Mpasuko kambi ya Oburu huku Junet, Millie, Ruth na Otiende wakikosa mkutano

MKUTANO wa ODM ambao uliandaliwa Kisumu Jumapili umeanika nyufa ndani ya mrengo wa chama hicho unaoongozwa na Seneta wa Siaya Dkt Oburu Oginga na wandani wake.

Baadhi ya viongozi wakuu wa chama ambao hapo awali wamekuwa wakiibua maswali kuhusu jinsi chama kinavyoendeshwa, walisusia mkutano huo wa Kisumu.

Naibu Mwenyekiti wa ODM na Mbunge wa Rarieda Otiende Amollo, Kiranja wa Wachache Millie Odhiambo, Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kisumu Ruth Odinga na Mbunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) Winnie Odinga, wote walikosa mkutano huo.

Jumapili, umayamaya wa wafuasi wa ODM walifurika uwanja wa Kirembe eneobunge la Kisumu Mjini Magharibi ambapo jamii ya Waluo iliamua kwa kauli moja kumuunga mkono Rais Ruto kwa muhula wa pili.

Hata hivyo, kukosekana kwa Kiongozi wa Wachache Bunge la Kitaifa Junet Mohamed kulionyesha mpasuko zaidi ndani ya mrengo huo.

Bw Mohamed ambaye hapo awali alikuwa akishiriki shughuli za ODM, amekengeuka na amekuwa akihepa mikutano muhimu ya chama. Alikosa warsha ya siku tatu ya ODM Mombasa mwezi uliopita.

Mbunge huyo pia alikosa hafla ya mchango katika eneobunge lake mnamo Mei 14 ambayo iliongozwa na Mwenyekiti wa ODM Gladys Wanga, Gavana wa Migori Ochilo Ayacko na Waziri wa Fedha John Mbadi.

Bw Mohamed ambaye alikuwa mwandani wa marehemu Kiongozi wa ODM Raila Odinga, alithibitishia Taifa Leo kuwa hakuhudhuria mkutano huo lakini hakutoa sababu za kufanya hivyo.

Duru ndani ya chama zilisema Bw Mohamed huenda amekosana na uongozi wa chama na uhasama wa wazi ulijitokeza kwenye warsha ya Mombasa.

“Wandani wake wanasema hana raha kuhusu jinsi chama kinavyoendeshwa kutokana na ukosefu wa mipango ya muda mrefu,” duru za chama zikaarifu.

Dkt Otiende Amollo na Bi Ruth waliambia Taifa Leo kuwa walikuwa na shughuli nyingine zilizosababisha wakose mkutano huo.

“Ulikuwa mkutano wa lazima? Nilihudhuria ule wa Mombasa lakini nikakosa huu wa Kisumu kwa sababu nilikuwa na shughuli Nairobi”

Alipoulizwa kuhusu jinsi ambacho chama kinaendeshwa, alielekeza Taifa Leo kwenye mahojiano yake na gazeti hili majuzi ambapo alikosoa chama kwa kutotoa nafasi kwa viongizi chipukizi.

Hasa alikosoa chama kwa kuwavuruga Katibu Mkuu Edwin Sifuna na Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino ambao wapo mrengo wa Linda Mwananchi.

Dkt Omollo na Bi Ruth hivi majuzi walidai kuwa kumtimua Bw Sifuna ilikuwa kosa la kisiasa lililofanywa na mrengo wa Dkt Oginga.

Gavana wa Kisumu Anyang Nyongó ambaye alihudhuria mkutano wa Kisumu alizua maswali kuhusu baadhi ya maamuzi ya chama.

Profesa Nyongó alisema mustakabali wa ODM hautaamuliwa na ngome zake Luo Nyanza pekee bali hata maeneo mengine ya nchi.



from Taifa Leo https://ift.tt/nopkSzM
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post