
MBUNGE wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) Winnie Odinga, ametangaza kuwa yuko tayari kushirikiana na mrengo wa amu yake Oburu Oginga, ili kuimarisha chama cha Orange Democratic Movement (ODM) nchini.
Hapo awali, mbunge huyo alikuwa akihusishwa na kundi la waasi ndani ya ODM la ‘Linda Mwananchi’, linaloongozwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Bw Edwin Sifuna pamoja na Gavana wa Siaya, Bw James Orengo.
Hata hivyo, hatua yake ya kuhudhuria mkutano ulioongozwa na mwenyekiti wa ODM jijini Nairobi na Mbunge wa Makadara, Bw George Aladwa, inatarajiwa kuibua mjadala mkubwa wa kisiasa ndani ya chama hicho, ingawa alisema yuko tayari kupigania ODM.
“Chama hiki ni nyumbani kwetu, nyumba aliyojenga baba yangu. Ninawezaje kuondoka hapa? Niende wapi? Nitasalia hapa ODM,” alisema Bi Odinga.
Akizungumza wakati wa mkutano huo uliofanyika katika Jaramogi Oginga Odinga Foundation (JOOF), Bi Odinga, alisema yuko tayari kuchukua jukumu ambalo marehemu baba yake, Raila Odinga, aliwahi kutekeleza kama mwakilishi wa Nairobi katika ngazi ya kitaifa ndani ya ODM.
Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Bi Odinga kuhudhuria mkutano katika taasisi hiyo tangu kifo cha babake, na pia ilikuwa mkutano wake wa kwanza na wajumbe wa ODM kutoka Nairobi.
Wajumbe hao pia waliunga mkono pendekezo litakalowasilishwa kwa uongozi wa ODM kabla ya mkutano mkuu wa wajumbe wa chama hicho (NDC), uliopangwa kufanyika Machi 27.
Wanataka katiba ya chama kurekebishwa ili kuanzishwa kwa wadhifa mwingine wa naibu kiongozi wa chama.
“Linapokuja suala la nyadhifa za chama, wale waliotoa maisha yao kupigania chama wanapaswa kupewa kipaumbele. Tutaenda huko, Nairobi lazima iwe na kiti mezani,” alisema.
Kulingana naye, Kaunti ya Nairobi ina idadi kubwa ya wapigakura ambao wamekuwa wakikiunga mkono chama hicho kwa miaka mingi, na hivyo inapaswa kuwakilishwa katika kamati za kufanya maamuzi ndani ya ODM.
“Nairobi itatoa sauti yake na Machi 27 itakuwa siku yetu. Ni wakati wa ODM,” alisema.
Wakati huo huo, viongozi wa ODM jijini Nairobi, walisema nafasi ya naibu kiongozi wa chama inaweza kuwa mwanzo wa safari ya kisiasa ya ndani ya nchi kwa Bi Odinga kuelekea uchaguzi wa 2027, ambapo anatarajiwa kugombea mojawapo ya viti jijini.
Bw Aladwa alisema wamekuwa wakifanya mikutano na viongozi wa ODM jijini Nairobi kwa miezi kadhaa, wakijadili jinsi ya kuhakikisha Kaunti hiyo inapata mwakilishi katika uongozi wa chama.
“Karibu kila eneo lina mwakilishi katika uongozi wa chama, lakini tangu Raila atuache hatuna mwakilishi. Tunataka Winnie Odinga awe katika meza kuu ya uongozi. Pendekezo hili lilitolewa mwaka jana na sasa tuko tayari kuliwasilisha katika NDC,” alisema.
Iwapo matakwa ya Nairobi yatakubaliwa, mbunge huyo atakuwa naibu wa nne wa kiongozi wa ODM, akifanya kazi pamoja na kiongozi wa chama Dkt Oburu.
Atajiunga na Gavana wa Kisii Simba Arati, Gavana wa Mombasa Abdulswamad Nassir na Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi, ambao tayari ni manaibu wa kiongozi wa chama.
Diwani wa Kilimani, Bw Moses Ogeto, alisema Bi Odinga ataleta nguvu mpya katika ODM jijini Nairobi na kusaidia chama hicho kurejesha umaarufu wake katika maeneobunge yote 17 ya uchaguzi jijini.
from Taifa Leo https://ift.tt/1Smbi5K
via IFTTT