Ndoa baridi za magavana na manaibu wao uchaguzi 2027 ukibisha

MAGAVANA kadhaa wanaowania muhula wa pili wanakabiliwa na kibarua kigumu cha kutafuta manaibu wapya baada ya uhusiano wao na waliowasaidia kushinda uchaguzi wa 2022 kuvurugika.

Takriban magavana 10 wamejipata katika hali hii huku uchaguzi wa 2027 ukikaribia, na sasa wanatafuta washirika wapya watakaowasaidia kuhifadhi viti vyao.

Mzozo wa hivi majuzi kati ya Gavana wa Kericho Erick Mutai na naibu wake Fred Kirui umeongeza orodha ya magavana waliokosana na manaibu wao.

Wengine wanaotafuta manaibu wapya ni magavana wa Trans Nzoia George Natembeya, Elgeyo Marakwet Wisley Rotich na Siaya James Orengo.

Magavana wa Homa Bay Gladys Wanga, Kisii Simba Arati na Uasin Gishu Jonathan Bii pia wametofautiana na manaibu wao.

Gavana wa Machakos Wavinya Ndeti na Abdi Guyo wa Isiolo pia wamewahi kuwa na uhusiano baridi na manaibu wao.

Kati ya magavana 29 wanaowania muhula wa pili, ni 19 ambao hawajawahi kuripotiwa kukosana na manaibu wao tangu walipochaguliwa mwaka 2022.

Kaunti hizo ni Nairobi, Kakamega, Busia, Migori, Nakuru, Nyamira, Samburu, Turkana, Kiambu, Murang’a, Nyandarua, Makueni, Embu, Meru, Mandera, Taita Taveta, Kilifi, Kwale na Mombasa.

Lakini uhusiano mzuri wa sasa haumaanishi kwamba magavana hao wataendelea kuwa na manaibu hao, hasa wakati wanasiasa wanapopanga upya ushirikiano kuelekea 2027.

Kikatiba, kila anayewania ugavana anapaswa kumteua mtu wa kuwa mgombea mwenza ambaye huwa naibu gavana.

Uhusiano kati ya magavana na manaibu wao umekuwa ukigubikwa na migogoro, maslahi ya binafsi, makubaliano yaliyovunjwa na wakati mwingine kuvumiliana.

Huko Kericho, Bw Mutai alitangaza Jumanne kwamba amekata uhusiano wa kisiasa na Bw Kirui, akimlaumu kwa kuhusika katika majaribio mawili ya kumng’atua.

Alisema sasa atashirikiana na waziri wa Fedha na Mipango ya Kiuchumi wa kaunti Jackson Rop, ambaye anatoka eneo la Kipkelion Magharibi sawa na Bw Kirui katika uchaguzi wa 2027.

Bw Kirui alidai awali kuwa wawili hao walikubaliana kugawana nyadhifa za serikali ya kaunti kwa uwiano wa asilimia 60 kwa 40, lakini mpango huo haukutekelezwa.

Bw Mutai alinusurika majaribio mawili ya kumtimua, mwaka 2024 na 2025, baada ya Seneti kuyakataa.

Huko Elgeyo Marakwet, uhusiano kati ya Bw Rotich na naibu wake Grace Cheserek pia umeharibika.

Mzozo wao uliibuka hadharani hivi majuzi baada ya Bi Cheserek kumkabili gavana wakati wa hafla ya uzinduzi wa Biblia iliyotafsiriwa kwa lugha ya Kimarakwet.

Huko Trans Nzoia, Bi Philomena Kapkory amekuwa akizozana na Bw Natembeya tangu 2023, akidai kutengwa katika maamuzi na usimamizi wa serikali ya kaunti.

Siaya pia imekumbwa na mzozo kama huo, huku Naibu Gavana William Oduol akidai uhusiano wake na Bw Orengo umedorora kabisa.

Na katika kaunti ya Homa Bay, Bw Wanga alimtimua naibu wake Oyugi Magwanga baada ya kumuunga mkono mgombea huru katika uchaguzi mdogo wa Kasipul badala ya mgombea wa ODM.

Kisii pia ilishuhudia Naibu Gavana Robert Monda akiondolewa kupitia mchakato wa kumtimua mwaka 2024 baada ya mzozo wa kisiasa na Bw Arati.

Na katika kaunti ya Uasin Gishu, Naibu Gavana John Barorot alijiuzulu mwaka 2024 na nafasi hiyo ikachukuliwa na MCA Evans Kapkea.

Tangu kuanzishwa kwa serikali za ugatuzi mwaka 2013, ni manaibu gavana 15 pekee ambao wamewahi kubaki na wakubwa wao katika uchaguzi uliofuata.

Hii inaonyesha ugumu wa “ndoa” ya kisiasa kati ya magavana na manaibu wao, ambayo mara nyingi huvunjika kabla ya kufika mwisho wa muhula.



from Taifa Leo https://ift.tt/pwsU4c2
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post