Kijiji cha ulevi Baringo kilichogeuka chanzo kikuu cha mauti ya vijana

KATIKA kipindi cha mwaka mmoja uliopita familia kadhaa katika kijiji cha Poror, eneobunge la Eldama Ravine, Kaunti ya Baringo, zimewapoteza zaidi ya vijana wao 10 kutokana na unywaji wa pombe haramu iliyowekwa sumu ya “ethanol”. Pombe imegeuka chanzo kikuu cha mauti katika hali ambayo imewatamausha wakazi. Kwa mfano, familia ya Toroitich ingali na majonzi wakati huu baada ya mpendwa wao Kelvin Kipkurui, 27 kufa baada ya kubugia kileo hicho. Kipkuria alizirai langoni mwa hospitali ambako alikuwa amekimbizwa kwa matibabu wiki jana. “Uraibu wake wa kubugia pombe haramu uligeuka kuwa mbaya zaidi kiasi kwamba angeiba mali ya familia na kuziuza ili apate pesa za kununulia pombe,” anasema Alice Toroitich, shangazi ya mwendazake. Kufikia Desemba mwaka jana, afya ya Kelvin ilikuwa imezorota kiasi cha ngozi ya mwili wake kugeuka manjano.  Aidha, aliishiwa na nguvu kiasi kwamba hakuweza kutembea vizuri. Madaktari katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Eldama Ravine walimpima na kuthibitisha kuwa ini na figo yake iliharibiwa na pombe. [caption id="attachment_185054" align="alignnone" width="1638"] Baadhi ya pombe haramu inayodaiwa kuwa na sumu ya ethanol iliyonaswa. Picha|Florah Koech[/caption] Kevin aliruhusiwa kuondoka hospitalini huku akishauriwa kukoma kabisa kubugia pombe. Hata hivyo, baada ya kuwasili nyumbani alitoweka kwa saa kadhaa. Aliporejea, alikuwa akikohoa na kutapika damu. Wiki moja baadaye, alizirai nje ya mlango wake na akashindwa kabisa kuamka. “Pombe hii yenye sumu imechukua maisha ya mtoto wetu mwngine. Kawaida watoto ndio huzika wazazi wao. Lakini hapa Poror, ni wazazi wanaozika watoto wao,” shangazi ya Kevin akaeleza. Sio Kevin pekee yake. Justus Kiptoo, baba wa watoto wanane, alikufa baada ya kunywa pombe iliyoshukiwa kuchanganywa sumu ya “ethanol”. “Viungo vya mwili wa kakangu viliharibiwa na alikufa kutokana na matatizo kiafya,” akasema kakake Kaisang Kirui. Katika kijiji hicho cha Poror imekuwa ni ada kwa wanakijiji kuandaa michango ya fedha kugharamia mazishi au matitabu ya wahanga wa pombe yenye sumu. Ajabu ni kwamba hata wataalamu walioheshimiwa hawajasazwa. Mark Chumba, ambaye ni mwalimu wa shule ya msingi, amekuwa ni mraibu wa pombe haramu kwa miongo kadhaa. “Mimi hukopa zaidi ya Sh30,000 kugharamia pombe. Mimi hunywa hadi pesa hizo kuisha kisha nikarejea nyumba bila chochote. Niko dhaifu kiasi kwamba ni vigumu kutembea,” anaeleza. Bw Chumba amewahi kufanyiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Moi (MTRH) baada ya kutatizwa na pombe. Baada ya kuchoshwa na changamoto hiyo, baada ya wakazi wameanzisha mikakati ya kuidhibiti. Kwa mfano, Kasisi Lawrence Bomet ameazisha kanisa la waraibu wa pombe na dawa za kulevya nyumbani kwake. “Kijiji changuj kiko na sifa mbaya ya utengenezaji na uuzaji pombe haramu. Nikataka kurekebisha hali hii kwa kuziba pengo kati ya Kanisa na waraibu,” anaeleza. Kanisa la Kasisi Bomet pia hutoa ushauri nasaha, makazi na mafunzo kwa waraibu wa maovu hayo. Lakini idadi ya watu wenye tatizo hilo ni kubwa kiasi kwamba Kanisa la Bomet linaonekana kulemewa. Changamoto nyingine ni kwamba watengenezaji pombe hiyo hawaadhibiwa na mkono wa sheria. Wao hufunguliwa mashtaka katika Mahakama ya Eldama Ravine kisha wanaachiliwa huru kwa dhamana, katika hali ya kutatanisha.

from Taifa Leo https://ift.tt/ynLBMI1
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post