SERIKALI haiwezi kuelezea waliko zaidi ya wanafunzi 700,000 waliofanya mtihani wa kidato cha nne (KCSE) mwaka 2024 na kupata kati ya alama ya C mpaka E.
Mkurugenzi Mkuu wa Huduma ya Kutengea nafasi Wanafunzi katika Vyuo Vikuu na Vyuo vya Ufundi (KUCCPS), Dkt Agnes Wahome, alifichua kuwa kati ya wanafunzi 961,144 waliofanya mtihani wa KCSE mwaka jana, waliofuzu kusomea Diploma ni waliopata C- (minus), Cheti cha Kiufundi ni D, wakati kozi za ufundi zinahitaji alama E.
Ili kusomea Diploma ya Sheria ni unahitaji C, Diploma ya Elimu ya Sekondari ni C+ na Diploma ya Elimu ya Walimu wa Msingi ni C.“Tunawajali Wakenya wote bila kuzingatia alama yao kuanzia A mpaka E,” alisema Dkt Wahome.
Dkt Wahome alifafanua kuwa wanafunzi 246,165 waliopata alama C+ na zaidi walistahili kuendelea na masomo ya vyuo vikuu. Wengine 711,389 waliopata alama chini ya C+ walistahili kupewa nafasi za kusomea Diploma, Vyeti, na Ufundi na ila kwa sasa hawajulikani waliko.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na KUCCPS, waliostahili masomo ya digrii (C+ na zaidi) ni kama ifuatavyo: A, 7,728; A- , 1,695; B+ , 19,131; B, 43,103; B- 75,268; C+ , 99,240.
Kwa hivyo, jumla ya waliostahili kujiunga na vyuo vikuu ni 246,165.Dkt Wahome aliongeza kuwa wanafunzi 3,590 walichagua kujaribu baadhi ya masomo waliyofeli, hasa kwa lengo la kujiunga na vyuo vya mafunzo ya matibabu.
Sayansi
“Waligundua walikuwa na alama duni katika somo la Bayolojia au Kemia na hivyo walipojaribu tena, matokeo yao yanajumuishwa kama U. Kutoka kwa wanafunzi 961,144, takriban 246,165 walipata alama C+ na zaidi kujiunga na vyuo vikuu.
Wengine 711,389 waliopata alama kati ya C na E, waliostahili kupewa nafasi kusomea Diploma, Cheti, na Ufundi katika vyuo, haibaini waliko. Hii ni changamoto kubwa kwa kuwa hatujawa na uwezo wa kuwapata,” Dkt Wahome aliambia seneti.
Ufichuzi wa Dkt Wahome umezua wasiwasi mkubwa miongoni mwa wadau, ambapo Kamati ya Elimu ya Seneti iliagiza Wizara ya Elimu kuhakikisha kwamba wanafunzi hao wanapatikana.
“Tunatarajia kuwa kwa Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za Elimu Kenya (KEMIS), tutaweza kuwafuatilia kwa kuwa tunaweza kufuatilia wale walio katika taasisi zinazodhaminiwa na serikali.
Lakini wale wanaoenda vyuo vya kibinafsi kama Ashleys na vinginevyo, hatuna mfumo wa kuwatambua,” alisema Dkt Wahome.Dkt Wahome alisema kwamba wanafunzi wa mwaka 2025/2026, jumla ya wanafunzi 338,955 walituma maombi na kupewa nafasi katika vyuo vikuu na vyuo vya kadri.
“Katika idadi hiyo, 182,241 walipewa nafasi kusomea digrii, 105,757 katika TVET, 38,653 KMTC, 500 Diploma ya Sheria, huku 11,804 wakipewa nafasi katika Vyuo vya Mafunzo ya Walimu,” alisema Wahome.Afisa huyo alisema kwamba wanafunzi 25,000 waliofuzu kusomea digrii walichagua kozi zisizo za shahada katika vyuo na taasisi za TVET.
from Taifa Leo https://ift.tt/SeAiZFV
via IFTTT