
PENDEKEZO la Jopokazi kuhusu Dhuluma za Kijinsia (GBV) la kuanzisha adhabu ya “kuhasiwa kwa kemikali” kwa wahalifu wa makosa ya kingono wanaopatikana na hatia limezua mjadala mpana nchini, huku wataalamu wa afya, wanasheria na wanaharakati wa haki za binadamu wakitoa maoni yanayokinzana kuhusu athari na uhalali wa hatua hiyo.
Jopokazi hilo lililoongozwa na aliyekuwa Naibu Jaji Mkuu Nancy Baraza, limependekeza marekebisho ya Sheria ya Makosa ya Kingono ya 2006 ili kujumuisha adhabu ya kuhasi kwa kemikali wanaume na wanawake wanaopatikana na hatia ya kuwadhulumu watoto na watu wenye ulemavu.
Ingawa pendekezo hilo limewasilishwa kama suluhu kali ya kukabiliana na ongezeko la visa vya dhuluma za kingono, wataalamu wanaonya kuwa linaweza kuwa na madhara ya kiafya, kimaadili na kisheria ya muda mrefu.
Dkt Ahmed Ali Yousef, daktari wa mfumo wa mkojo na Mkuu wa Idara katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Aga Khan, anaeleza kuwa kuhasi kwa kemikali ni suala nyeti linahusu tiba, maadili na sheria.
Kwa mujibu wake, hatua hiyo inaweza kuchukuliwa kama aina ya ukatili unaotumia tiba kama chombo cha adhabu.
Mtaalamu huyo mwenye tajriba ya zaidi ya miaka 30 katika kudhibiti homoni za kiume, hasa kwa wagonjwa wa saratani ya tezi dume, anasema testosterone ni homoni yenye nguvu inayochangia si tu hamu ya ngono, bali pia afya ya mifupa, misuli, nguvu za mwili na uthabiti wa kiakili.
Anatahadharisha kuwa kuipunguza ghafla hushtua mwili mzima.
Kitaalamu, kuhasi kwa kemikali hufanywa kwa kutumia dawa zinazozuia uzalishaji wa homoni hiyo, na si upasuaji.
Dawa hizo hutolewa kwa njia ya sindano za mara kwa mara, kila mwezi au baada ya miezi kadhaa, na athari zake hupungua iwapo matibabu yatasitishwa.
Lengo ni kufikia kiwango cha chini kabisa cha homoni hiyo, kinacholingana na hali ya mtu aliyehasiwa kwa upasuaji.
Hata hivyo, wataalamu wanasema madhara yake ni makubwa. Mbali na kupoteza hamu na uwezo wa ngono, mhusika anaweza kukumbwa na msongo wa mawazo, mabadiliko ya hisia, joto kali mwilini, kuongezeka kwa uzani, kudhoofika kwa mifupa, magonjwa ya moyo, kisukari na hatari ya kujiua.
Wakili na mtetezi wa haki Omoke Morara anasema utekelezaji wa adhabu hiyo utahitaji marekebisho ya wazi ya sheria, kwani adhabu za jinai lazima zibainishwe wazi.
Anaonya pia kuwa wahalifu wanaweza kupinga adhabu hiyo mahakamani kwa misingi ya madhara ya kiafya na ukiukaji wa haki za binadamu, ikiwemo marufuku ya adhabu za kudhalilisha kama ilivyoainishwa katika Katiba na mikataba ya kimataifa.
Naye mtetezi wa haki za binadamu, Adrian Kibe wa Tume ya Haki za Binadamu Kenya anasema sera kama hiyo inahitaji uangalizi huru na maadili thabiti ya kitabibu hali ambayo ni vigumu kufanikisha kwa mfungwa.
Anaonya kuwa kusisitiza adhabu kali kunaweza kupuuza chanzo halisi cha ukatili wa kingono, unaochochewa zaidi na masuala kama malezi na kiwewe cha kisaikolojia.
Wadau wanasema kuwa ingawa jamii ina hamu ya kuona haki ikitendeka, hatua zozote lazima zizingatie ulinzi wa waathiriwa na haki za binadamu.
from Taifa Leo https://ift.tt/fECdFnp
via IFTTT