Natembeya kulipwa Sh2.5m kwa kupakwa tope la ufisadi 2025

MAHAKAMA Kuu imefuta mashtaka ya ufisadi dhidi ya Gavana wa Trans Nzoia, George Natembeya, yaliyotokana na uchunguzi kuhusu ufisadi wa Sh1.4 bilioni, na kumlipa Sh2.5 milioni kama fidia kwa ukiukaji wa haki zake za kikatiba.

Katika uamuzi wake, mahakama ilikosoa wapelelezi wa Serikali, ikisema taarifa za M-Pesa zilizotumika kama ushahidi zilipatikana kinyume cha sheria, jambo lililovunja haki za faragha za gavana.

Mahakama pia ilisema kuwa uamuzi wa kumfikisha Gavana Natembeya mahakamani haukuwa na msingi wa kisheria na ulikuwa matumizi mabaya ya mfumo wa haki.

“Kuruhusu mashtaka kuendelea kutakuwa ukiukaji wa utaratibu wa mahakama na kutumia mfumo wa haki za jinai kwa malengo ambayo haukukusudiwa kuyashughulikia, na kudhuru haki na imani ya umma katika sheria,” mahakama ilisema.

Kesi hiyo ilianza kutokana na uchunguzi wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kuhusu ununuzi na malipo yaliyodhaniwa kuwa kinyume cha sheria katika Serikali ya Trans Nzoia.

Wachunguzi walimshutumu Natembeya pamoja na baadhi ya maafisa wa kaunti kwa kuingilia zabuni na kupokea rushwa kutoka kwa wakandarasi katika miradi ya thamani ya Sh1.4 bilioni.

Mnamo Mei 2025 maafisa wa EACC walivamia makazi ya Natembeya eneo la Milimani, Kitale, wakitafuta stakabadhi zinazohusiana na ufisadi aliodaiwa kuhusika nao.

Baadaye alikamatwa, kuzuiliwa katika makao makuu ya EACC Nairobi, na kufikishwa katika Mahakama ya Milimani, Nairobi akishtakiwa kwa mashtaka ya mgongano wa maslahi na ununuzi wa mali za umma kinyume cha sheria.

Alikana mashtaka yote na kuachiliwa kwa dhamana.

Katika kesi aliyowasilisha katika Mahakama Kuu, Natembeya alidai wapelelezi walivunja haki zake wakati wa kukamatwa na uchunguzi, kama vile kumnyima kupata wakili mara moja.

Mahakama ilikubaliana naye, ikisema kuwa tabia ya wachunguzi ilikuwa kinyume cha katiba.

Mahakama ilibatilisha karatasi ya mashtaka iliyowasilishwa Mei 20, 2025, na kuzuia Idara ya Uchunguzi wa Jinai (DCI) na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kufufua kesi hiyo kwa msingi wa ushahidi iliyotumia.

“Uamuzi wa kumshutumu mshitakiwa, ukiangaliwa kwa undani, haukuwa na msingi sahihi,” mahakama ilisema.

Upande wa mashtaka ulipinga kesi ya gavana huyo, ukisema kuwa kukamatwa, kuchunguzwa na kufikishwa mahakamani kulikuwa halali na kulitekelezwa ndani ya mamlaka ya kikatiba.

Hata hivyo, mahakama ilipuuza hoja hizo, ikibaini kuwa uchunguzi ulikiuka haki za kikatiba, ikiwa ni pamoja na faragha na haki ya kuwakilishwa kwa mshukiwa kisheria.

“Ukiukaji huu ulikuwa wa makusudi na unaonyesha kutojali sheria, haki asilia na heshima ya binadamu,” mahakama ilisema, na kumpa Gavana Sh2.5 milioni kama fidia kwa madhara yote pamoja na kuagiza waliopinga kesi ya Natembeya kulipa gharama zote za kesi.

Mahakama pia ilibaini kuwa ushahidi muhimu, hasa taarifa za M-Pesa, ulipatikana kinyume cha sheria na haukubaliki.



from Taifa Leo https://ift.tt/eJVDLZF
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post