Marufuku kupiga picha bandarini baada ya video kuvuja ikionyesha ndege ya kijeshi ya Amerika

MAMLAKA ya Bandari za Kenya (KPA) imeonya wafanyakazi wake na watumiaji wa bandari dhidi ya kupiga picha na kurekodi video ndani ya maeneo ya bandarini.

Hii ni baada ya video ya ndege ya kijeshi ya Amerika iliyokuwa ikitua katika bandari ya Mombasa kusambaa mitandaoni.

Taarifa kwa wafanyakazi wote kutoka kwa Meneja wa Huduma za Usalama wa KPA Tony Kibwana, ilisema kitendo hicho kinakiuka utaratibu wa kimataifa wa kulinda kituo kilicho chini ya ulinzi maalumu.

Arafa hiyo, iliyoandikwa Septemba 22, 2025, ilitolewa saa chache baada ya video ya ndege aina ya Bell Boeing V-22 Osprey bandarini kuenezwa mitandaoni.

“Bandari ya Mombasa na vituo vyote vya bandari chini ya KPA, yakiwemo maghala ya nchi kavu ya mizigo, ni maeneo yanayolindwa, na upigaji picha au video umepigwa marufuku isipokuwa kwa kibali na idhini kutoka kwa usimamizi. Kwa mujibu wa Kanuni za Kimataifa za Usalama wa Meli na Vituo vya Bandari, KPA imeweka mabango ya taarifa na onyo kuhusu upigaji picha na video katika maeneo haya,” alisema Bw Kibwana.

Video hiyo ilizua maswali miongoni mwa umma kuhusu jukumu la ndege hizo bandarini. Kwa mujibu wa duru za kuaminika, ndege kama hizo sita zinatarajiwa kutua kabla ya Septemba 25, kabla ya kupakiwa ndani ya meli ya kivita.

Hata hivyo, bado haijulikani wazi zitakaposafirishwa.

Mnamo Machi mwaka huu, meli ya kijeshi ya USS Lewis B. Puller (ESB-3 ya Amerika pia iliwasili Mombasa.

Taarifa rasmi zilisema kuwa, meli hiyo ilitia nanga Mombasa kwa ajili ya kuongeza vifaa vilivyohitajika na kuimarisha ushirikiano wa kijeshi kati ya Kenya na Amerika.

Meli nyingine kadhaa za kijeshi za Amerika pia zimewahi kutia nanga Mombasa katika miaka iliyopita, ikiwemo USS Hershel “Woody” Williams (ESB-4) mwaka 2021.

Meli hiyo ilipowasili Mombasa Februari 2021, iliashiria ziara ya kwanza ya Jeshi la Wanamaji la Amerika nchini Kenya baada ya zaidi ya muongo mmoja.



from Taifa Leo https://ift.tt/xs3WZGV
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post