vya usalama, walioshuhudia mwili huo ukiliwa na mbwa wakipita, waliporudi kupitia njia hiyo baada ya saa kadhaa na bado ulikuwa pale, ukiendelea kutafunwa.

Kenya, chini ya Umoja wa Mataifa, inaongoza kikosi cha kupambana na magenge nchini Haiti. Vikosi vyake vimefanikiwa kufungua bandari, kurejesha makao makuu ya polisi, na kufungua baadhi ya shule na biashara.

Lakini changamoto ni nyingi huku Rais William Ruto akisema kikosi hicho kimekuwa kikifanya kazi kwa asilimia 40 tu ya uwezo wake, huku vifaa muhimu kama magari ya kivita yakiwa chakavu au yakivunjika katikati ya operesheni.

Maafisa watatu wa polisi wa Kenya tayari wamepoteza maisha. Koplo Kennedy Nzuve, Samuel Kaetuai, na Benedict Kabiru ni baadhi ya waliouawa kwenye operesheni nchini humo.

Haiti haina huduma ya hifadhi ya maiti wala wataalamu wa uchunguzi wa vifo. Miili inapelekwa Jamhuri ya Dominica kwa uchunguzi kabla ya kurudishwa Kenya. mchakato unaochukua muda mrefu.

Katika hotuba yake kwenye mkutano wa 80 wa Umoja wa Mataifa (UNGA), Rais Ruto alisema:Watu wa Haiti ni wa asili ya Kiafrika, lakini wao ni binadamu kama sisi. Wanastahili heshima, usalama, na msaada – sio matusi na kupuuzwa.”

Ingawa sehemu za jiji kama Petion-Ville bado zinaonekana kuwa tulivu zikiwa na mabalozi na mashirika ya kimataifa – maeneo mengine yamekuwa vituo vya mateso ya kila siku. Barabara ni nyembamba, magari ya kivita yanashindana na magari mabovu ya abiria, huku wananchi wakijaribu kuuza bidhaa pembeni mwa barabara zilizojaa damu na hofu.

Kwa maafisa wa Kenya walioko huko, maisha ni tahadhari ya juu kila wakati. Lakini hata katikati ya hayo, wameweza kuanzisha mazoezi ya viungo, mpira wa miguu, na mazoezi ya kijeshi, ili kujenga mshikamano na kupunguza mzigo wa kisaikolojia.



from Taifa Leo https://ift.tt/D2iPGdC
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post