Makachero wakusanya ushahidi wa ndege iliyoua mbunge huku rubani akiombolezwa

WAPELELEZI wamemaliza kukusanya ushahidi muhimu katika eneo ilipotokea ajali ya helikopta iliyomuua Mbunge wa Emurua Dikirr, Johana Ng’eno, na watu wengine watano Jumamosi alasiri.

Kikosi kinachojumuisha wapelelezi kutoka Idara ya Uchunguzi kuhusu Uhalifu (DCI) na wataalamu wa usafiri wa ndege, walitumia Jumatatu kukagua eneo la ajali hiyo na kutoa vifaa vya ndege na vya kiufundi vilivyofafanuliwa kuwa sawa na kifaa maalum cha kuhifadhi mawasiliano kwenye ndege.

Vifaa hivyo vinatarajiwa kutoa data kamilifu kuhusu nyakati za mwisho za ndege hiyo kabla ya ajali.

Wapelelezi sasa wamegeukia uchunguzi wa kiufundi Nairobi, kuashiria awamu mpya ya kutegua kitendawili kuhusu mkasa huo wa helikopta, huku makachero wakinuia kuunganisha nyakati za mwisho za ndege hiyo na kutoa majibu thabiti kuhusu ajali hiyo.

Wakati huo huo, familia, jamaa na marafiki wamemwomboleza rubani aliyekuwa miongoni mwa watu sita, akiwemo mbunge wa Emurua Dikirr Joshua Ng’eno, walioangamia kwenye ajali ya helikopta Jumamosi katika Kaunti ya Nandi.

Katika kijiji chake cha Durubi, Nyakach, Kaunti ya Kisumu, majonzi yametanda kwenye boma ambapo jamaa na marafiki wanaendelea kukusanyika kuomboleza na kufariji familia.

Bi Margaret Akinyi, shangazi yake rubani George Were, aliposikia kwa mara ya kwanza kuhusu mkasa huo, aligubikwa na wasiwasi kwa mbali.

“Habari zinazochipuka zilipojitokeza, nilitatizika mno. Nilitaka tu kujua ni nani alihusika. Hata kama sio mtu niliyemjua, watu sita kuangamia kwenye helikopta ni tukio la kuhuzunisha sana,” alisema.

Akipania kutegemea ripoti zilizothibitishwa pekee, alisubiri thibitisho kutoka kwa kituo cha televisheni ya kitaifa badala ya kugeukia mitandao ya kijamii.

“Mimi si mtu anayetegemea habari kutoka mitandao ya kijamii kwa sababu nyingi huwa ni za kupotosha. Mtangazaji alipotaja George Were kama mmoja wa wahasiriwa, nusura nivunje televisheni. Sikutarajia habari za aina hiyo,” alisema machozi yakimlengalenga.

Mama yake wa kambo, Bi Jane Odero, alimtaja Bw Were kuwa nguzo ya familia. Familia inasubiri maandalizi ya mazishi, huku simanzi ikiwagubika kuhusu mazingira ya kifo chake.

Jumapili, familia ilifichua marehemu Were alikuwa anajiandaa kustaafu baadaye mwaka huu baada ya kuhudumu miongo kadhaa.

Dkt Francis Were alifichua kaka yake mdogo alitazamiwa kustaafu Septemba baada ya kutimiza miaka, 65.
Kulingana na Dkt Were, marehemu ameacha mjane na wana wawili walio chuoni.



from Taifa Leo https://ift.tt/bGEjrfI
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post