Ruto alitumia uteuzi wa Ruku kuwatega wandani wake Mlima Kenya – Wachanganuzi

RAIS William Ruto alitoa nafasi ya uchaguzi mdogo kufanyika katika eneobunge la Mbeere Kaskazini ili kutathmini ushawishi wa wandani wake katika siasa za Mlima Kenya, wachanganuzi sasa wanaamini. Wanasema Rais Ruto alifahamu fika mtihani uliokuwa ukimsubiri katika shughuli kama hiyo ikizingatiwa kuwa aliteua aliyekuwa mbunge wa eneo hilo Geoffrey Ruku kuwa Waziri wa Utumishi wa Umma mwezi Aprili mwaka huu. “Wakati Rais alipofikia uamuzi huo, hasira zilikuwa zimepanda dhidi ya serikali yake katika eneo la Mlima Kenya. Hii ni baada ya kutimuliwa kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua. Tayari wakazi wa Embu walikuwa wameanza kumkaidi hata waliwahi kumzomea mara mbili tangu kutimuliwa kwa Gachagua Oktoba 18, 2025,” akasema Prof Peter Kagwanja. “Ni katika kaunti hiyo ambako Rais alijipata akigongana na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu na Waziri wa Utumishi wa Umma Justin Muturi,” akaongeza, akirejelea kufutwa kazi kwa Bw Muturi mnamo Machi na jinsi kulivyosababisha uhasama dhidi ya Rais eneo hilo. Kulingana Prof Kagwanja, Dkt Ruto, ambaye hupokea habari za kijasusi kila siku, alifahamu kuwa umaarufu wake na ule wa chama chake cha UDA ulikuwa umeshuka Mlima Kenya ambako alipata asilimia 87 ya kura 2022. “Kwa hivyo, bila shaka Rais aliruhusu kufanyike uchaguzi mdogo eneo hilo kwa lengo la kupima umaarufu wa wandani baada ya kupoteza ufuasi wake,” anasisitiza. Kwa upande wake, mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Embu, Malila Munywoki anasema, “Nilishangaa namna Rais angekuwa na ujasiri kiasi hicho.” “Lazima alikuwa na sababu. Kuna uwezekano alikuwa amepata ukweli fulani kuhusu ushawishi wake, kisiasa, katika eneo hili,” anaeleza. Kwa mtazamo wa Bw Munywoki, uchaguzi mdogo katika eneobunge la Mbeere Kaskazini ni mtihani kwa Naibu wa Rais, Prof Kithure Kindiki, mwenyekiti wa UDA ambaye pia ni Gavana wa Embu, Cecily Mbarire na Bw Ruku miongoni mwa wengine waliounga mkono kutimuliwa kwa Bw Gachagua. Baada ya kutimuliwa kwa Gachagua anayetoka Kaunti ya Nyeri, Dkt Ruto alimteua Prof Kindiki kujaza nafasi hiyo, hatua iliyofasiriwa kulenga kutuliza wakazi wa Mlima Kenya. Hatua hiyo pia ilionekana kama jaribio lake la kujijengea himaya ya kisiasa katika Mlima Kenya Mashariki, eneo linaloshirikisha kaunti za Embu, Meru na Tharaka Nithi, zinazochukuliwa kuwa ngome ya Prof Kindiki. Japo Rais Ruto aliwahi kusema kuwa viongozi wa Mlima Kenya ndio walimshinikiza aruhusu kutimuliwa kwa Gachagua, Bw Munywoki anasema ni wazi kuwa hatua hiyo na hata kuteuliwa kwa Prof Kindiki hakukutimiza malengo yaliyokusudiwa. Badala yake, wakazi wa Mlima Kenya walionekana kumhurumia Bw Gachagua kutokana na masaibu yaliyomfika. Akiongea katika Kaunti ya Murang’a mnamo Septemba 15, Bw Gachagua alisema lengo la Rais lilikuwa kupanga upya siasa za Mlima Kenya na kuwaondoa viongozi wakuu na "kujaza nafasi zao na vikaragosi wake”. “Hii ndiyo sababu ilimfanya kudhamini hoja ya kunitimua, kisha akamwendea Muturi, Waziri wa zamani wa Kilimo Mithika Linturi, Inspekta Jenerali Japhet Koome na wengine wengi,” akasema. “Huu uchaguzi mdogo wa Mbeere Kaskazini ni muhimu na tunapaswa kuupa uzito. Ninawaomba watu wetu kuongozwa na hekima,” Bw Gachagua akasema. Kiongozi huyo wa chama cha Democracy for Citizens Party (DCP) aliwashangaza wafuasi wake alipotangaza kuwa chama hicho hakitashiriki katika uchaguzi huo na badala yake kitaunga mkono mgombeaji atakayedhaminiwa na chama cha Democratic Party (DP), chake Justin Muturi. Hatua hii imekanganya mrengo wa serikali huku Waziri Ruku akilalamika kuwa Gachagua ni “mwoga kwani huzunguka Mlima Kenya akidai ndiye kigogo lakini anafeli kudhamini mgombeaji hapa kuthibitisha ubabe wake”.

from Taifa Leo https://ift.tt/t7ORPjn
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post