Atwoli achaguliwa kuongoza COTU kwa muhula wa sita baada ya kukosa mpinzani

KATIBU Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi Kenya (COTU) Francis Atwoli ataongoza kwa muhula wa sita mfululizo baada ya kuchaguliwa bila kupigwa katika mkutano wa wajumbe uliofanyika katika Chuo cha Mafunzo ya Leba cha Tom Mboya, Kisumu.
Zaidi ya wajumbe 250 kutoka vyama 47 vya wafanyakazi wakiwakilisha wafanyakazi zaidi ya milioni nne, walihudhuria mkutano huo ambapo Atwoli mwenye umri wa miaka 76 alichaguliwa kuongoza Cotu hadi 2031.
Tofauti na uchaguzi mwingine nchini Kenya unaojulikana kwa ushindani mkali, uchaguzi wa COTU ulifanyika kwa utulivu na kwa maelewano, huku Bw Atwoli akikosa mpinzani wa wadhifa wa Katibu Mkuu.
Uchaguzi huo ulimpa muhula wa sita tangu alipochukua wadhifa huo mwaka 2001 baada ya kumrithi Joseph Mugalla, na kumfanya kuwa Katibu Mkuu aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi katika historia ya COTU na mmoja wa viongozi wenye ushawishi mkubwa zaidi katika harakati za wafanyakazi nchini Kenya.
Kwa zaidi ya miaka 32, Bw Atwoli pia amekuwa kiongozi wa Kenya Plantation and Agricultural Workers Union (KPAWU) chenye makao yake makuu Nakuru. Wachanganuzi wanasema uchaguzi wake bila mpinzani ulitokana na mikakati makini kabla ya kuanza rasmi kwa uchaguzi.
Awali, Bw Atwoli alikutana na viongozi wa vyama 42 kati ya 44 Januari 6, kabla ya uchaguzi wa matawi na kitaifa kuanza.
Baada ya mkutano huo, vyama hivyo vilimuidhinisha kwa muhula mwingine wa miaka mitano, na hivyo kuondoa uwezekano wa kupingwa.
“Ninafurahishwa na msaada niliopata kutoka vyama 42 kwa muhula mwingine wa miaka mitano, tutaendelea kulinda haki za wafanyakazi na kuimarisha COTU (K) kwa siku za usoni,” Bw Atwoli alisema wakati huo.
Mkutano huo wa wajumbe ulithibitisha umahiri wa kisiasa wa Bw Atwoli, huku baadhi ya vyama vikiwabado kukamilisha uchaguzi wa matawi.
Uchaguzi huu ulifanyika miezi kadhaa kabla ya tarehe ya mwisho ya Agosti 30 iliyowekwa na Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi ya vyama vya kitaifa kama COTU na Trade Union Congress (TUC) kukamilisha uchaguzi wao.
Miongoni mwa sababu za kufanikisha ushindi wake ni mipango yake ya mapema, uhusiano wa muda mrefu na viongozi wa vyama, na uwezo wake wa kushawishi wajumbe.
Uchunguzi miongoni mwa wajumbe unaonyesha imani kubwa katika uongozi wake na uthabiti alioleta katika vyama vya wafanyakazi.
Bw Atwoli amesisitiza kwamba wadhifa wake si kwa manufaa yake binafsi, bali ni kwa maslahi ya wafanyakazi milioni nne wanaowakilishwa na COTU (K). “Huu ni wadhifa wa wafanyakazi wote, si wangu binafsi,” alisema.
Mwaka uliopita, alichaguliwa tena kama Mjumbe wa Shirika la Leba Ulimwenguni na kuwa mjumbe aliyehudumu kwa muda mrefu.
Aidha, amehudumu kama Rais wa Shirika la Vyama vya Wafanyakazi la Muungano wa Afrika miongoni mwa nyadhifa nyingine za kimataifa.


from Taifa Leo https://ift.tt/C7pKz14
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post