MASHINDANO ya Riadha za Dunia ya 2025 yaliyofanyika jijini Tokyo yamefungua ukurasa mpya kwa historia ya michezo ya Kenya.
Hii ni kwa sababu taifa hili limezoeleka kutawala mbio ndefu.
Hata hivyo, matokeo ya Wakenya kwenye mbio fupi katika mashindano haya yamethibitisha kwamba vipaji vya asili vya wanariadha wa Kenya haviko tu kwenye mbio za masafa marefu, bali pia kwenye mbio fupi.
Ushindi na ulizopatikana kwenye mbio za mita 800 uliwafurahisha mashabiki na kuzua mjadala muhimu kuhusu uwekezaji katika mbio hizi.
Kenya haina budi kuchukua hatua za makusudi ili kuendeleza vipaji vipya kwenye mbio fupi.
Kwanza, mafanikio ya Tokyo yametoa ishara kuwa mashindano ya kimataifa hayana tena mtazamo kuwa ni himaya ya Wakenya.
Ikiwa wanariadha wachache waliopewa mafunzo na vifaa vya kisasa wameshinda medali, basi ikizingatiwa uwekezaji mwingi zaidi, Kenya inaweza kuibua kizazi cha wanariadha wa kasi watakaoshindana bega kwa bega na wakali kutoka Marekani, Jamaica na Canada.
Pili, uwekezaji katika mbio fupi utapanua wigo wa utambulisho wa michezo ya Kenya.
Kwa muda mrefu, taifa limejulikana kwa marathon na mbio za kati, lakini kujikita pia kwenye mbio fupi kutaleta heshima mpya na kuongeza idadi ya medali zinazotwaliwa.
Hali hii itawapa vijana wengi motisha ya kuingia kwenye riadha, kwani si kila mmoja ana uwezo wa kustahimili mbio ndefu. Wapo wenye misuli na mwendo wa kasi wanaohitaji tu kupewa nafasi na mafunzo.
Aidha, kukuza mbio fupi kutachangia ukuaji wa miundomsingi ya michezo nchini. Vifaa maalum, teknolojia ya saa za kisasa na mafunzo ya kiufundi vitahitajika.
Ujenzi wa kambi maalum za mazoezi na ajira ya makocha wa kiwango cha kimataifa kutaongeza ubora wa mafunzo si kwa watimkaji pekee bali pia kwa wanariadha wengine.
Wakati umewadia kwa serikali kupitia Wizara ya Michezo, pamoja na Shirikisho la Riadha Nchini, kuunda sera mahsusi ya kukuza mbio fupi.
Mashirika ya kibinafsi na wadhamini pia wanapaswa kushirikiana katika ufadhili.
Ikiwa taifa litawekeza, basi katika miaka michache ijayo Kenya haitatajwa tu kama mfalme wa masafa marefu bali pia kama kitovu cha wakimbiaji wa mbio fupi duniani.
Kwa jumla, mafanikio ya Tokyo hayakuja kwa kubahatisha, yanafaa kuwa uzinduzi mpya.
Kenya ikijipanga na kuwekeza ipasavyo, hakuna kitakachozuia vijana wetu kutwaa dhahabu si tu kwenye masafa marefu, bali pia kwenye mbio fupi.
from Taifa Leo https://ift.tt/KyNbrMa
via IFTTT