Ombi la Passaris kwa adhabu zaidi kwa wanaotumia mamlaka kunyanyasa kingono lazimwa

KAMATI ya Bunge la Kitaifa kuhusu maombi ya umma imekataa pendekezo la kuanzisha sheria mpya inayopendekeza adhabu kali dhidi ya watu wanaoshiriki katika visa ambapo watu kutumia mamlaka au ushawishi kuwataka watu kushiriki ngono ili kupata huduma, kazi au rasilmali fulani.

Katika pendekezo hilo, waliohusika wangefungwa miaka 15 jela, kutozwa faini ya Sh5 milioni au adhabu zote mbili. Hata hivyo, kamati hiyo ilikataa ombi hilo kwa misingi kuwa makosa hayo tayari yanashughulikiwa kupitia Sheria ya Makosa ya Kingono na Sheria ya Matumizi Mabaya ya Kompyuta na Uhalifu Mtandaoni ya 2018.

“Kamati haikubali pendekezo la kurekebisha Sheria ya Makosa ya Kingono (Kifungu cha 63A) au sheria nyingine zinazohusika ili kuainisha wazi tabia hii kama kosa, kuweka adhabu maalum au msaada kwa waathiriwa,” inasema ripoti ya kamati.

Tabia hii inaelezewa kama matumizi mabaya ya mamlaka ya mtu kutoa au kunyima huduma, fursa au rasilmali fulani mtu mwingine kwa masharti ya ngono au upendeleo wa kimapenzi.

Kamati ilieleza kuwa vipengele kuhusu tabia hiyo tayari vimo kwenye Kifungu cha 43 cha Sheria ya Makosa ya Kingono, na vinaweza kushughulikiwa chini ya makosa kama unyanyasaji wa kingono, matumizi mabaya ya mamlaka, na kulazimisha kwa hila.

Pia, kamati ilikosoa ombi hilo kwa kushindwa kueleza wazi vipengele ambavyo havijashughulikiwa kwenye sheria zilizopo.“Kamati haikubaini pengo lolote katika sheria zilizopo ambalo linaweza kuhitaji kutungwa kwa sheria mpya,”ripoti inasema.

Pendekezo la marekebisho hayo liliwasilishwa bungeni mwaka jana na Mwakilishi wa Wanawake Kaunti ya Nairobi, Esther Passaris, kwa niaba ya Wakenya waliokuwa na wasiwasi kuhusu ongezeko la visa hivyo.

Bi Passaris alieleza kuwa tabia hiyo ni kikwazo kikubwa kwa usawa wa kijinsia, utawala bora na maendeleo endelevu. Alisema visa vya kushurutishwa kushiriki ngono ili kupata huduma au kazi vimekuwa vikiwaathiri hasa wanawake na wasichana maskini, wasio na elimu, wenye ulemavu, au waliotengwa kisiasa.

Kwa mujibu wa ombi hilo, asilimia 41 ya wanawake wanaoishi mitaa ya mabanda waliripoti kuwa waathiriwa wa tabia hii, huku visa vya 'ngono kupata maji' vikishuhudiwa katika maeneo ya mashambani, hasa Magharibi mwa Kenya.

Wanawake wanasiasa pia wameelezwa kuwa waathiriwa wa mashambulizi ya kidijitali, ambapo picha zao hubadilishwa kwa matusi na matusi ya ngono kwa lengo la kuwaaibisha na kuwaweka katika mazingira ya kudhalilishwa.

Katika mawasilisho yake kwa kamati, Mwanasheria Mkuu alisema kuwa Sheria ya Makosa ya Kingono tayari inatambua ‘sextortion’ kama kosa la kingono, kwa kuwa inalenga tendo lolote la kuomba au kulazimisha ngono kwa kutumia mamlaka au ushawishi.

Kifungu cha 42(1)(a) na 43(2)(c) kinatambua kuwa tendo la kingono ni kosa iwapo linafanyika kwa mazingira ya kulazimishwa, hasa pale ambapo kuna matumizi ya mamlaka.



from Taifa Leo https://ift.tt/ARpOzZ4
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post