Sababu za maombi ya kubadilisha Sekondari Pevu kukataliwa

MAOMBI ya wanafunzi 143,821 wa Gredi ya 9 ya kubadilisha shule za Sekondari Pevu yamekataliwa kutokana na masomo waliyochagua au ukosefu wa nafasi katika shule walizochagua, Wizara ya Elimu imetangaza.

Waziri wa Elimu, Julius Ogamba, alisema kati ya maombi 355,457 yaliyopokelewa baada ya uteuzi wa awali Desemba 19, ni maombi 211,636 pekee yaliyoidhinishwa.

Alisema wengi walitaka shule bora za kitaifa kama vile Alliance, Kenya High na Mang’u, ambazo kila moja ilipokea hadi maombi 20,000 licha ya kuwa na wastani wa nafasi 500 pekee.

Waziri alisema uteuzi wa wanafunzi kuingia Gredi ya 10 katika Sekondari Pevu ulianza Desemba 14, 2025, na kuendelea hadi Desemba 19, 2025, wakati matokeo yalipotangazwa.

“Wanafunzi walipewa fursa ya kubadilisha shule kuanzia Desemba 23, 2025. Maombi yalishughulikiwa na kukamilika Desemba 29, 2025, na matokeo sasa yanapatikana kwenye tovuti ya uteuzi,” alisema Bw Ogamba katika taarifa kwa vyombo vya habari.

Aliongeza kuwa asilimia 88 ya wanafunzi wameteuliwa shule kulingana na chaguo zao za awali au zilizorekebishwa.

Wanafunzi ambao hawajaridhika bado watapata fursa nyingine ya kuomba wahamishiwe nyingine kuanzia Januari 6, 2026, hadi Januari 9, 2026.

Wanafunzi 1.13 milioni waliofanya mtihani wa kwanza wa KJSEA wanatarajiwa kuripoti katika shule za Sekondari Pevu kuanzia Januari 12, 2026.

Baada ya uteuzi wa awali, jumla ya maombi 355,457 ya kubadilisha shule yalipokelewa, huku kila mwanafunzi akiruhusiwa kuwasilisha hadi maombi manne.

“Baada ya kuyazingatia, maombi ya wanafunzi 211,636 yameidhinishwa. Maombi mengine yamekataliwa hasa kutokana na kukosekana kwa mchanganyiko wa masomo uliopendekezwa au ukosefu wa nafasi katika shule zilizochaguliwa,” alisema Bw Ogamba.



from Taifa Leo https://ift.tt/cGw7U1f
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post