
BEI ya unga wa mahindi imeanza kupanda katika maeneo ya North Rift baada ya baadhi ya kampuni za kusaga bidhaa hiyo kumaliza akiba ya zao hilo, huku wakulima wakianza kuficha mahindi wakisubiri bei ipande zaidi kutokana na hofu ya uhaba unaokaribia. Gunia la mahindi la kilo 90 sasa linauzwa kwa Sh4,200 kutoka Sh3,800 wiki chache zilizopita, huku wakulima wengi wakichagua kuhifadhi mazao yao wakitarajia bei kupanda zaidi. Hatua hiyo imejiri licha ya serikali kutoa muda wa siku 30 kwa wakulima kuuza mahindi yao, la sivyo iruhusu uagizaji wa mahindi bila ushuru ili kushusha bei ya unga. Bw Jackson Kosgei, mkulima kutoka Moiben, Kaunti ya Uasin Gishu, alisema uhaba wa chakula hauwezi kuepukika kutokana na uzalishaji mdogo msimu huu uliosababishwa na mabadiliko ya tabianchi wakati wa upanzi. “Kampuni nyingi za kusaga unga tayari zimeishiwa na akiba na mavuno hayakuwa mazuri. Hali hii itasababisha upungufu mkubwa,” alisema. Bei ya unga imepanda katika maduka mengi ya rejareja eneo la North Rift, huku pakiti ya kilo mbili ikiuzwa kwa Sh160 kutoka Sh120 hapo awali. Ongezeko hilo linajiri huku zaidi ya Wakenya 2.5 milioni wakikabiliwa na uhaba wa chakula unaochangiwa na ukame wa muda mrefu. Ukaguzi uliofanywa katika maduka mbalimbali umebaini kuwa wauzaji wengi wameongeza bei licha ya juhudi za serikali kujaribu kuidhibiti. Bw David Maina, alisema kupungua kwa usambazaji wa mahindi kumesababisha gharama kupanda. “Gharama ya mahindi imeongezeka na imetulazimu kuongeza bei ya unga ili kuendelea na shughuli,” alisema.
from Taifa Leo https://ift.tt/yaqE6jV
via
IFTTT