
MAUTI ya Mbunge wa Emurua Dikirr Johana Ng'eno yamezua kumbukumbu kuhusu safari yake ya kisiasa ilipoanzia hasa jinsi ambavyo alipokonywa ushindi katika uchaguzi mkuu wa 2007 akiwania kiti cha eneobunge la Kilgoris.
Uchaguzi huo ulifanyika wakati ambapo eneobunge hilo halikuwa limegawanywa na kutoa nafasi ya eneo jipya la Emurua Dikirr.
Katika uchaguzi huo wa 2007, Bw Ng'eno alikuwa akitumia chama kisicho na umaarufu cha Kaddu kusaka uongozi wakati huo akiwa na umri wa miaka 32.
Ni maeneobunge mawili pekee ambayo hayakuwa na wakilishi baada ya uchaguzi huo; Kilgoris na Wajir Kaskazini.
Kwenye eneobunge la Kilgoris hakukuwa na matokeo ya kutangazwa nako Wajir Kaskazini wagombeaji wawili walitoshana kwenye idadi ya kura za washindi.
Kilgoris, Bw Ng'eno alikuwa akielekea kumbwaga Waziri wa Usalama wa Ndani wakati huo Gideon Konchellah, ambaye alikuwa akiwania kupitia PNU lakini ghasia zilitokea katika ukumbi wa kuhesabu kura.
Licha ya kuwania kupitia UDM, Bw Ng'eno alikuwa kifua mbele dhidi ya Julius Sunkuli (Kanu), Peter Sapalan (ODM), Simon ole Maasi (ODM-K), Samuel Tunai (UDM) lakini hakutangazwa mshindi kutokana na ghasia zilizochipuka.
Hali ilikuwa tete zaidi kwa sababu hakukuwa na matokeo ya kutangaza baada ya ukumbi ambako vifaa vya uchaguzi vilikuwa vikihifadhiwa kuteketezwa na wananchi wenye hasira.
Uhasama wa kisiasa hasa ulikuwa kati ya jamii kubwa ya Maasai na Kalenjin ambao ndio walikuwa wachache katika eneobunge hilo.
Hii ndiyo ilisababisha Bw Ng'eno aelekee kumbwaga Bw Konchellah kwa sababu jamii ya Maa licha ya wingi wao, waligawanya kura kati ya wawaniaji wengi waliokuwa debeni.
Katika uchaguzi mdogo ulioandaliwa baadaye, ODM wakati huo ikiongozwa na Raila Odinga na William Ruto akiwa na ushawishi mkubwa katika jamii ya Wakalenjin, walimuunga mkono Bw Ng’eno.
Kwa upande mwingine, Waziri wa zamani marehemu William Ole Ntimama na Joseph Nkaissery nao waliasi chama na kusimama na jamii yao wakimfanyia Bw Konchellah kampeni kali.
Siku ya kura, viongozi hao walihakikisha kwamba kila Maasai anayeishi Kilgoris anajitokeza kupiga kura na hivyo ndivyo Bw Konchellah aliwahi ushindi na kuendelea kuongoza eneobunge hilo kabla ya kubwagwa kwenye uchaguzi wa 2022.
Hata hivyo, baada ya kubuniwa kwa eneobunge la Emurua Dikirr, Bw Ng'eno amekuwa na wakati rahisi kuwahi ushindi hata kama hayuko ndani ya vyama vikubwa.
from Taifa Leo https://ift.tt/E7Oihc9
via IFTTT