
KENYA inaelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027 huku ndimi za moto za wanasiasa zikianza kuwaka, hali inayozua hofu ya kuibuka kwa siasa za chuki, ukabila na ghasia.
Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) imeanza kuchunguza matamshi ya viongozi mbalimbali ambayo inasema yanaweza kuchochea migawanyiko ya kikabila, ghasia au kuvuruga amani nchini.
Miongoni mwa viongozi walioangaziwa na tume hiyo ni aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, ambaye ameagizwa kufika mbele ya NCIC Agosti 27 kuelezea kuhusu matamshi aliyotoa katika mikutano ya kisiasa kaunti za Vihiga, Kisii na Meru.
Bw Gachagua, ambaye sasa anaongoza chama cha Democracy for Citizens Party (DCP), atahojiwa kuhusu muktadha, nia na athari zinazoweza kusababishwa na kauli hizo.
NCIC imesema matamshi hayo yanaweza kuwa ya ubaguzi au ya kuchochea. Tume imeambatanisha agizo hilo na nakala za matamshi inayochunguza.
Afisa Mkuu Mtendaji wa NCIC Daniel Giti ameonya kuwa iwapo Bw Gachagua hatafika mbele ya tume, huenda akakamatwa na kuwasilishwa mbele ya tume.
Uchunguzi huo unafanyika huku wanasiasa wakizidisha kampeni za mapema kuelekea uchaguzi wa 2027, mikutano ya kisiasa ikigeuka kuwa majukwaa ya mashambulizi makali dhidi ya wapinzani.
Katika tukio moja linalochunguzwa, Bw Gachagua anadaiwa kutoa matamshi katika mkutano Luanda, Vihiga, Juni 12 ambayo tume inasema yanaweza kuchochea mgawanyiko wa kikabila.
Pia anahojiwa kuhusu kauli alizotoa katika Uwanja wa Gusii, Kisii, Februari 23, ikiwemo zilizomhusu Mbunge wa Nyaribari Chache Zaheer Jhanda.
Ziara yake ya Meru mwishoni mwa Julai pia inamlikwa na NCIC baada ya tume kusema baadhi ya matamshi aliyotoa yanaweza kuchukuliwa kuwa ya kuchochea vurugu na kulenga jamii fulani.
Lakini Bw Gachagua si mwanasiasa pekee anayechunguzwa.
Gavana wa Busia Paul Otuoma pia ameitwa na NCIC kujibu madai ya kuchochea hisia dhidi ya wafanyabiashara kutoka maeneo mengine ya nchi katika mkutano wa hadhara huko Bulanda Junction mnamo au karibu na Juni 27.
Mbunge wa Homa Bay Town Peter Kaluma anakabiliwa na uchunguzi kama huo kuhusu matamshi aliyotoa kabla ya mkutano wa Linda Mwananchi uliofanyika Homa Bay Agosti 16.
Bw Kaluma aliitwa kufika mbele ya tume Jumatano.
Wanasiasa wengine wanaochunguzwa ni Waziri wa Afya Aden Duale, Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku, Mbunge wa Mukurwe-ini John Kaguchia, Mbunge wa Sirisia John Waluke na Naibu Gavana wa Mandera Ali Mohamud.
NCIC ilitangaza Julai 28 kuwa imeanza kuchunguza matamshi yaliyohusishwa na baadhi ya viongozi hao, akiwemo Bw Duale, Bw Ruku, Bw Otuoma na Bw Waluke.
Wengine ni Mbunge wa Kipipiri Wanjiku Muhia na Mbunge wa Nakuru Town East David Gikaria.
Mwenyekiti wa NCIC Kepha Omae alisema mazingira ya kisiasa nchini yanaendelea kuwa makali huku matamshi ya uchochezi, vitisho na siasa za kikabila yakizidi.
“Tunaona mazingira ya kisiasa yanayozidi kuwa makali ambapo matamshi ya uchochezi, kulenga jamii fulani, vitisho na kuwachochea vijana vikiwa jambo la kawaida,” alisema.
Hata hivyo, alisema NCIC haiwezi kukimbilia kufikisha kesi kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) bila kuwa na ushahidi wa kutosha.
“Hauwezi kupeleka faili kwa DPP achukue hatua bila ushahidi wa kutosha. Ndio maana kesi nyingi huishia hapo,” alisema.
Bw Omae alisema wachunguzi wa tume hulazimika kusafiri hadi maeneo ambako matamshi hayo yalitolewa, kubaini muktadha wake na kutafuta mashahidi walio tayari kutoa taarifa rasmi.
Alisema tatizo kubwa ni kwamba Wakenya wengi huwa wepesi kuripoti matamshi yanayowaudhi lakini husita kuwa mashahidi.
“Wakenya ni wazuri katika kuripoti na kulalamika lakini wanapotakiwa wawe mashahidi na hata kuweka malalamiko yao kwa maandishi hawataki kwa sababu wanafikiri wataitwa mahakamani,” alisema.
NCIC imesema imefanikisha hukumu tano huku kesi nyingine tatu zikiwa mahakamani. Hata hivyo, hakuna mwanasiasa aliyepatikana na hatia katika kesi hizo.
Malalamiko yaliyohusu mwanaharakati wa haki za binadamu Khelef Khalifa, Mbunge wa Tigania East Mpuru Aburi na chifu mkuu Wilson Kaloi yalikataliwa na DPP kwa sababu ya kukosa ushahidi wa kutosha.
Kesi ya mbunge Peter Salasya nayo ilisitishwa baada yake kuomba msamaha.
Uchunguzi wa sasa umeibua mjadala kuhusu iwapo taasisi za serikali zinachukua hatua mapema ya kutosha kuzuia matamshi hatari kabla hayajageuka kuwa vurugu.
NCIC imekuwa ikichunguza pia matukio ya nyuma tangu uchaguzi wa 2022.
Wakati wa uchaguzi mdogo wa Ol Kalou, Mbunge wa Kipipiri Wanjiku Muhia na Bw Gikaria walitozwa faini ya Sh1.5 milioni na Sh2.5 milioni mtawalia na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwa kukiuka kanuni za maadili ya uchaguzi.
Huku hayo yakijiri, baadhi ya wanasiasa wamejikuta wakilazimika kuomba msamaha baada ya matamshi yao kuzua hasira.
Katibu Mkuu wa UDA Hassan Omar alikabiliwa na wito wa kujiuzulu mwezi Mei baada ya matamshi yake kutafsiriwa na wakosoaji kuwa yalilenga jamii fulani. Baadaye aliomba msamaha.
Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga pia aliomba msamaha na kujiuzulu kama naibu mwenyekiti wa Baraza la Magavana baada ya matamshi yake kufuatia kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga Novemba 2025 kuzua ukosoaji.
Wakati huo huo, Bw Duale anaendelea kuchunguzwa kuhusu matamshi aliyotoa katika hafla ya umma eneo la Lafey, Mandera.
Waziri huyo amekana kufanya kosa akisema matamshi yake yalipotoshwa na kutolewa nje ya muktadha.
Mwakilishi wa Wanawake wa Murang’a Betty Maina pia ameangaziwa na NCIC kutokana na matamshi aliyotoa dhidi ya Bw Gachagua.
from Taifa Leo https://ift.tt/8ITJije
via IFTTT