Utawala wa Kenya Kwanza kukopa Sh5.9 trilioni ndani ya miaka 3 kufadhili matumizi yake

SERIKALI itakopa Sh5.9 trilioni katika miaka mitatu ya fedha ijayo ili kufadhili matumizi yake, jambo ambalo litafanya deni la umma la nchi kuwa zaidi ya Sh12.25 trilioni.

Mpango wa kukopa katika mwaka wa fedha wa 2026/27 hadi 2028/29 umefafanuliwa katika Mkakati wa Kudhibiti Deni wa Muda wa Kadri 2026 (MTDS), hati ya serikali iliyotayarishwa na Wizara ya Fedha na kuwasilishwa Bungeni.

Hati hiyo ya serikali inakadiri deni la taifa litakuwa takribani Sh15.7 trilioni ifikapo Juni 2029, kutokana na mchanganyiko wa mikopo ya ndani ya asilimia 82 na ya nje ya asilimia 18, “kwa kutegemea uthabiti wa kifedha na usimamizi wa deni”.

Ukopaji kwa miaka hiyo mitatu ni sawa na Sh2 trilioni kwa mwaka, Sh163.9 bilioni kwa mwezi, Sh5.5 bilioni kwa siku, Sh227.6 milioni kwa saa, Sh3.8 milioni kwa dakika na Sh63,228 kwa sekunde.

Kamati ya Bunge ya Deni la Umma na Ubinafsishaji, katika ripoti yake, inatoa tahadhari kuwa kuongezeka kwa deni kunapunguza fedha za matumizi kutokana na kuongezeka kwa malipo ya madeni.

Kwa kuzingatia serikali inategemea mikopo ya kibiashara, Kamati inapendekeza Wizara ya Fedha kuweka mfumo thabiti wa kuripoti matumizi ya mikopo hiyo ili kuboresha uwajibikaji, “hasa pale fedha hizo zinapotumika kupiga jeki bajeti ya jumla.”

Kamati hiyo inasema serikali inaendelea na mageuzi ya kimuundo yanayoelekezwa kuongeza ukuaji na ushindani, ikiwa ni pamoja na mageuzi yanayoongeza uzalishaji, kukuza mauzo ya nje na kuboresha mazingira ya uwekezaji, yote kwa lengo la kudumisha deni kwa muda mrefu.

Ripoti ya kamati inaonyesha kuwa katika kipindi cha 2026/27–2028/29, gharama za riba za wastani wa Sh1.2 trilioni zitakuwa takribani asilimia 54 ya Pato la Taifa (GDP) na kuchukua karibu asilimia 41 ya mapato ya jumla.

Hii ina maana kuwa sehemu kubwa ya mapato itatumiwa kulipa madeni badala ya kuwekeza katika miradi ya kuongeza uzalishaji na ukuaji wa Pato la Taifa.

Ofisi ya Bajeti ya Bunge (PBO) imesema kuwa ukopaji unaotarajiwa unaweza kupunguza matumizi ya pesa za maendeleo na kuzua visiki visivyo vya moja kwa moja kwa serikali za kaunti.

Mkakati wa Kudhibiti Deni wa Muda wa Kadri ni muhimu kwa kuongoza mikopo ya serikali na kusimamia deni la umma kwa mujibu wa katiba na Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma (PFM).

Unatoa mpango wa Wizara ya Fedha wa kukidhi mahitaji ya kifedha ya serikali kila mwaka huku ikijaribu kupunguza gharama na kudhibiti hatari muhimu, hasa hatari za riba, ukosefu wa fedha za kigeni na mikopo ya muda mrefu.

Kufikia Novemba 2025, deni la taifa lilikuwa Sh12.25 trilioni, likijumuisha Sh6.78 trilioni zilizokopwa humu nchini na Sh5.47 trilioni kutoka nje ya nchi.

Kwa kuwa nakisi ya bajeti iliyopendekezwa ya mwaka 2026/27 ni Sh1.2 trilioni, kamati inatarajia mikopo ya kibiashara kuendelea, “hivyo basi kuongeza gharama ya jumla ya deni.”



from Taifa Leo https://ift.tt/xnNXiJB
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post