#RejectEbolaFacility: Wakenya wapinga dili ya Amerika na Ruto kuhusu Ebola

UPINZANI dhidi ya mpango kati ya Serikali ya Kenya na Amerika wa kuanzisha kituo cha kutenga wagonjwa wa Ebola katika Kaunti ya Laikipia umeanza kushika kasi, baada ya viongozi wa eneo hilo, madaktari na mashirika ya kiraia kuungana kupinga utekelezaji wake.
Wakenya wanasema mpango huo haujafafanuliwa kikamilifu kwa wananchi na unaibua maswali mazito ya kiusalama na kisera.
Mahakama Kuu tayari imesitisha utekelezaji wa mpango huo kufuatia kesi iliyowasilishwa na Katiba Institute, hatua iliyopokelewa kwa furaha na viongozi wa Laikipia na baadhi ya makundi ya kisiasa nchini.
Kwa mujibu wa taarifa zinazoendelea kujadiliwa nchini, Amerika inapanga kuanzisha kituo cha vitanda 50 katika Laikipia, Nanyuki, ambacho kitatumika kutenga raia wake walio katika hatari ya maambukizi ya Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Kituo hicho kitasimamiwa na maafisa wa afya wa Amerika na kuwa na wataalamu takribani 30 kutoka Huduma ya Afya ya Umma ya Amerika.
Hata hivyo, mpango huo umekumbana na upinzani mkali kutoka kwa Wakenya, ambao wanasema unaleta hatari ya kugeuza nchi kuwa kituo cha kuhifadhi wagonjwa wa nje huku mfumo wa afya wa ndani ukiwa bado dhaifu.
Viongozi wa Laikipia Mbunge wa Laikipia Mashariki Mwangi Kiunjuri, wenzake wa Laikipia Magharibi Wachira Karani, Sarah Korere wa Laikipia Kaskazini na Mwakilishi wa Kike Jane Kagiri walisema kwa pamoja kuwa, hawakubaliani na mpango huo, wakisisitiza kuwa haujazingatia maslahi ya wananchi wa eneo hilo wala usalama wa taifa.
“Kwa mtazamo wetu kama wawakilishi wa wananchi wa Laikipia, tunaona hakuna mantiki kwa kaunti yetu kuwa eneo la kituo cha Ebola. Serikali lazima iwe wazi kwa wananchi kuhusu makubaliano haya na kwa nini Laikipia imechaguliwa,” walisema katika taarifa yao ya pamoja.
Viongozi hao walihoji pia kwa nini Amerika haijaweka kipaumbele kuanzisha kituo hicho katika eneo la mlipuko wa ugonjwa huo, hasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, badala ya kusafirisha raia wake kwenda nchi ya tatu. Walisema hatua hiyo inaibua maswali ya kimaadili na kiusalama kuhusu uwajibikaji wa kimataifa katika udhibiti wa magonjwa hatari.
Walisema pia wananchi wa Laikipia wanastahili kulindwa na serikali yao na si kuwa sehemu ya majaribio ya mipango ya kimataifa isiyoeleweka vizuri.
Jana, Chama cha Madaktari, Wafamasia na Madaktari wa Meno (KMPDU) kilitoa onyo kali kikisema Kenya haijajiandaa kikamilifu kukabiliana na mlipuko wa Ebola iwapo utatokea.
Katibu Mkuu wa KMPDU, Davji Atellah, alisema mfumo wa afya nchini bado unakabiliwa na changamoto kubwa za uhaba wa watumishi, ukosefu wa vifaa vya kisasa na vitengo duni vya wagonjwa mahututi (ICU), hali inayofanya taifa kuwa katika hatari kubwa iwapo ugonjwa huo utaingia.
“Je, serikali imeweka mipango gani kwa Wakenya? Je, wahudumu wa afya wamefundishwa? Je, ICU ziko tayari? Hatupaswi kuanza kujadili makubaliano na wageni wakati Wakenya wenyewe hawana huduma bora za afya,” alisema Atellah.
Aliongeza kuwa serikali inapaswa kwanza kuimarisha hospitali, kuajiri madaktari waliokosa ajira na kuwekeza katika vifaa vya matibabu kabla ya kufikiria makubaliano ya kuanzisha vituo vya karantini kwa raia wa kigeni.
KMPDU ilisisitiza kuwa, njia bora ya kupambana na Ebola ni kuimarisha juhudi za kudhibiti ugonjwa huo katika chanzo chake, hasa DRC, ambako maambukizi yanaendelea kuripotiwa kutokana na changamoto za usalama na miundombinu.
Mahakama Kuu ilipotoa amri ya kusitisha mpango huo, ilieleza kuwa kesi hiyo inahusisha masuala mazito ya kikatiba yanayohusu afya, ushiriki wa umma na usalama wa taifa. Uamuzi huo ulifungua mlango wa mjadala mpana zaidi kuhusu uwazi wa mikataba ya kimataifa inayoathiri afya ya wananchi.
Wakati huo huo, baadhi ya maafisa wa serikali ya Amerika wameripotiwa kuonyesha matumaini kwamba, mzozo huo unaweza kutatuliwa kupitia mazungumzo na serikali ya Kenya. Hata hivyo, upande wa Kenya haujatoa maelezo rasmi ya kina kuhusu makubaliano hayo, hali iliyoongeza taharuki miongoni mwa wananchi.
Wakenya mitandaoni walikataa mpango unaopendekezwa wa kituo cha karantini ya Ebola mjini Nanyuki, kaunti ya Laikipia.
Wengi wameeleza hofu ya usalama wakitaka serikali itoe maelezo ya wazi kabla ya kukubali mpango huo. Mmoja wa watumiaji wa X aliandika: “Hatukatai msaada wa kimataifa, lakini kwa nini Laikipia na kwa nini Kenya wakati ugonjwa uko Congo?” Mwingine alisema: “Afya yetu sio majaribio ya kisiasa. Serikali itueleze ukweli wa haya makubaliano na Amerika.”
Kwenye Facebook, baadhi ya maoni yalikuwa makali zaidi, yakilenga uwazi wa serikali. Mchangiaji mmoja aliandika: “Kama Amerika wanaogopa kupeleka wagonjwa wao nyumbani, sisi tunakubali kwa nini? Hii ni hatari kwa wananchi.”
Wengine walikosoa miundombinu ya afya nchini wakisema mfumo hauko tayari. Mtumiaji mmoja alisema: “Hatutakuwa na ICU za kutosha, halafu tunaleta Ebola? Hii ni kutupeleka mautini.”
Hata hivyo, wapo wachache waliotetea mpango huo wakisema ni sehemu ya ushirikiano wa kimataifa. Mmoja aliandika: “Kama kutakuwa na ufuatiliaji mkali wa afya, ushirikiano huu unaweza kuwa na manufaa. Mjadala huo unaendelea kushika kasi mtandaoni huku #RejectEbolaFacility na nyingine zikisambaa kuonyesha jinsi suala hilo lilivyoibua wasiwasi mkubwa kitaifa .


from Taifa Leo https://ift.tt/BoE7rfu
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post