ODM yakemea UDA na kuitaka iache kabisa kunyemelea ngome zake

CHAMA cha ODM kimeonya UDA kwamba, hakitakubali muafaka wowote ambao utaruhusu chama hicho tawala kuwasimamisha wagombeaji katika ngome zake kwenye uchaguzi mkuu wa 2027.

Jana, viongozi wa ODM waliibua wasiwasi kutokana na kile walichosema ni mwenendo wa UDA kuwatambua wagombeaji wa nyadhifa mbalimbali katika ngome zake ilhali wanashirikiana ndani ya Serikali Jumuishi.

Hasa wabunge hao walitaja Magharibi mwa Nchi na Pwani kama maeneo ambako UDA imeanza kutangaza kuwa itawasimamisha wagombeaji ilhali maeneo hayo ni ngome ya ODM.

“Kilifi kwa mfano ni ngome ya ODM lakini jinsi tulivyo, tayari nina mshindani kutoka UDA ilhali watu wetu wanaambiwa waendelee kurindima ngoma ya Rais William Ruto kuhudumu kwa mihula miwili,” akasema Mbunge mmoja kutoka Kilifi.

“Nataka kufahamu iwapo UDA itakuwa na mgombeaji au la ili nijipange,” akaongeza.

Alisema hayo baada ya ODM kuandaa mkutano wa kwanza wa kundi la wabunge na maseneta wake tangu kuaga dunia kwa aliyekuwa Kiongozi wa chama hicho Raila Odinga.

Mkutano huo ulihudhuriwa na baadhi ya wabunge waasi ambao wanaegemea mrengo wa Katibu Mkuu anayekabiliwa na utata Edwin Sifuna.

Kiongozi wa ODM Dkt Oburu Oginga aliongoza kikao hicho ambacho duru zinaarifu wabunge wengi walisema kuwa iwapo UDA itaingilia ngome za chama chao basi hakuna haja ya kumakinikia muafaka na Rais Ruto.

Kiongozi wa wachache Junet Mohamed akiongea baada ya mkutano huo, alisema suala la UDA kutokuwa na wagombeaji ni kati ya masuala ambayo yanazungumziwa kwenye muafaka unaonukia na UDA kuelekea 2027.

“Tumempa Kiongozi wa Chama wajibu wa kuibuka na mfumo utakaotumika pamoja na kusaka msimamo kuhusu hili suala la ODM kuachiwa ngome zake,” akasema Bw Mohamed.

Mbunge huyo wa Suna Mashariki alisema haja yao kuu ni kuhakikisha kuwa ODM inadumisha viti ambavyo chama hicho kinashikilia na hata kuongeza zaidi katika uchaguzi wa 2027.

“Kile ambacho tunamakinikia sana ni kwamba tunataka kuongeza idadi ya viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi mkuu wa 2027,” akaongeza Bw Mohamed.

Kiongozi huyo aliyaonya makundi mengine ya kisiasa wanayoshirikiana nayo kuwa ikifikia kuhusu idadi ya wawakilishi, ODM haitalegeza kamba.

“Idadi ya wanachama wetu bungeni ni suala ambalo hatutajadiliana au kukubali ipungue kwa sababu ndiyo nguvu yetu,” akasema Bw Mohamed.

Dkt Oginga naye aliwakumbusha wabunge hao kuwa wanaposisitiza ngome za ODM zisiingiliwe, lazima wafanye juhudi za kuimarisha chama mashinani.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo mnamo Jumatatu, Mwenyekiti wa Bodi ya Uchaguzi wa UDA Anthony Mwaura alisema chama hicho kitakuwa na wagombeaji wa nyadhifa mbalimbali kote nchini, kauli iliyofasiriwa kupinga msimamo wa ODM.

Bw Mwaura aliongeza kuwa katika maeneo ambapo ODM na UDA zina nafasi finyu ya kuwahi ushindi, basi vyama hivyo vitashiriki mchujo wa pamoja kuibuka na mgombeaji bora.

Mwenyekiti huyo hata hivyo alisema kuwa marehemu Raila Odinga alikuwa amekubali kuwa ODM na UDA ziandae mchujo wa pamoja maeneo teule.

“Tumeweka wazi kuwa hakuna kuachiana viti maeneo fulani kwa sababu UDA itakuwa na wagombeaji,” akasema Bw Mwaura.

Naye Katibu Mkuu wa UDA Hassan Omar pia alinukuliwa akisema hawataachia ODM viti kwa sababu wote wanatafuta kuwa na idadi ya wawakilishi wengi.

“Hakuna kutengeana viti na kila mtu lazima ajipiganie kushinda viti. Wale ambao wana kura tatu wazilete kama tu wale wenye kura 300,” akasema Bw Omar.

“Mbona uogope ushindani kama unahisi eneo ambalo unawania ni ngome yako ya kisiasa,” akaongeza.

Mwenyekiti wa ODM Gladys Wanga na Mbunge wa Homa Bay mjini Opondo Kaluma wamekuwa kati ya wanasiasa ambao wamekuwa wakisisitiza chama hicho kinastahili kuachiwa ngome zake nao pia hawatakuwa na wagombeaji kwenye ngome za UDA.

“Ngome za ODM lazima zilindwe na kuachiwa chama na kama hili halitaheshimika basi mazungumzo hayo yataporomoka,” akasema Bw Kaluma hivi majuzi.

“Unahitaji kuwa na idadi ya juu ya viongozi ambao wamechaguliwa ili kuwa na sauti kabla na baada ya uchaguzi. Baada ya kila uchaguzi, ukihitaji mgao, idadi ya wawakilishi ndio huangaliwa,” akaongeza.

Mkutano wa jana ulihudhuriwa na wabunge wengi ila Bw Sifuna hakuwepo.

Wabunge kutoka mrengo wake wa Linda Mwananchi waliohudhuria ni Wilberforce Oundo (Funyula), Obadiah Barongo (Bomachoge Borabu) na Clive Gisairo (Kitutu Masaba) pamoja na Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi.



from Taifa Leo https://ift.tt/dr9hzy8
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post