Kiti moto cha IEBC: Mrithi wa Marjan anavyosubiriwa na jinamizi kuu

KUONDOKA kwa Afisa Mkuu (CEO) wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Hussein Marjan kulikotajwa kama “makubaliano ya pande zote”, kumezua maswali mengi, hasa ikizingatiwa kuwa amekuwa wa tatu kuondoka katika wadhifa huo ambao sasa unaonekana kuwa kiazi moto.

Hatua hiyo imejiri chini ya miaka miwili kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027, jambo linalomaanisha kuwa uamuzi wa kumtema akiwa afisa aliyesalia kati ya wakuu wa tume hiyo waliosimamia uchaguzi tata wa 2022 utaendelea kupigwa darubini.

Ukweli ni kwamba Bw Marjan amefuata nyayo za waliomtangulia, Ezra Chiloba na James Oswago, ambao wote waliondolewa ofisini kwa mazingira tata, upinzani ukishinikiza wawajibishwe.

Ni wiki jana tu ambapo kiongozi wa chama cha Wiper Patriotic Front, Kalonzo Musyoka, aliongoza Muungano wa Upinzani kushinikiza Bw Marjan aondolewe kabla ya kumaliza muhula wake.

Bw Kalonzo alisema uchaguzi wa 2027 hauwezi kuwa huru na wa haki ikiwa Bw Marjan ataendelea kuwa ofisini.

“Bw Marjan hawezi kuaminika kusimamia Uchaguzi Mkuu wa 2027. Alipwe mshahara wa mwaka mmoja uliosalia kwenye mkataba wake. Uchaguzi hautakuwa huru na wa haki ikiwa ataendelea kuwa ofisini,” alisema Bw Musyoka.

Hata hivyo, madai hayo yanaibua upya hali ya ofisi hiyo yenye joto, ambayo imeshuhudia waliowahi kuishikilia wakiondoka kwa njia zisizo za heshima.

Ingawa wadhifa wa Afisa Mkuu Mtendaji haufungwi kwa muhula mmoja wa miaka sita kama ilivyo kwa makamishna, hakuna hata mmoja kati ya maafisa wakuu wa IEBC aliyedumu kwa muda wa kutosha kufikiria kuongezewa mkataba.

Bw Marjan aliteuliwa kushika wadhifa huo Machi 2022, baada ya kujiunga na tume hiyo kama Naibu wa Afisa Mkuu Mtendaji mnano Aprili 2015.

Kabla yake kuingia katika ofisi hiyo, kuondolewa kwa Bw Chiloba kulikuwa na kizaazaa katika muda mfupi aliokaa ofisini.

Alisimamishwa kazi hadharani na aliyekuwa Mwenyekiti wa IEBC marehemu Wafula Chebukati pamoja na makamishna wa zamani Abdi Guliye na Boya Molu.

Mvutano kati ya Bw Chebukati na Bw Chiloba ulikuwa mkali kiasi kwamba Chiloba alifungiwa nje ya ofisi yake, na kufuli kuwekwa mlangoni baada ya fununu kuenea kuwa alikuwa akirejea kazini.

Barua ya kusimamishwa kwake ilisema hatua hiyo ilichukuliwa kusubiri kukamilika kwa ukaguzi wa kina wa ununuzi uliohusiana na Uchaguzi Mkuu wa Agosti 8, 2017, pamoja na uchaguzi wa marudio wa Oktoba 26, 2017.

Alitumwa likizo ya lazima Aprili 2018 kabla ya kusimamishwa rasmi Juni 14, na hatimaye kufutwa kazi Oktoba 12, 2018.

Alikuwa ameteuliwa mwaka wa 2015. Bw Chiloba alipinga uamuzi huo mahakamani akidai kuondolewa kwake kulikuwa kinyume cha sheria, na kudai fidia ya angalau Sh52.5 milioni.

Kuhusu Bw Oswago, kuondoka kwake kulihusishwa moja kwa moja na sakata ya “Chickengate”, ambapo alifikishwa mahakamani. Oswago aliteuliwa CEO wa mpito wa IEBC Novemba 2011 kabla ya kuthibitishwa rasmi.

Kashfa hiyo ilihusisha kampuni ya Uingereza ya Smith & Ouzman, iliyopatikana na hatia ya kutoa hongo ya Sh47 milioni ili kupata zabuni ya kuchapisha karatasi za kura kwa kaimu wa tume huru ya uchaguzi iliyotangulia IEBC.

IEBC imeendelea kukumbwa na kashfa karibu kila msimu wa uchaguzi, hasa kuhusu ununuzi wa vifaa vya uchaguzi, mara nyingi kwa njia ya zabuni za moja kwa moja, hali inayozua maswali kuhusu uwazi na uwajibikaji.

Kwa muktadha huo, kuondoka kwa Bw Marjan kunazidisha taswira ya kwamba wadhifa wa Afisa Mkuu Mtendaji wa IEBC una mkosi huku ikisubiriwa kuona atakayechukua wadhifa wake.



from Taifa Leo https://ift.tt/pjfY4cq
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post