
HOSPITALI za kibinafsi ambazo zipo chini ya Muungano wa Hospitali za Mijini na Mashinani (KUPHA) zimetangaza kuwa hazitawatibu walimu na polisi wakihamishwa hadi Bima ya Afya ya Jamii (SHA). Mwenyekiti wa Rupha, Dkt Brian Lishenga, alitangaza uamuzi huo kwenye kikao na wanahabari ambapo alisema walimu na polisi wanastahili kuhamishwa hadi SHA pale tu madeni wanayowadai yawe yamemalizwa. Dkt Lishenga alisema kuwa wanadai Kampuni ya Minet na Medical Administrators Kenya ambazo zimekuwa zikitoa huduma kwa walimu na polisi pesa ambazo lazima zilipwe kabla hawajahamishwa hadi SHA. Haya yanafanyika siku chache baada ya Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa TSC, Eveleen Mitei, kufika mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu elimu ambapo alisema kuwa kuna mpango wa kuwahamisha walimu hadi SHA. Kampuni ya Medical Administrators hutoa bima kwa zaidi ya walimu 450,000 na mkataba wao utatamatika mnamo Novemba 30. “Hatutaki kuwa na utata kama ule ambao ulitokea katika NHIF ambapo watu walihamishwa bila ya madeni yanayodaiwa hospitalini kulipwa,” akasema Bw Lishenga. Afisa huyo alifichua kuwa hospitali kadhaa bado hazijapokea malipo yao kwa kuwahudumia walimu na polisi kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Bima ya polisi huwa ni Sh8.9 bilioni kila mwaka nayo ya walimu ni Sh20 bilioni kwa kipindi hicho. Alifichua kuwa deni la Sh33 bilioni la NHIF liliongezeka wakati ambapo walimu na polisi walihamishwa hadi bima za kampuni za kibinafsi. “Badala ya kuyalipa madeni wanahamishwa hadi bima nyingine wala hatutavumilia uhamisho huo. Lazima wahamishwe tu SHA kama hawana deni na hatutaki kubeba deni kutoka upande huo mwingine,” akaongeza. Mwenyekiti huyo wa Rupha alithibitisha kuwa wagonjwa watalipa pesa taslimu kufuatia kuondoa huduma wanazotoa kwa waliojisajili na SHA. Hatua hiyo inakuja baada ya notisi ya siku 14 waliyotoa kukamilika. “SHA haikushughulikia malalamishi yetu wiki mbili zilizopita. Tumezungumzia masuala haya karibu kwa mwaka mmoja na sasa hospitali hazina pesa kabisa. “Msimamo wetu ni kwamba hospitali lazima zipewe pesa ili zihudumie wagonjwa. Bila hii usawa wa afya ambao umekuwa ukirindimwa na serikali hauna maana,” akasema. Dkt Lishenga alisema kuwa mfumo wa ufadhili wa SHA hautekelezeki kwa sababu bima hiyo hailipi madeni yake baada ya hospitali kutoa huduma kwa wagonjwa. “Wamekuwa wakikataa stakabadhi za matibabu na kuzitaja kama zisizofaa. Wanaougua kansa na magonjwa ya figo wamekuwa wakiumia sana baada ya matibabu yao kukosa kuidhinishwa,” akasema.
from Taifa Leo https://ift.tt/BsuE27W
via
IFTTT