
ENEO la Magharibi limeibuka kuwa ulingo mpya wa kisiasa unaong’ang’aniwa na mirengo mikuu kuelekea uchaguzi wa 2027, takwimu za Tume ya Uchaguzi (IEBC) zikiashiria litakuwa na zaidi ya kura milioni 3.2.
Idadi hiyo ya juu ya wapigakura imewavutia wanasiasa wakuu ambao baadhi yao wamemwaga ahadi kochokocho, ikiwemo kulitengea eneo hilo nafasi ya mgombea mwenza 2027 na urais 2032.
Wandani wa Rais William Ruto wameambia eneo hilo lijiandae kutoa mrithi wake 2032 huku wanasiasa wa Muungano wa Upinzani wakifichua nia yao ya kulituza nafasi ya mgombea mwenza.
Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna, ameibuka kuwa mwanasiasa maarufu zaidi anayepigiwa upatu kuwa mshikilizi wa nafasi ya naibu rais katika mrengo wa upinzani akiegemea Linda Mwananchi.
Magharibi inajumuisha kaunti za Vihiga, Busia, Kakamega, Bungoma na Trans Nzoia na kwa mujibu wa takwimu za IEBC itakuwa na zaidi ya kura 3.2m katika uchaguzi ujao. Mrengo wa Rais Ruto una Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi, Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula na Waziri wa Vyama vya Ushirika Wycliffe Oparanya, Gavana wa Kakamega, Fernandes Barasa na Katibu Mkuu wa COTU Francis Atwoli, wote kutoka Magharibi.
Viongozi hao wamekuwa wakiwahimiza wakazi kwamba Magharibi ina nafasi ya kumrithi Dkt Ruto 2032 iwapo atashinda muhula wa pili.
Aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua na Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka wanawategemea waziri wa zamani Eugene Wamalwa anayeongoza chama cha DAP-K, Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya na aliyekuwa seneta wa Kakamega Cleophas Malala kuwahi kura za eneo hilo.
Bw Sifuna na Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi pia wameungana katika juhudi za kuilambisha serikali sakafu kupitia mrengo wao wa Linda Mwananchi.
Wikendi iliyopita, viongozi wa Serikali na Upinzani walipiga kambi Magharibi, eneo ambalo halijaelekeza kura zake katika kapu moja tangu kifo cha aliyekuwa Makamu wa Rais Michael Wamalwa mnamo 2003.
Bw Mudavadi aliwakemea viongozi wa Upinzani kwa madai ya kujaribu kupotosha wakazi, akisema wananufaika zaidi wakiwa serikalini kuliko Upinzani.
“Kuna watu wanaojaribu kuelekeza jamii yetu kusikofaa ilhali walishawahi kuondolewa madarakani na hawajui mustakabali wao. Sisi kama viongozi wenu tumeamua kumuunga mkono Rais Ruto,” akasema Bw Mudavadi.
“Niliwaambia 2022 kwamba Ruto ndiye njia, na sasa nawaambia tena bado ndiye njia. Tuwe makini na tusidanganywe,” akaongeza.
Bw Mudavadi, Wetang’ula na Oparanya ni kati ya viongozi wakongwe ambao wameamua mkondo wa siasa za Magharibi kwa miaka mingi.
Bw Wetang’ula amekuwa akiwapokea wajumbe nyumbani kwake Kabuchai, Bungoma na kuhudhuria shughuli za kupiga jeki makundi mbalimbali ya wanawake na vijana.
“Msiruhusu watu wa nje kuwagawanya kwa msingi wa kikabila. Tukibaki tumeungana, mmoja wetu bila shaka atashinda urais 2032,” alisema Bw Wetang’ula akiwa ameandamana na wabunge wanaounga mkono serikali eneobunge la Khwisero.
Gavana wa Bungoma Ken Lusaka ni miongoni mwa viongozi wanaosema wazi kuwa fursa bora ya eneo hilo ni 2032 badala ya kuwania urais 2027.
Baada ya ziara ya siku tatu Kakamega, Trans Nzoia na Bungoma, viongozi wa Upinzani sasa wanaonekana kuteka eneo hilo kisiasa.
“Tumeungana na 2027 tutaiangusha serikali ya Ruto wala hakuna mgawanyiko. Zaidi ya asilimia 80.5 watapiga kura ya kumwondoa Ruto,” akasema Malala.
Kupanda kwa sifa za Bw Sifuna kumefurahisha Magharibi huku Bw Osotsi, Seneta Khalwale na baadhi ya wazee wakimuidhinisha kama kigogo wao na kumtaka awanie urais.
Katika mikutano mbalimbali, wananchi huondoka au kuwazomea viongozi wanaompinga Bw Sifuna.
Kwa mujibu wa utafiti wa TIFA uliotolewa mwezi uliopita, Bw Sifuna ndiye kiongozi maarufu zaidi miongoni mwa jamii ya Waluhya akiwa na uungwaji mkono wa asilimia 44.
Ushirikiano wake na Kalonzo Musyoka pia unazidi kushabikiwa miongoni mwa wafuasi wa upinzani.
Seneta huyo wa Nairobi amefanya mikutano katika kaunti zote za Magharibi, ambapo amepata uungwaji mkono mkubwa, ingawa bado hajatangaza hadharani kama atagombea urais.
“Katika kundi letu tuna Natembeya na Osotsi, na kiongozi tunayempigia debe ni Sifuna,” akasema Dkt Khalwale akikanusha kuwa mrengo wa Umoja wa Upinzani umeteka eneo hilo kisiasa.
Licha ya kupiga kura marehemu Raila Odinga tangu 2007, eneo hilo mara nyingi limegawanya kura zake.
from Taifa Leo https://ift.tt/T53ib9n
via IFTTT