ALIYEKUWA Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i, ameashiria kwa mara ya kwanza kuwa, huenda atawania urais kupitia chama cha Jubilee, kinachoongozwa na Rais (mstaafu) Uhuru Kenyatta.
Dkt Matiang’i alitoa ishara hiyo alipohudhuria kikao cha mashauriano na baadhi ya viongozi wa Jubilee kilichofanyika katika hoteli ya Safari Park, jijini Nairobi, mnamo Jumanne.
Kikao hicho kilikuwa maandalizi ya Mkutano Maalum wa Kitaifa wa Wajumbe (NDC) wa chama hicho unaopangwa kufanyika Ijumaa, Septemba 26, 2025.
Kwa mujibu wa vyanzo vya kuaminika, huenda Rais mstaafu Kenyatta akawa anapanga kumkabidhi Dkt Matiang’i uongozi wa chama hicho ili kumwandaa kwa kinyang’anyiro cha urais 2027.
Waliohudhuria kikao hicho ni pamoja na Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni, aliyekuwa gavana wa Kiambu James Nyoro, aliyekuwa Mbunge wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu, na viongozi wengine wa ngazi ya kitaifa.
Bw Kioni alisema kuwa mkutano huo ulikuwa sehemu ya mikakati ya kufufua chama cha Jubilee na kuandaa ajenda mpya kwa uchaguzi mkuu ujao.
“Tulikutana kuimarisha chama, kubadilishana mawazo na kuandaa mwelekeo mpya. Dkt Matiang’i alikuwa miongoni mwa waliochangia mjadala huu muhimu,” alisema Kioni.
Kwa upande wake, Bw Wambugu alisema mkutano huo ni mwanzo wa mikakati ya Jubilee kurejea mamlakani kupitia uchaguzi wa kidemokrasia.
“Kumbuka Dkt Matiang’i alikuwa mtekelezaji mkuu wa manifesto ya Jubilee kwa miaka 10. Mbali na Rais Kenyatta, hakuna anayeelewa Jubilee kuliko yeye,” alisema Wambugu.
Wadadisi wa siasa wanasema kuwa, Mkutano Maalum wa Ijumaa unaweza kutangaza rasmi Dkt Matiang’i kuwa Kiongozi wa Chama cha Jubilee pamoja na mgombea wake wa urais 2027.
Katika taarifa rasmi ya mwaliko kuhusu mkutano huo, Bw Kenyatta alisema wajumbe watajadili marekebisho ya katiba ya chama, sera mpya, na mpango wa kukiimarisha mashinani.
“Tutapokea ripoti ya hali ya chama kutoka kwa Kamati Kuu ya Taifa na kufanya maamuzi muhimu kuhusu uongozi na mustakabali wa Jubilee,” ilisema taarifa hiyo.
Katika mahojiano ya awali, Dkt Matiang’i alithibitisha kuwa bado hajafanya uamuzi kuhusu chama atakachotumia lakini alikuwa akishauriana na vyama mbalimbali.
“Niko katika mashauriano na vyama kadhaa. Siwezi kuchukua hatua mapema kabla ya kusikiliza kila upande,” alisema.
Dkt Matiang’i, ambaye alihudumu katika wizara mbalimbali muhimu serikalini, anaungwa mkono na sehemu kubwa ya viongozi wa zamani wa Jubilee ambao wamekuwa wakilalamikia mwelekeo wa sasa wa serikali ya Kenya Kwanza.
Kulingana na wachambuzi wa siasa, endapo Dkt Matiang’i atachukua usukani rasmi kutoka kwa Kenyatta, atakuwa mpinzani mkuu wa Rais William Ruto katika uchaguzi wa 2027, na huenda akajenga upya upinzani wa kisiasa wenye mtazamo wa kitaifa.
Lakini changamoto kubwa itakuwa ni jinsi atakavyofanikiwa kuunganisha vyama vya upinzani vilivyogawanyika, kurejesha imani ya wapigakura, na kujiweka mbali na siasa za mizozo ya zamani ambazo zimewakera wananchi.
Hata hivyo, kutokana na tajriba yake serikalini, na mtandao wa kitaifa, wengi wanaamini kuwa Dkt Matiang’i ana nafasi ya kuibuka kuwa mhusika mkuu wa kisiasa kuelekea uchaguzi wa 2027.
Kwa mujibu wa azimio la Mkutano Mkuu wa Wajumbe wa Narc-Kenya uliofanyika Novemba 2024, chama hicho kiliafikia kujiondoa rasmi kutoka Azimio.
Hii ni licha ya kuwa Bi Karua ndiye aliyekuwa mgombea mwenza wa Raila Odinga katika uchaguzi wa urais wa mnamo 2022 kupitia muungano huo.
Chama cha Narc-Kenya kinachoongozwa na Martha Karua, ambacho sasa kimebadilisha jina kuwa People’s Liberation Party (PLP), pamoja na Democratic Action Party–Kenya (DAP-K), ni miongoni mwa vyama tanzu vya muungano wa Azimio ambavyo vimeanza rasmi mchakato wa kujiondoa kutoka kwa muungano huo wa upinzani.
Wakati huo huo, chama cha Jubilee, ambacho sasa kinaonekana kuwa katika harakati za kujifufua chini ya uongozi wa Rais (mstaafu) Kenyatta, kinadaiwa kuwa katika mazungumzo ya kuunda muungano mpya na vyama vingine vya upinzani vyenye mwelekeo sawa.
Miongoni mwa vyama hivyo ni pamoja na DAP-K, United Progressive Alliance (UPA), Chama Cha Kazi cha aliyekuwa Waziri Moses Kuria, KANU ya Gideon Moi, na Party of National Unity (PNU) kinachohusishwa na aliyekuwa waziri Peter Munya.
Chama cha UPA, kilichoasisiwa na Gavana wa Nyamira Amos Nyaribo, kimekuwa kikimtangaza Dkt Fred Matiang’i kama chaguo lao la urais kwa uchaguzi mkuu wa 2027.
Seneta wa Kisii, Bw Richard Onyonka, ambaye ni mshirika wa karibu wa Dkt Matiang’i, alifichua kwamba tayari kuna mazungumzo ya kina kuhusu kumpa Dkt Matiang’i uongozi wa chama cha Jubilee pamoja na tiketi ya kugombea urais 2027.
“Ni jambo linalozungumzwa. Tumekubaliana kufanya tathmini ili kuchunguza kwa makini nguvu, udhaifu, fursa na hatari zilizopo kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho,” alisema Seneta Onyonka.
Alikiri kuwa kuna waliotaka Dkt Matiang’i atumie chama cha kikanda kama UPA, lakini wengine wanashinikiza atumie Jubilee kutokana na umaarufu wake wa kitaifa na miundombinu ya chama iliyo tayari.
“Tukiweza kuwa na ndoa ya kisiasa kati ya Jubilee na UPA, itakuwa vyema. Lakini ikiwa Jubilee kupitia Mkutano wa Wajumbe itamuidhinisha Dkt Matiang’i kama kiongozi wa chama, sisi tutakuwa tayari – mradi tu yeye mwenyewe anakubali,” aliongeza.
Katika mahojiano ya awali na Taifa Leo Katibu Mkuu wa Jubilee, Bw Jeremiah Kioni, alibainisha kuwa Dkt Matiang’i tayari anaungwa mkono na watu kutoka pembe zote za nchi, akisema itakuwa ni kamari ya kisiasa kwake kuwania urais kupitia chama cha kikanda kisicho na sura ya kitaifa.
from Taifa Leo https://ift.tt/1nZSabW
via IFTTT