
MJI wa Wajir unakabiliwa na uhaba mkubwa wa malazi huku ukijiandaa kuwa mwenyeji wa sherehe za kitaifa za Madaraka Dei zitakazoongozwa na Rais William Ruto Jumatatu ijayo.
Maelfu ya wageni kutoka sehemu mbalimbali za nchi wanatarajiwa kuhudhuria hafla hiyo, wakiwemo viongozi wa kitaifa, maafisa wa usalama, wanamuziki na wageni wengine mashuhuri.
Hata hivyo, maandalizi hayo sasa yameibua changamoto kubwa ya ukosefu wa vyumba vya kulala katika mji huo ambao kwa kawaida huwa mtulivu na wenye idadi ndogo ya wageni.
Hoteli na nyumba za wageni zilizopo tayari zimejaa siku kadhaa kabla ya sherehe hizo huku baadhi ya wageni wakikosa mahali pa kulala.
“Maafisa fulani wa serikali wametuomba tusitoe vyumba vyetu katika wiki ya mwisho wa mwezi huu kwa sababu vinahifadhiwa kwa wageni wa serikali,” alisema Caroline Kinoti, msimamizi wa New Lodge mjini Wajir.
Inaelezwa kuwa hoteli zote nane zilizopo mjini humo zimejaa kabisa huku ada ya vyumba ikiongezeka mara mbili kutoka wastani wa Sh1,500 hadi Sh3,000 kwa usiku.
Mmiliki wa hoteli moja mjini humo Ismael Hassan alisema Wajir haina uwezo wa kutosha wa kuwahudumia wageni wote wanaotarajiwa.
“Tunahitaji uwekezaji mkubwa katika sekta ya hoteli ili wakati wa hafla kama hizi tuweze kutoa huduma zinazohitajika,” alisema.
Aliongeza kuwa hoteli yake imejaa hadi Juni 5, 2026 na sasa wanawasiliana na wenye nyumba binafsi ili kuzikodisha kwa wageni zaidi.
Kutokana na hali hiyo, serikali kwa ushirikiano na kaunti imeanza kukodisha nyumba za watu binafsi ili kuwahudumia wageni wa kitaifa.
Kamishna wa Kaskazini Mashariki John Otieno alikiri kuwa Wajir inakabiliwa na uhaba mkubwa wa malazi.
“Hii ni hafla kubwa inayotarajiwa kuleta watu wengi sana na tumegundua kuwa malazi yaliyopo hayatoshi,” alisema.
from Taifa Leo https://ift.tt/nzHkBfh
via IFTTT