
KIONGOZI wa Chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, ameanza kujiandaa mapema kwa uchaguzi mkuu wa 2027 kwa kuunda kikosi cha wataalamu, wanasiasa na wanamikakati kitakachoendesha kampeni yake ya kuwania urais dhidi ya Rais William Ruto.
Kwa mujibu wa washirika wake, Kalonzo ameanzisha ofisi maalumu ambayo imekuwa ikifanya kazi kimyakimya kwa miezi kadhaa huku mazungumzo ya kuunda muungano wa upinzani yakiendelea. Hatua hiyo inaonyesha kuwa safari hii hataki tena kuonekana kama mgombea wa maridhiano au wa pembeni, bali analenga kuwania urais kwa nguvu zote.
Ofisi hiyo inaongozwa na Mercy Wambua, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Chama cha Wanasheria nchini (LSK). Bi Wambua amechukua nafasi ya Zein Abubakar na anatarajiwa kuratibu shughuli zote za kampeni.
Timu hiyo pia inajumuisha aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Azimio Philip Kisia, Katibu Mkuu wa Azimio Caroli Omondi, Profesa Geoffrey Mwanza Muluvi na mwanasiasa Raphael Tuju.
Wote wana uzoefu mkubwa katika kupanga kampeni za kitaifa, kusuka miungano na kusimamia shughuli za uchaguzi.
Wachambuzi wa siasa wanasema Kalonzo anajaribu kutumia miundombinu na uzoefu aliopata katika kampeni zilizopita za upinzani, hasa zile zilizoongozwa na Raila Odinga, ili kujenga msingi imara wa safari yake ya kuelekea Ikulu.
Katika hafla ya kuchangisha fedha iliyofanyika Nairobi wiki iliyopita, Kalonzo alimtambulisha Mercy Wambua rasmi kama mkuu wa ofisi hiyo na kuwasihi Wakenya kujitokeza kujitolea kwa kampeni.
“Yeye ndiye nguzo ya sekretarieti hii. Nina imani ataongoza vyema na tutahitaji mchango wa kila Mkenya katika safari hii,” alisema Kalonzo.
Tofauti na kampeni nyingi ambazo hutegemea wafadhili wakubwa, washirika wake wanasema wanataka kujenga harakati zitakazofadhiliwa na wananchi wa kawaida. Gavana wa Machakos Wavinya Ndeti anasema hata mama mboga anayechangia Sh100 atakuwa sehemu ya kumiliki kampeni hiyo na serikali itakayoundwa baadaye.
Seneta wa Makueni Dan Maanzo anasema tayari wameanzisha mfumo wa kidijitali unaofanana na ule uliotumiwa na aliyekuwa Rais wa Amerika Barack Obama, utakaowezesha Wakenya wa ndani na wanaoishi ughaibuni kuchangia fedha na kujitolea kuendesha kampeni.
Kwa mujibu wake, mfumo huo pia utarahisisha kuhamasisha wapigakura katika maeneo mbalimbali nchini kupitia mitandao ya kujitolea badala ya kutegemea viongozi wa kisiasa pekee.
“Tumekuwa tukisaidia kampeni za Raila Odinga kwa miaka 15 iliyopita. Sasa tunatumia uzoefu huo kujenga kampeni ya Kalonzo na tayari sekretarieti imeanza kufanya kazi,” alisema Maanzo.
Mbali na mikakati ya kifedha, kampeni hiyo pia inalenga kuonyesha uzoefu mkubwa wa Kalonzo katika utumishi wa umma. Washirika wake wanasema amehudumu kwa zaidi ya miaka 40 serikalini, akiwa Makamu wa Rais, Waziri wa Mashauri ya Kigeni na mwanadiplomasia, jambo linalompa uwezo wa kuongoza taifa.
Wanasisitiza pia kuwa alifanya kazi katika serikali ya Rais Mwai Kibaki wakati uchumi wa Kenya ulikuwa ukikua kwa kasi na mageuzi mbalimbali yalipotekelezwa. Hivyo basi, wanaamini rekodi hiyo inaweza kumfanya aonekane kama kiongozi mwenye uwezo wa kurejesha utulivu wa kiuchumi.
Hata hivyo, safari yake bado ina changamoto nyingi. Upinzani bado haujakubaliana kuhusu mgombeaji mmoja wa urais huku majina ya Rigathi Gachagua, Fred Matiang’i, Martha Karua na Eugene Wamalwa yakiendelea kutajwa kama wanaoweza kuwania kiti hicho.
Profesa David Monda anaamini Kalonzo ana sifa za kuwa mpatanishi na mwanasiasa mwenye uzoefu, lakini pia anakabiliwa na taswira ya kuonekana kama mwanasiasa wa kizazi cha zamani ambaye amekuwa karibu na madaraka kwa muda mrefu bila kufikia urais.
Kwa maoni yake, maandamano ya vijana wa Gen Z yalibadilisha siasa za Kenya na kuongeza hamu ya kuwa na viongozi wapya, jambo ambalo linaweza kumlazimu Kalonzo kubadilisha mikakati ili kuwavutia wapigakura vijana.
Aidha, mafanikio yake yatategemea kwa kiasi kikubwa uwezo wa upinzani kuungana na hasa iwapo ataungwa mkono na Gachagua, ambaye ameibuka kuwa mmoja wa viongozi wenye ushawishi mkubwa katika siasa za upinzani.
Kwa sasa, Kalonzo ameweka msingi wa kampeni yake mapema kuliko wengi walivyotarajia.
from Taifa Leo https://ift.tt/dBPJEou
via IFTTT
Tags
TRENDING NEWS