Mgawanyiko katika chama cha Alfred Mutua, mwandani wake akukutana na Ruto

MVUTANO wa kisiasa kati ya Waziri wa Leba na Ulinzi wa Jamii, Alfred Mutua na Mbunge wa Kibwezi West, Mwengi Mutuse umeibuka wazi baada ya mbunge huyo kuongoza kundi la viongozi wa Maendeleo Chap Chap Party (MCCP) kuondoka kwenye chama hicho kinachohusishwa na Mutua.
Mutuse sasa ameanza kupigia debe chama cha United Democratic Alliance (UDA), hatua iliyomkera Mutua huku kukiwa na madai kuwa Rais William Ruto anashinikiza kuvunjwa kwa MCCP.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika AIC Mukuni, Kaunti ya Machakos, Mutua alisema baadhi ya viongozi wameiaibisha jamii ya Wakamba.
Kauli hiyo ilieleweka kuwalenga viongozi wa MCCP kutoka Machakos na Makueni walioongozwa na Mutuse waliokutana na Rais Ruto katika ikulu ya Nairobi siku iliyotangulia.
Mvutano huo ulianza baada ya kundi la viongozi wa MCCP wanaomuunga mkono Mutuse kukutana na Rais Ruto bila kumhusisha Mutua kujadili hatima ya chama hicho.
Mutuse, mbunge wa muhula wa kwanza aliyepata umaarufu kitaifa baada ya kuongoza mchakato wa kumbandua aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, kwa miaka mingi amekuwa mshirika wa karibu wa Mutua kisiasa.
Katika wiki mbili zilizopita, Mutuse ameongoza ujumbe wa viongozi kutoka Machakos na Makueni kukutana na Rais katika Ikulu, jambo linaloashiria mabadiliko ya kisiasa huku Mutua akifanya mikutano  kujadili shinikizo za kuvunjwa kwa chama chake.
“Tutafanya kazi kwa karibu zaidi na Rais Ruto chini ya UDA. Hata hivyo, vyama havivunjwi wala kuunganishwa rasmi kwa sasa,” Mutuse aliambia Taifa Leo katika mahojiano.
Hatua hiyo imejiri takriban wiki tatu baada ya msaidizi wa Rais Farouk Kibet kumshawishi Mutuse kuondoka MCCP na kujiunga na UDA. Inadaiwa pia alimweleza kuwa ana nafasi nzuri ya kuteuliwa kuwa katibu wa kitaifa wa chama hicho.
Tangu wakati huo, Mutuse amebadilisha rangi ya mikutano yake kutoka zambarau ya MCCP hadi manjano, rangi rasmi ya UDA, ishara ya kujiweka karibu na chama hicho. Hata hivyo, Mutua ameendelea kutumia rangi ya zambarau katika mikutano yake.
Ingawa hajathibitisha wazi iwapo ataondoka MCCP, Mutua amesema bado anafikiria shinikizo kutoka kwa Rais Ruto la kuvunja chama hicho.
Mutua alikumbusha jinsi aliyekuwa Mbunge wa Kibwezi marehemu Kalembe Ndile alivyodaiwa kusalitiwa kisiasa baada ya kuvunja chama chake kabla ya uchaguzi wa 2017.
Wachambuzi wa siasa wanaamini mvutano huo unatokana pia na tamaa za kisiasa za viongozi hao wawili. Mutua anaripotiwa kulenga kuwania kiti cha Seneta wa kaunti ya Machakos katika uchaguzi wa 2027 huku pia akitajwa kuwa na ndoto za urais mwaka 2032.
Kwa upande mwingine, Mutuse anaonekana kutumia mtandao wa UDA kujijengea ushawishi wa kitaifa mapema kabla ya uchaguzi.
Mgogoro huo umevuta pia ukosoaji kutoka kwa washirika wa kiongozi wa Wiper Democratic Movement Kalonzo Musyoka, huku Gavana wa Machakos Wavinya Ndeti akisema hatua ya Mutuse ni sawa na kile Mutua alifanya alipohama chama cha Wiper kuanzisha MCCP.
Hata hivyo, Mutuse amepuuza mgawanyiko huo akisema hatua ya kujiunga na chama kikubwa cha kitaifa inalenga kuunganisha nchi na kuharakisha maendeleo kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027.


from Taifa Leo https://ift.tt/M7qjTuc
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post