
RAIS William Ruto ametuma ujumbe wa pongezi kwa Rais mteule wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kufuatia ushindi wake katika uchaguzi wa urais uliofanyika Jumatano, Oktoba 29, 2025. Aidha, Dkt Ruto Jumatatu, Novemba 3, 2025 alimtuma Naibu wake Profesa Kithure Kindiki amwakilishe katika sherehe ya kuapishwa kwa Rais Samia jijini Dodoma, Tanzania. “Kwa niaba ya serikali na wananchi wa Jamhuri ya Kenya na kwa niaba yangu, ninampongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kufuatia ushindi wake katika uchaguzi wa urais uliofanyika Oktoba 29, 2025,” Ruto akasema kwenye ujumbe wake Jumatatu asubuhi, Novemba 3, 2025. Katika ujumbe wake, Rais Ruto alielezea uhusiano mzuri kati ya Kenya na Tanzania katika moyo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki huku akiahidi kudumisha uhusiano huo kwa manufaa ya mataifa hayo mawili. “Kenya na Tanzania iko na uhusiano mpana wa kihistoria na maazimio ya ustawi na uthabiti kwa manufaa wa raia wetu yaliyokita katika uanachama wetu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC),” akaeleza Dkt Ruto, ambaye ndiye mwenyekiti wa jumuiya hiyo wakati huu. Bi Samia aliibuka mshindi kwa kupata asilimia 97.6 ya kura zilizopigwa katika uchaguzi huo uliogubikwa na fujo. Dkt Ruto ndiye Rais wa pili wa mataifa wanachama wa EAC kutuma risala za pongezi  wa Rais Samia. Wa kwanza alikuwa Rais wa Somalia Sheikh Mohamed Mohamoud. Mwingine aliyetuma risala kama hizo za pongezi ni Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) Mohamoud Ali Yousouf.
from Taifa Leo https://ift.tt/VdX3pWk
via 
IFTTT