
KENYA itachukua hatua muhimu kujinafasi kama kituo kikuu cha nishati na viwanda kikanda Rais William Ruto atakapoongoza hafla ya kuzindua mradi uliopendekezwa wa Kiwanda cha Mafuta Afrika Mashariki mjini Lamu hapo kesho, chenye thamani ya Sh2 trilioni.
Kiwanda hicho chenye uwezo wa kusafisha mapipa 700,000 kwa siku kinachofadhiliwa na bilionea wa Nigeria Aliko Dangote, kinatarajiwa kuwa kikubwa zaidi cha aina hiyo Afrika Mashariki na kusambaza bidhaa za petroli nchini na masoko ya nchi jirani.
Eneo lake katika Bandari ya Lamu vilevile inatarajiwa kuimarisha nafasi ya Kenya kama kituo kikuu cha kawi na biashara barani.
Kulingana na serikali, hafla hiyo itahudhuriwa na viongozi kadhaa wa mataifa na wageni wengineo wa ngazi za juu huku Bw Dangote akiwa miongoni mwa wanaotarajiwa kuhudhuria.
Nyuma ya uwekezaji huo, uwezo wake na maazimio makuu kuhusu mradi huo ni mwanamme ambaye jina lake limehusika kwa karibu na ufanisi wa biashara barani Afrika.
Dangote anachukuliwa kuwa mtu tajiri zaidi Afrika huku jarida la Forbes likikadiria mali yake kuwa na thamani ya Sh4.7 trilioni kufikia Septemba 2026.
Ni mwasisi, rais na mkurugenzi wa kampuni kwa jina Dangote Group, moja kati ya mashirika makubwa zaidi ya biashara Afrika Magharibi.
Maisha yake yalianzia Kano, Nigeria, alipozaliwa Aprili 10, 1957, katika familia tajiri ya Hausa Muslim.
Mama yake Mariya Sanusi Dantata alitoka familia yenye ushawishi mkuu ya wafanyabiashara, Dantata huku baba yake Mohamed Dangote, akiwa mfanyabiashara na mshiriki wa Dantatas.
Biashara, hivyo basi, haikuwa jambo geni kwa familia ya Dangote, ilikuwa sehemu ya mazingira alimokulia bilionea huyo.
Kupitia mama yake, Dangote ni kitukuu wake Alhassan Abdullahi Dantata, moja kati ya watu tajika na wafanyabiashara wakwasi Afrika Magharibi enzi ya ukoloni wa Uingereza.
Dantata alijenga mali yake kupitia biashara ya bidhaa, ikiwemo kola nuts na njugu karanga na kuanzisha himaya ya biashara ambayo baadaye ingeunda sehemu ya urithi wa familia ya Dangote.
Yamkini hata jina lake lilidokeza kuhusu kilichosubiri mbele. Kulingana na biografia, Aliko ina maana ya “mshindi anayetetea binadamu.”
Dangote kisha aliunda himaya ya biashara ambayo viwanda, mashamba, vituo vya mafuta na bidhaa nyinginezo zimeajiri maelfu ya watu kote Afrika.
Alilelewa kama Muislamu abapo alipokea mafunzo ya kidini katika madrassa kabla ya kuendelea na elimu yake rasmi.
Baadaye alihudhuria shule ya serikali na kukamilisha elimu ya sekondari katika miaka ya 1970.
Alisafiri Cairo, Misri ambapo alisomea Taaluma ya Biashara na Usimamizi katika chuo kikuu cha Al-Azhar.
Aliporejea Nigeria, Dangote alijitosa katika tasnia ya biashara akisaidia na familia yake kifedha.
Simulizi ya taaluma yake mwanzoni inasema alipata mkopo kutoka kwa mjomba yake na kutumia hela hizo katika biashara ya bidhaa kama vile mchele, sukari, na simiti.
1978, Dangote alianza rasmi taaluma yake ya biashara. Kufikia1981 biashara yake iligeuka Dangote Group.
from Taifa Leo https://ift.tt/iPKWZJb
via
IFTTT