
GAVANA wa Trans Nzoia George Natembeya amekwezwa kisiasa baada ya upinzani kumteua kama kigogo na mratibu wa shughuli zao zote katika Ukanda wa Magharibi mwa nchi.
Tangazo hilo lilitolewa na aliyekuwa Naibu Rais, Rigathi Gachagua, wakati wa mkutano wa kisiasa uliofanyika Kitale Jumapili iliyopita na kuhudhuriwa na kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, kiongozi wa DAP-Kenya, Eugene Wamalwa pamoja na viongozi wengine wa upinzani.
Uamuzi huo unampa Bw Natembeya jukumu la kuratibu shughuli za kisiasa katika kaunti za Trans Nzoia, Bungoma, Busia, Kakamega na Vihiga.
Hatua hiyo pia inamuinua Bw Natembeya kutoka nafasi ya uongozi wa kaunti hadi kuwa mmoja wa viongozi muhimu katika juhudi za kutafutia upinzani kura na kuwasaidia kuwafikia wananchi mashinani katika jitihada za kusaka uungwaji mkono.
Vigogo wengine wa upinzani waliohudhuria mkutano huon ni aliyekuwa Spika wa Bunge la Kitaifa, Justin Muturi, Mbunge wa Saboti, Caleb Amisi na Mbunge wa Mumias Mashariki, Peter Salasya.
Wote kwa kauli mmoja walisisitiza upinzani kumsimamisha mgombeaji mmoja mnamo 2027.
Magharibi mwa Kenya imeendelea kuwa ngome muhimu ya kisiasa kutokana na idadi kubwa ya wapigakura huku iking’ang’aniwa na kila mrengo wa kisiasa.
Kwa mujibu wa takwimu za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC) eneo hilo litakuwa na zaidi ya wapigakura milioni 3.2 kufikia 2027.
Bw Gachagua alisema upinzani unalenga kuimarisha umoja wa eneo hilo na kuzuia juhudi zozote za kugawanya kura zake huku akimtaja Bw Natembeya kama mwanasiasa tegemeo wa kuwavumisha mrengo wa upinzani.
“Nawaomba mumuunge mkono Gavana Natembeya kwa muhula wa pili na atakuwa akiongoza kampeni zetu eneo hili. Sote tunashirikiana kumwondoa Rais Ruto madarakani 2027,” akasema
“Iwe ni Eugene, Natembeya, Matiang’i au Kalonzo, tutamuunga mkono,” akaongeza.
Katika mkutano huo, Bw Gachagua aliishutumu serikali ya Kenya Kwanza kwa usimamizi mbaya wa uchumi, akisema upinzani utatilia mkazo kufufua uchumi hasa sekta ya kilimo.
Bw Natembeya amejizolea umaarufu wa kisiasa kitaifa kutokana na misimamo yake kuhusu utawala bora na uwajibikaji na wadadisi wa kisiasa wanamtaja kama mmoja wa viongozi wanaoibuka ambao wana ushawishi mkubwa katika siasa za 2027 na 2032.
Ingawa majukumu yake mapya hayajafafanuliwa rasmi, uteuzi huo unaonekana kuwa mbinu ya upinzani ya kuwa na vigogo wa kuongoza kampeni zake maeneo mbalimbali nchini.
Katika hotuba yake, Bw Natembeya alisema yupo tayari kupambana na wapinzani wake wa kisiasa kwenye ugavana wa Trans Nzoia.
Aliyekuwa Mbunge wa Kimilili Chris Wamalwa na Waziri wa zamani wa Afya Susan Nakhumicha na Mbunge wa Kiminini Kakai Bisau ni kati ya wale wanaolenga ugavana Trans Nzoia 2027.
Wakati wa mkutano huo Diwani wa Wadi ya Bidii James Mwangi alitangaza kuwa amehama UDA na kujiunga na mrengo wa upinzani huku akiahidi kumpigia Bw Natembeya kampeni kali ya kutetea kiti chake.
from Taifa Leo https://ift.tt/34vYAdu
via IFTTT