Uhuru apanua kikosi kupiga jeki Matiang’i uchaguzi wa 2027

KIONGOZI wa Chama cha Jubilee, Rais mstaafu Uhuru Kenyatta ameanza kupanua mabawa ya chama hicho kukiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2027.

Katika mkakati ambao haukutarajiwa jana, chama hicho kilitangaza kuwa kitashirikiana na chama cha Party of National Unity (PNU) hatua inayotafsiriwa kama mbinu ya kuimarisha fursa ya mazungumzo ya mgombea urais wake, Dkt Fred Matiang'i na vyama vingine vikuu vya upinzani kuelekea 2027.

Tayari Jubilee imemteua rasmi Dkt Matiang’i kuwa mgombea wake wa urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Uhuru alianza kwa kumteua Dkt Matiangi naibu kiongozi wa chama ili kumuandaa kwa kinyang’anyiro cha urais 2027.

“Kwa kutambua hulka yake, sifa zake za uongozi na rekodi yake iliyothibitishwa ya mageuzi katika utumishi wa umma, PNU imeamua haitawasilisha mgombea wa urais na badala yake itamuunga mkono Bw Matiang’i,” PNU ilisema katika hafla ambayo ilihudhuriwa na maafisa wa vyama hivyo Jubilee akiwemo Dkt Matiang’i na Peter Munya.

Bw Munya, ndiye kiongozi wa chama cha PNU na alifanya kazi na Dkt Matiang’i katika baraza la mawaziri la Uhuru chini ya chama cha Jubilee.

Vyama hivyo vilivyowahi kutawala, viliashiria uwezekano wa kuundwa kwa mkataba wa kisiasa kuelekea 2027.

“Vyama vinajitolea kufanya kazi kwa pamoja na vyama vingine vyenye mwelekeo sawa ndani ya upinzani ili kuunda mfumo wa pamoja wa kazi, ambao utapitishwa na kutiwa saini rasmi wakati mwafaka,” alisema Katibu Mkuu wa Jubilee, Ole Kenta.

Mnamo 2018, Uhuru aliingia mamlakani kupitia Jubilee kutawala kwa muhula wa pili, huku Rais Mwai Kibaki akichaguliwa kwa tiketi ya PNU pia kwa muhula wa pili mnamo 2007, jambo linalopatia ushirikiano huo uzito wa kihistoria na wa kiishara.

Akiwa kiongozi wa Jubilee, hatua hizo zinatazamwa kuwa na baraka za Bw Kenyatta licha ya kutohudhuria hafla ya jana.

Muungano huo mpya unaonekana kulenga kufufua mitandao ya kisiasa ya Uhuru na Kibaki ili kuonyesha nguvu na uwezo wa kujadiliana ndani ya familia pana ya muungano wa upinzani.

Hata hivyo, hatua hiyo huenda ikamkera kiongozi wa Democracy for the Citizens Party (DCP) Rigathi Gachagua, anayejichukulia kama kinara wa siasa katika eneo la Mlima Kenya.

Wakati huo huo, muungano huo unaweza kutafsiriwa kama mikakati ya Dkt Matiang’i kuwania urais kivyake mwaka 2027 iwapo muafaka ndani ya upinzani hautapatikana.

Kulingana na Profesa David Monda wa Chuo Kikuu cha City University of New York, uteuzi wa mgombea urais wa pamoja wa muungano utategemea ni nani ataweza kumshawishi Bw Gachagua kumuunga mkono na iwapo atakuwa tayari kukidhi masharti yake.

Kwa mujibu wa mhadhiri huyo, kuungwa mkono na Bw Gachagua ni muhimu kwa muungano wa upinzani kwani anaweza kuathiri pakubwa mwelekeo wa siasa kwa kubaki upinzani au kurejea upande wa Rais Ruto.

Kuhusu mgombea mwenza, Profesa Monda alisema vigezo vitajumuisha uwiano wa kikanda au kikabila, jinsia, na uwezo wa kuleta kura pamoja na rasilmali za kifedha mezani.



from Taifa Leo https://ift.tt/VJ94Srb
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post