
UFUGAJI wa ndege wa mapambo unazidi kushika kasi humu nchini kila uchao kutokana na ukosefu wa ajira za afisini, Wakenya wengi sasa wanawazia kila mbinu bunifu zinazoweza kuwainua kimaisha kwa kuwazolea pato lao la kila siku.
Katika Kaunti ya Kisii, barobaro mmoja George Eshiwan Bota, 30, amezamia ufugaji wa ndege wa mapambo ambao umemtuliza baada ya kuhangaika kwa muda mrefu akisaka kazi.
Akilimali ilimzuru Eshiwan nyumbani kwao Kiogoro, eneobunge la Nyaribari Chache kufahamu mengi kuhusu ufugaji huo aliouanzisha miaka saba iliyopita.
Eshiwan ni daktari aliyefuzu lakini kwa kuwa bado hajaajiriwa kufanya utabibu huo, kwa sasa anafanya ufugaji wa ndege hao.
“Nilianza ufugaji wa ndege wa mapambo mwaka 2019. Nilizama katika ufugaji huu baada ya kumtembelea rafiki yangu jijini Kisumu. Rafiki huyo alinieleza kuwa ufugaji huu una kipato kizuri na nikavutiwa. Bila kusita, nilirudi nyumbani nami nikaanza kuwafuga ndege hawa mara moja,” Eshiwan anadokeza.
Shambani mwake, kuna makundi mawili ya ndege wa mapambo. Kuna ndege wafananao na kuku na kuna ndege wa njiwa. Katika kundi la kuku wa mapambo, Eshiwan ana sampuli tano.
Zinajumuisha aina za brahma, silkies bantams, polish bantams, Swedish flower na giant chicken.
Katika upande wa njiwa, kuna sampuli sita ambazo ni Indian fantail, Pomeranian pouter, shungi flair, capuchin, speckled pigeon na local pigeon.
[caption id="attachment_184842" align="alignnone" width="1080"]
George Eshiwan Bota akiwa bandani anakofugia ndege wa mapambo. PICHA | WYCLIFFE NYABERI[/caption]
Pia mkulima huyu ana kanga na bata.
Eshiwan anahoji kuwa alipoanza ufugaji, haikuwa rahisi kwake kupata ndege wa kuanzia kwani kijijini humo kwao hakukuwa na mkulima yeyote ambaye angempa vifaranga.
Ilimbidi anunue baadhi ya ndege hao kutoka kwa rafikiye wa Kisumu na akaongeza wengine kutoka kwa wafugaji waliofahamiana kupitia mitandaoni.
“Ilinibidi nifanye utafiti wangu kwa kina. Kutokana na ujio wa utandawazi, niliweza kupata mtu aliyeniuzia vifaranga nilioanza kuunda nao jamii yangu ya ndege wa mapambo,” Eshiwan anasema.
Kilimo cha ndege wa mapambo kulingana na Eshiwan ni kilimo chenye faida mno ikilinganishwa na kuku wa kawaida.
Mfugaji huyu anadokeza kuwa, ndege wa mapambo hawali chakula kingi kama kuku wa kawaida.
Pia anaongeza kuwa unapouza mayai ya ndege hao au hata ndege wenyewe, pesa unazozipata ni za juu ikilinganishwa na kuku wa kawaida.
Anasema kuwa ikiwa mtu anataka kununua kifaranga wa siku moja kutoka shambani mwake, kifaranga huyo anamuuza kwa Sh1,000.
Ikiwa ni njiwa kwa mfano, mkulima huyu huuza jozi kwa Sh40,000.
Kutokana na ufugaji huo, Eshiwan anasema kwa mwezi mzuri, anaweza kutia kibindoni zaidi ya Sh50,000 katika mwezi mzuri.
Kulingana naye, kuku wa mapambo wana manyoya laini mithili ya manyoya ya sungura. Manyonya hayo yametamalaki kote miilini mwao hadi miguuni lakini wanatofautishwa kutokana na mataifa wanayotokea na rangi zao.
“Brahma wana manyoya miguuni mwao. Asili yao ni nchini Marekani. Wakishakomaa, jogoo wanaweza kufikisha uzani wa hadi kilo 10 ilhali majike yanaweza kuwa kilo saba,” anaongeza.
Mkulima huyu anasema anaonea kilimo chake fahari hasa katika ufugaji wa njiwa. Kulingana naye, ufugaji wa njiwa una soko kubwa zaidi na yeyote aliye na moyo, anaweza kujizolea pato kubwa kutokana na ndege hao.
Anaeleza kuwa yeye hupata wateja wengi wanaotaka kununua njiwa kutoka kwake hasa maharusi wanapofunga pingu za maisha.
Anaeleza kuwa, njiwa wa manyoya meupe hupendelewa sana na maharusi.
“Njiwa ni kitega uchumi kikubwa shambani mwangu. Huwa ninapata wateja wengi ambao ni maharusi wakitaka njiwa wakati wa fungate zao. Mara nyingi, wanaofanya harusi hununua njiwa wakiwa jozi. Jozi moja huwa naiuza Sh50,000,” anaeleza barobaro huyo.
Eshiwan pia anadokeza kuwa njiwa hupendelewa na watu wakati wa kuandikishana mapatano ya amani.
“Wakati makubaliano hufanyika kuleta amani hasa katika ulingo wa siasa, njiwa huachiliwa kama ishara ya amani,” anadokeza.
Anawahimiza vijana ambao bado hawajapata ajira zozote licha ya kuhitimu vyuo vikuu kukumbatia ukulima na ufugaji ili kuyamudu maisha yao.
“Kuna pesa katika kilimo au ufugaji. Ninawahimiza vijana wenzangu tukijaribu kilimo. Tusiwe watu wa kubagua kazi,” Eshiwan anaeleza huku akidokeza kuwa yuko huru kuhamasisha vijana wenza kuhusu ufugaji huo bila malipo yoyote.
Ndani ya miaka mitano ijayo, Eshiwan angependa kugeuza nyumbani kwao kituo cha kufanya utafiti na mafunzo kuhusu ndege wa mapambo.
Mfugaji huyo anadokeza kuwa anafahamu kuwa hilo litagharimu rasilimali nyingi za fedha lakini ana imani ikiwa atapata msaada kutoka kwa serikali au wahisani wengine, basi ataweza kuafikia malengo hayo.
from Taifa Leo https://ift.tt/g5DVpT9
via IFTTT