Mnajiaibisha kwa kutukanana, maaskofu wakemea viongozi

MAASKOFU wa Kanisa Katoliki Kenya wamelaani vikali matusi yanayoendelea kati ya Rais William Ruto na viongozi wa upinzani, wakitaka wanasiasa kupunguza maneno makali katika majukwaa ya umma. Akizungumza jana, mwenyekiti wa Baraza Kuu la Maaskofu hao (KCCB) Askofu Mkuu Maurice Muhatia Makumba, alisema matusi yanayorushwa hadharani yanavunja heshima ya viongozi na pia kuwadharau wananchi wanaowasikiliza. “Mnatukanana hadharani mbele ya wananchi, hamdharau tu wenzenu bali pia mnawadharau wananchi. Huo ndio ujumbe mnaotutumia,” alisema askofu huyo. Askofu Mkuu Muhatia, ambaye pia ni kiongozi wa dayosisi ya Kisumu ya Kanisa Katoki, alitoa kauli hiyo mjini Machakos wakati wa hafla ya kumtawaza rasmi Askofu Joseph Mwongela kama askofu wa Dayosisi ya Machakos, kufuatia kustaafu kwa Askofu Norman King’oo Wambua. Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Mwakilishi wa Papa nchini Kenya, Askofu Mkuu Hubertus Matheus van Megen, ambaye alitangaza kuwa Askofu Mwongela ataendelea kuhudumu kama msimamizi wa muda wa dayosisi ya Kitui hadi Papa atakapoteua askofu mpya. Mabadilishano ya maneno makali kati ya Rais Ruto na upinzani unaoongozwa na kiongozi wa chama cha Democracy for the Citizens Party, Rigathi Gachagua, yalitawala mazungumzo katika hafla hiyo. Askofu Muhatia alisema matusi hayo yanaathiri vibaya taswira ya uongozi mbele ya vijana na watoto wanaotazama viongozi wao. “Watoto wanaowasikiliza wameshtuka. Vijana wanaowasikiliza wameathirika kisaikolojia kwa sababu ndani yenu wanaona ndoto zao za uongozi zikivunjika. Watu wazima wanaowasikiliza wanaona aibu; nyinyi ni mfano mbaya wa kizazi chetu,” alisema. Aliongeza kuwa viongozi wanaweza kutofautiana kisiasa bila kutumia lugha ya matusi. Kwa upande wake, Gavana wa Machakos County, Wavinya Ndeti, aliwahimiza viongozi kuonyesha heshima wanapozungumza hadharani. “Watu wazima wanapotukanana hadharani, vijana huiga tabia hiyo. Hatupaswi kushangaa vijana wanapotutukana sisi viongozi. Lazima tuheshimiane, la sivyo tunaweza kuingiza nchi katika machafuko,” alisema. Aliongeza kuwa viongozi wanapaswa kukumbuka kuwa Kenya ndiyo nchi pekee waliyonayo  na hivyo wanapaswa kulinda umoja na heshima katika siasa za taifa.

from Taifa Leo https://ift.tt/dYVGkR1
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post