Mwanzo wa talaka kundi la Sifuna likiapa kususia mkutano wa ODM-UDA

BAADHI ya wabunge wanaoegemea mrengo wa Linda Mwananchi wamesema kuwa hawatahudhuria Mkutano wa pamoja wa Kundi la Wabunge (PG) ambao umeitishwa na Rais William Ruto na Kiongozi wa ODM Oburu Oginga hii leo.

Katika kile kinachoonekana kama kuendeleza upinzani wao dhidi ya serikali, wabunge hao walisema hawawezi kuhudhuria mkutano ambao utatumika kuidhinisha ripoti ya Ajenda 10.

Muafaka wa ajenda hizo ulitiwa saini na Rais Ruto na marehemu Raila Odinga mnamo Machi 7 mwaka jana.

Masharti ya muafaka huo ni kutekelezwa kwa yaliyomo ndani ya mwaka mmoja lakini wabunge hao wanasema hilo halijafanyika.

Wabunge hao walitaja polisi kuendelea kuvuruga mikutano ya upinzani, kucheleweshwa kwa fidia kwa wahanga wa maandamano, kupanda kwa gharama ya maisha kama baadhi ya sababu ambazo zimefanya wasusie mkutano huo.

Wakizungumza na Taifa Leo, waliothibitisha hawataenda ikulu ni Naibu Kiongozi wa ODM ambaye pia ni Seneta wa Vihiga, Godfrey Osotsi na wabunge Anthony Kibagendi (Kitutu Chache Kusini), Caleb Amisi (Saboti) na Wilberforce Oundo (Funyula).

Seneta wa Kisii, Richard Onyonka alisema bado anashauriana na wenzake ndani ya Linda Mwananchi ili waamue kuhusu suala hilo pamoja.

Hata hivyo, alisema mkutano huo unahusu malengo ambayo wamekuwa wakiyapinga.

Katibu Mkuu wa ODM, Bw Edwin Sifuna ambaye amekuwa sura ya Linda Mwananchi hata hivyo hakujibu maswali iwapo atahudhuria mkutano huo au la.

Viongozi wengine ambao hawakujibu iwapo watakuwa ikulu leo au la ni Gavana wa Siaya James Orengo, Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, Caroli Omondi (Suba Kusini) na Majimbo Kalasinga (Kabuchai) ambaye alichaguliwa kupitia Ford Kenya.

Bw Osotsi alisema hakubaliani na ajenda ya mkutano huo akiwashutumu viongozi wa ODM watakaohudhuria kama wanaomsaliti marehemu Raila Odinga.

Kulingana naye, ajenda 10 hazijatekelezwa ndani ya mwaka mmoja jinsi ambavyo Bw Odinga alikubaliana na Rais Ruto.

“Mbona nihudhurie na sikubaliani na kile wanachofanya? Rais Ruto na wandani wake ODM hawajatekeleza ajenda 10 na wamekuwa mstari wa mbele kuuangamiza muafaka huo,” akasema Bw Osotsi.

“Mrengo wa Ruto hauna haja ya kutekeleza ajenda hizo bali unaangalia tu maslahi yao. Msingi wa Serikali Jumuishi ni ajenda 10 bora na bila hiyo, ushirikianao huo unastahili kuporomoka,” akaongeza.

Bw Amisi alisema hawezi kujihusisha na UDA aliyosema inaongoza nchi vibaya hasa kwa kuwakandamiza viongozi wa upinzani.

Alidai wanaokosoa Kenya Kwanza wanakamatwa na wanasiasa wa upinzani kurushiwa vitoza machozi ilhali hayo ni kati ya maovu ambayo Hayati Raila aliyakashifu alipokuwa hai.

“Siwezi kuhudhuria mkutano na hutawahi kuniona kwenye mkutano wowote na UDA. Nimewahi kusema hapo awali kuwa UDA ni mbaya kwa nchi hii,” akasema.

“Hawajatekeleza chochote walichoahidi Raila mbali na kuanzisha Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC). Gharama ya maisha bado iko juu, hakuna fidia, baadhi ya vijana waliokamatwa wakati wa maandamano bado wanazuiliwa na hakuna uhuru wa kuzungumza na kutangamana,” akaongeza Bw Amisi.

Kwa tathmini yake, Bw Kibagendi alisema asilimia 30 ya muafaka huo ndiyo imetekelezwa. Alisema hawezi kuenda Ikulu ilhali wasiounga Serikali Jumuishi wamekuwa wakilengwa visivyo na kuondolewa kwenye nyadhifa wanazoshikilia katika kamati za bunge.

“Uongozi wa ODM nje na ndani ya bunge haujali maslahi ya raia na binafsi sitahudhuria mkutano huo kwa sababu nimelengwa na Serikali Jumuishi.”

“Junet (Mohamed) na wenzake wamekuwa wasaliti na ukweli ni kwamba hakuna chochote cha maana ambacho kimetekelezwa chini ya muafaka huu,” akasema Bw Kibangendi.

Bw Oundo alisema amezungumza na Wakenya na wengi wanahisi ajenda 10 haijatekelezwa huku akisema mkutano wa kundi la wabunge wa ODM na UDA hauko kwenye katiba ya chama cha Chungwa.

“Hakuna chama kinachofahamika kama Serikali Jumuishi. Tunasubiri kuona ripoti yao kwa umma lakini nimetangamana na raia na wamesema hakuna kilichotendeka,” akasema Bw Oundo.

Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung’wah na mwenzake wa wachache Junet Mohamed Ijumaa wiki jana walituma mwaliko kwa wabunge wa Kenya Kwanza na ODM kuhudhuria mkutano huo ambao utakuwa maadhimisho ya kwanza tangu muafaka wa Rais na Bw Odinga utiwe saini.

Bw Mohamed alisema kuwa Rais Ruto na Kiongozi wa ODM Dkt Oburu Oginga watatumia mkutano huo kutoa mwongozo wa ushirikiano kati ya ODM na UDA kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.



from Taifa Leo https://ift.tt/D9jMPEJ
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post