
NAIBU wa Rais Kithure Kindiki amejitenga na madai ya njama ya kuiba kura katika Uchaguzi Mkuu wa 2027, huku baadhi ya wabunge wa chama tawala cha UDA kutoka Magharibi mwa Kenya wakisisitiza kuwa lazima Rais William Ruto “arejee madarakani” liwe liwalo baada ya uchaguzi wa 2027.
Profesa Kindiki aidha amewataka viongozi wanaoegemea mrengo wa serikali kukoma kutoa semi za madai ya wizi wa kura, akisema zinaweza kuleta uhasama na chuki miongoni mwa Wakenya na hata kulichoma taifa.
Akizungumza wakati wa hafla za kukagua miradi ya maendeleo jana katika eneobunge la Kitutu Chache Kaskazini, Kaunti ya Kisii, Profesa Kindiki alisema lengo pekee la serikali ni utoaji wa huduma na kwamba matokeo ya 2027 yataamuliwa na Wakenya na si mipango ya kisiasa.
“Hakuna mipango, na hapatakuwa na mipango, ya kuingilia maamuzi ya wananchi mwaka 2027. Yeyote anayedai vinginevyo anajisemea mwenyewe,” Profesa Kindiki aliwaambia wakazi wa Geteri, kufuatia mwaliko wa mbunge wa eneo hilo Japheth Nyakundi.
“Hakuna mtu atakayeiba kura. Kazi yetu ni kutumikia Wakenya. Wakati huo utakapofika, tutajiwasilisha kwa wananchi wa Kenya. Wakitutaka, watatupa mamlaka tena na nina imani watatupa tena kwa kuwa tumefanya kazi," akaongeza Prof Kindiki.
Naibu Rais aliitetea Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) akionyesha imani kwamba itaandaa uchaguzi huru na wa haki mwaka ujao.
"Nyinyi mnajua, serikali iliyopita haikuwa inamuunga mkono rais wa sasa William Ruto. Lakini kwa kusimamia haki, ilitangaza mshindi kulingana na mapenzi ya Wakenya," akasema Profesa Kindiki.
Matamshi ya Profesa Kindiki yanajiri siku chache baada ya wabunge kadhaa wa UDA kutoka Magharibi mwa Kenya kuzua gumzo kuhusu wizi wa kura wikendi iliyopita.
Naibu Gavana wa Kakamega Ayub Savula na Mbunge wa Hamisi Charles Gemose, waliwaambia wazi wajumbe wa chama tawala UDA wanaotoka eneo la Magharibi wasaidie katika kuvuruga matokeo ya uchaguzi kwenye vituo vya kupigia kura maeneo yao siku ya uchaguzi Agosti 9.
Wanasiasa hao walidai kuwa IEBC ni kiungo cha serikali kwa sababu inategemea “bajeti kutoka serikali ya Rais Ruto,” na hivyo haiwezekani kwake kushindwa katika kinyang’anyiro kitakachoendeshwa na taasisi hiyo.
“Nataka nyinyi kama wajumbe wa UDA mnapoenda kwenye vituo vya chaguzi (2027), mhakikishe mnamfanyia ukarabati Ruto. Nimekuwa bungeni kwa mihula mitatu na ninajua mambo haya (kuingilia),” akasema Bw Gemose.
Bw Savula alisema, "ni sisi (serikali) tunalipa IEBC na makamishina. Ruto ndiye anayemiliki bajeti inayofadhili IEBC. Mna kichaa ikiwa mnafikiri anaweza kushindwa kwenye chaguzi."
Matamshi hayo yaliyotolewa mbele ya Gavana wa Bungoma Ken Lusaka, anayeongoza kampeni ya Rais Ruto eneo hilo, yameongeza mdahalo wa umma unaozidi kuchacha kuhusu njama za kuingilia chaguzi za 2027.
from Taifa Leo https://ift.tt/ersybaF
via IFTTT