Washirika wa Ruto wamchemkia Uhuru, waponda kwa kukosa serikali

Washirika wa Rais William Ruto, jana walimjibu kwa hasira Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta kufuatia matamshi yake ya kuikosoa serikali ya Kenya Kwanza, wakimuonya kwamba kurejea kwake kwenye siasa kunaweza kumfanya apoteze marupurupu ya uzeeni anayolipwa na serikali.

Wabunge wanaomuunga mkono Rais Ruto walipuuza madai ya Bw Kenyatta kwamba imethibitishwa alikuwa sahihi kuhusu uongozi wa Ruto, wakisisitiza kuwa serikali ya sasa imeimarisha uchumi na kuboresha huduma kwa wananchi.

“Tulipitisha mswada unaompa rais mstaafu marupurupu. Ikiwa Uhuru ataendelea na anachofanya, tutafuta hayo marupurupu,” alisema Seneta wa Nandi, Samson Cherargei. “Alileta maendeleo yasiyo na usawa nchini.”

Kwa mujibu wa Sheria ya Marupurupu ya Marais Wastaafu ya 2003, rais mstaafu anastahili malipo ya Sh39.6 milioni, pensheni ya kila mwezi ya Sh1.32 milioni, pamoja na magari, ofisi, burudani, na bima ya afya. Hata hivyo, sheria hiyo inamtaka rais mstaafu kujiuzulu kutoka uongozi wa chama miezi sita baada ya kuondoka mamlakani – sharti ambalo Bw Kenyatta hajatekeleza, akiendelea kuwa kiongozi wa Jubilee na mwenyekiti wa baraza la Azimio.

Kwenye mkutano wa wajumbe wa Jubilee jijini Nairobi, Bw Kenyatta alisema kuwa alikusudia kujiuzulu, lakini kuingiliwa kwa chama chake na serikali kulimlazimu kubaki uongozini.

“Nilikabidhi mamlaka kwa amani. Nilitarajia hali kama hiyo kwa chama chetu. Lakini walituma watu kuiba chama, nikaamua kubaki,” alisema.

Wandani wa Rais Ruto walionyesha wasiwasi kuhusu kurejea kwa Bw Kenyatta katika siasa, wakisema huenda Jubilee ikawa kitovu kipya cha upinzani. Wengine walimhusisha moja kwa moja na matatizo ya sasa ya kiuchumi, hasa kupitia mikopo kama Eurobond.

Mbunge wa Nyaribari Chache, Zaheer Jhanda, alisema: “Alishindwa kuwakomboa Wakenya kwa miaka 10. Sasa anamtaka Ruto ashindwe pia? Aliharibu uchumi, na sasa tunarekebisha nchi.”

Mbunge wa Mwala, Vincent Musyoka Kawaya, aliongeza: “Uhuru hawezi kusema tumeharibu urithi wa Jubilee. Bei ya mbolea na unga zimeshuka. Ni urithi upi anazungumzia. Ninapata shida kuelewa ni mafanikio gani yameharibika,” alisema. “Unazungumzia Eurobond ambayo mlikopa na sasa tumeshalipa?”

Naibu Rais Kithure Kindiki alimtaka Kenyatta kutumia hoja, si propaganda, kukosoa serikali. “Mpango wa Linda Mama ulikuwa wa akina mama wajawazito. Lakini sasa huduma za afya kwa wote zinafaidi kila mtu.”

Mbunge wa Kapseret, Oscar Sudi, alimshauri Kenyatta aepuke siasa kabisa. “Kama unataka kumshauri Rais, enda ukamuone. Umezeeka kisiasa. Acha kujifanya msafi. Tunajua ulivyoshindwa kurekebisha HELB na NHIF. Usilete uongozi wa kifamilia hapa.”

Katika hotuba yake yenye maneno mazito, Kenyatta alisema serikali ya sasa imekuwa ikibomoa ustawi ambao utawala wake ulifanikisha na ina njama ya kisiasa ya kumdhalilisha, hali aliyosema imezua migawanyiko miongoni mwa Wakenya. Alidai kuwa Jubilee ilikuwa imeweka misingi thabiti ya maendeleo, lakini mafanikio hayo yanafutwa na serikali ya sasa.

“Hatuwezi kuruhusu nchi yetu irudi nyuma. Tuliweka msingi wa maendeleo kupitia Ajenda Nne Kuu, lakini sasa tumeona mipango hiyo ikipuuzwa. Nina wajibu wa kusimama na kuzungumza,” alisema Kenyatta.

Hotuba yake iliashiria kurejea kwa kishindo katika siasa na ilikuwa na dalili za kufufuliwa kwa chama cha Jubilee, ikiwa ni pamoja na vidokezo kuwa chama hicho kinaweza kuwasimamisha wagombea kote nchini mwaka wa 2027.

Bw Kenyatta alitetea kwa nguvu rekodi ya serikali yake katika sekta ya afya, elimu na miundombinu – jambo lililoonyesha si tu jaribio la kibinafsi la kurejesha heshima ya urithi wake, bali pia jitihada pana za kukipa chama cha Jubilee nafasi ndani ya upinzani. Kwa kutangaza kwamba “haendi popote,” alikusudia kuonyesha kuwa bado ana nafasi ya kudumu katika ulingo wa kisiasa ambapo viongozi wa zamani kwa kawaida hujiondoa na kustaafu.

Katika hatua ya kushangaza, baadhi ya viongozi wa upinzani waliunga mkono kauli ya Kenyatta wakisema kuna haja ya kuwepo kwa sauti mbadala serikalini. Mbunge wa Alego Usonga, Samuel Atandi, alisema: “Uhuru ana kila haki ya kujitetea. Wale wanaomshambulia wanaogopa ukweli.”

Lakini mbunge w Emurua Dikirr MP Yohana Ng’eno alimshambulia vikali Kenyatta, akimhusisha na uovu mkubwa serikalini. “Alifuja pesa za COVID-19. Vijana waliuawa na kutupwa mtoni. Aache unafiki.”

Msaidizi wa kisiasa wa miaka mingi wa Rais Ruto, Farouk Kibet, alitoa onyo kali kwa Kenyatta. “Usituchochee. Tulisubiri miaka 10 uondoke kwa amani. Ukivuka mstari, tuko tayari kukukabili.”

Hasira hizi zinaashiria kuwa mapambano ya kisiasa kati ya Kenyatta na mrithi wake bado hayajaisha, huku siasa za 2027 zikianza kupamba moto.



from Taifa Leo https://ift.tt/uPEaIX6
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post