Tuju asema atatetea mali yake hata kama ni kwa uhai wake

MASAIBU ya aliyekuwa waziri, Raphael Tuju kuhusu mali anayozozania na benki yanaendelea huku akidai kuwa polisi waliingia kwa nguvu kwenye jengo lake la Dari Park, Karen, Ijumaa Machi 13, 2026 usiku na kujeruhi mmoja wa watoto wake.
Bw Tuju alisema kikosi kikubwa cha polisi kilifika bila habari saa tisa usiku na kufunga lango la Dari Business Park ili kuzuia watu kuingia.
“Walifukuza walinzi wangu na wafanyakazi. Wametwaa mali yangu kwa nguvu,” alisema.
Hali hii iliathiri biashara karibu 25 zilizo ndani ya jengo hilo, ikiwemo ofisi ya Bw Tuju.
“Mmoja wa watoto wangu ambaye alikuwa akisimamia eneo hili alikimbizwa katika hospitali ya MP Shah na anapokea matibabu,” aliongeza.
Bw Tuju alisisitiza kwamba hatatoka kwenye mali yake na kudai kuwa maafisa hawakuonyesha amri yoyote ya mahakama kuwaruhusu kuingia.
“Sitatoka hapa, watalazimika kunibeba kwa machela, hawana amri ya mahakama. Hata wakiwa nayo, sheria hairuhusu kufurushwa saa tisa usiku. Hii si halali,” alisema.
Alidai pia kuwa kuna watu wenye nguvu wanaomezea mate mali yake.
“Kuna mtu mkubwa hapa nchini aliyejaribu kununua mali yangu na nilikataa. Sitaki kutaja majina kwa sasa kwa sababu ukweli utafichuka,” alisema. Aliongeza kuwa wanalenga mali yake ya thamani na si pesa; “Nina fedha za kulipa,” alisema.
Katika video zilizosambazwa mitandaoni, Tuju alisema maafisa walifika kwa magari sita.
“Wakenya wenzangu, sasa ni saa tisa na nusu asubuhi, bado nimesimama nje ya lango. Nimefukuzwa na polisi wenye silaha waliokuja kwa magari sita yasiyo na utambulisho,” alisema, akiongeza ni ukiukaji wa sheria kwa sababu hawakuwa na amri ya mahakama.
Alisema maafisa hao walikuwa wamefunika nyuso zao.
Bw Tuju alisisitiza alikuwa analinda tu biashara ya familia yake na kuwaomba Wakenya kusimama kidete kulinda haki zao.
“Niko imara. Niko tayari kufa kwa sababu wengine wengi wametoa kafara kama hii. Ni kafara ya ukweli,” alisema.
Kesi hii inahusiana na mgogoro wa kisheria kati yake na East African Development Bank kuhusu mkopo wa Sh2.2 bilioni uliochukuliwa mwaka 2015.
Mahakama Kuu ya Uingereza na Wales ilimuagiza Tuju kulipa mkopo huo mwaka 2019, uamuzi uliothibitishwa baadaye na mahakama za Kenya.
Mahakama ya Rufaa Kenya pia ilithibitisha uamuzi huo, huku Mahakama Kuu ikikataa kuahirisha utekelezaji wa uamuzi huo.
Mgogoro unahusu mali mbili za thamani kubwa mtaani Karen, ikiwemo Entim Sidai Wellness Sanctuary na jengo la Tamarind Karen pamoja na Dari Business Park.
Baada ya mchakato mrefu wa kisheria, Jaji Josephine Mongare aliruhusu wakopeshaji na madalali kutwaa mali hizo, huku akikataa jaribio la Tuju kufungua kesi upya akisema “ni ukiukaji wazi wa mchakato wa mahakama” uliolenga kuzuia utekelezaji halali baada ya mchakato mrefu wa kisheria.
Hata hivyo, Licha ya kikwazo hiki, Mahakama Kuu imemruhusu.
Raphael Tuju na kampuni yake, Dari Limited kukata rufaa dhidi ya uamuzi uliotolewa mapema mwezi huu. Mahakama imemwelekeza kuwasilisha rufaa na kesi itatajwa Machi 17, 2026 kwa maagizo zaidi.


from Taifa Leo https://ift.tt/3ky0n2E
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post