
MAASKOFU wa Kanisa Katoliki nchini wamekosoa serikali ya Kenya Kwanza inayoongozwa na Rais William Ruto, wakisema kuwa baadhi ya miradi yake mikuu haionyeshi matokeo ya kuridhisha wananchi.
Maaskofu hao wametaja kuendelea kudorora kwa hali ya usalama, changamoto katika sekta ya elimu, pamoja na matatizo katika Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA), wakizihusisha na kile walichoita kuvunjika kwa mifumo iliyoundwa kushughulikia mahitaji ya wananchi.
Kupitia Baraza lao la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Kenya (KCCB), viongozi hao walisema wanazidi kuwa na wasiwasi kuhusu mwelekeo wa taifa, huku maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao yakishika kasi.
Wakizungumza Nairobi jana, maaskofu hao walimtaka Rais Ruto na viongozi wengine kuchukua hatua za haraka kukabiliana na ongezeko la makundi ya wahuni wakionya kuwa hali hiyo inaweza kuwa hatari zaidi isipodhibitiwa.
“Tunaamini kwamba lazima wanafadhiliwa na watu wenye ushawishi mkubwa. Wanazunguka nchini bila hofu ya kuwajibishwa.
“Haiwezekani watu waende kuua wengine na kuvuruga mikutano ya hadhara huku maafisa wa usalama wakitazama bila kuchukua hatua. Hili linatutia wasiwasi—ni kina nani wanaowaongoza hawa wahuni?” alisema Mwenyekiti wa KCCB, Askofu Mkuu Maurice Muhatia.
Maaskofu hao walitoa mfano wa kushambuliwa kwa Seneta wa Vihiga, Godfrey Osotsi jijini Kisumu pamoja na visa vingine vya kuvurugwa kwa mikutano ya kisiasa.
Walisema kurejea kwa makundi ya wahuni ni jambo la kutia hofu hasa ikizingatiwa historia ya nchi hii wakati wa maandamano ya vijana dhidi ya serikali.
“Kuenea kwa desturi ya wahuni wanaotumika kutisha, kuvuruga mikutano na hata kuua kunawezekana tu ikiwa wanafadhiliwa na kulindwa na watu wenye ushawishi,” taarifa yao ikasema.
Aidha, maaskofu hao wamekosoa matamshi yasiyo na maadili kutoka kwa baadhi ya viongozi wa kisiasa, wakisema yanadhalilisha heshima ya ofisi za umma na umoja wa taifa.
“Tunalaani matamshi haya ya aibu tunayoshuhudia kutoka kwa viongozi wetu. Heshima ni ya pande zote na lazima idumishwe bila kujali tofauti za kisiasa,” walisema.
Kuhusu uchumi, maaskofu hao wametaka serikali kuchukua hatua za haraka kupunguza athari za kupanda kwa bei ya mafuta, wakisema maisha ya wananchi yanazidi kuwa magumu kutokana na mabadiliko ya soko la mafuta duniani yanayosababishwa na mgogoro wa vita katika ukanda wa Mashariki ya Kati.
Walisisitiza umuhimu wa mazungumzo ili kupunguza madhara ya kiuchumi kwa wananchi na biashara.
Aidha, walielezea wasiwasi wao kuhusu kucheleweshwa kwa malipo kwa taasisi za afya zinazomilikiwa na makanisa, wakisema hospitali nyingi zinakabiliwa na madeni makubwa.
“Madeni ya hospitali zetu za Kikatoliki yanazidi Sh5.7 bilioni, yakijumuisha madai yaliyokataliwa na kurejeshwa. Hali hii haifai kuendelea,” walisema.
Kuhusu elimu, maaskofu hao walikosoa mfumo wa Elimu ya Umilisi (CBE), wakisema ulianzishwa bila maandalizi ya kutosha na bila ushirikishaji wa wadau muhimu.
“Hatupaswi kuwaweka watoto wetu katika hali ya majaribio ya mara kwa mara. Mfumo huu unaonekana haujapangwa vizuri na kutekelezwa ipasavyo,” walisema.
Kuhusu suala la ufisadi, maaskofu hao walisema bado kuna wizi wa mali ya umma, mikataba ya ufisadi na uporaji wa ardhi, wakitaja pia madai ya kujaribu kunyakua ardhi ya taasisi za kidini.
Walisema hakuna dalili za dhamira ya dhati ya kupambana na ufisadi na kuwataka Wakenya kushirikiana kuupinga.
“Hatujaona dhamira ya kweli ya kupambana na ufisadi. Wakenya lazima tuamke na kukataa kuwa sehemu ya mfumo huu,” walisema.
from Taifa Leo https://ift.tt/vtJhHfB
via IFTTT