Kundi la Linda Mwananchi linaloongozwa na Sifuna, Babu lapokelewa kwa kishindo Kisumu

VIONGOZI wa Linda Mwananchi jana waliteka jiji la Kisumu kwa kishindo huku wakidai wao ndio wana maono ya marehemu kigogo wa siasa za Luo Nyanza Raila Odinga. Gavana wa Siaya James Orengo, Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna, Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino wakiwa wameandamana na wanasiasa wengi waliteka jiji la Kisumu kabla ya kuhutubia umayamaya wa watu kwenye uga wa Kowuor eneobunge la Kisumu mjini Mashariki. Kuelekea mkutano huo kulikuwa na taharuki jijini humo kutokana na madai kuwa makabiliano yangezuka kati ya wafuasi wa Linda Mwananchi na Linda Ground. Kulikuwa na makabiliano kati ya makundi hayo mawili kwenye mzunguko wa Kachok katika barabara ya Kisumu-Nairobi lakini polisi wakaingilia kati na kutuliza hali kwa kurusha vitoza machozi. Bw Orengo alimshutumu Rais William Ruto akidai amekuwa akihusika na mauaji ya waandamanaji. “Hii ndiyo maana tunampleka Ruto nyumbani. Aliwaua Baby Pendo, Albert Ojwang’ na Gen Z,” akasema Bw Orengo. Aliwashutumu baadhi ya viongozi wa ODM akiwataja Dkt Oburu Oginga, Gavana wa Gladys Wanga na Kiongozi wa Wachache Bungeni Junet Mohamed akidai ‘waliuza’ ODM. Aidha alisisitiza kuwa Kundi la Linda Mwananchi litakuwa na mwaniaji wa urais 2027. “Kuna watu ambao walikuwa wakilala kwenye madarasa ya Raila Odinga. Waache sisi ambao tulikuwa tukimakanika darasani tusalie na uongozi wa chama,” akasema Bw Orengo. Alidai kuwa Bw Odinga alikuwa amemwonya dhidi ya kuendelea kushirikiana na Rais William Ruto. “Marehemu Raila Odinga aliniambia hakuna haja ya kutembea na viongozi kama Rais Ruto,” akaongeza seneta huyo wa zamani Siaya. Huku wakikariri kuwa wao ndio wana maono ya Raila Odinga, viongozi hao walisema Rais Ruto, Dkt Oginga, Bi Wanga na Bw Mohamed ndio tatizo ndani ya ODM. Bw Sifuna alidai kuwa alihadaiwa kusafiri hadi India kuleta mwili wa marehemu Raila Odinga nyumbani baada ya mauti ya waziri huyo mkuu wa zamani. “Niliabiri ndege hiyo bila kujua ilikuwa ni mpango. Tukiwa India, watu hawa walimweka Dkt Oburu Oginga kama kiongozi wa chama,” akasema huku akisisitiza kuwa ndiye katibu halisi wa ODM. Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi naye alishutumu viongozi wa ODM kwa kuandaa mikutano ya chama katika ikulu ya Nairobi. “Kabla ya mwili wa Raila kuja, watu hawa waliandaa mkutano ikulu na kumweka Dkt Oburu Odinga kama kiongozi wa chama. Raila Odinga aliweka wazi kuwa iwapo hayuko, Profesa Anyang’ Nyong’o atasimamia chama lakini hao watu wakaenda ikulu na kumpa Dkt Oburu uongozi wa ODM,” akasema Bw Osotsi. “Walisema Raila alipoaga dunia sasa wao ni mayatima na mayatima huwa wana masharti. Walitupeleka kwa Rais Ruto atuongoze na sasa wanaendesha mikutano ya ODM ndani ya Ikulu,” akaongeza. Bw Owino aliwaambia wafuasi kuwa ziara yao Kisumu ilikuwa ya amani na yalimakinikia tu mazungumzo na wananchi. “Huku ni nyumbani na ukienda nyumbani huji na ghasia bali amani na upendo. Tumekuja hapa kuzungumza na Wakenya,” akasema Bw Owino. Aliwashutumu baadhi ya wanasiasa kutoka Kisumu kwa kufadhili na kupanga ghasia dhidi yake na akawaomba vijana wajiepushe kutumiwa na wanasiasa kueneza ghasia.

“Kwa wanasiasa wanaowalipa wahuni, tunawajua. Mmepewa pesa kupanga ghasia lakini hamtaongoza Kisumu,” akasema Bw Owino akiwataka wakazi wamakinikie maendeleo ya kiuchumi.

Licha ya vitisho na madai ya kukodishwa kwa wahuni kuvuruga mkutano wa Linda Mwananchi, viongozi wake walienda ibada kanisani, wakaandaa mikutano kando kando ya barabara na kuhutubia mkutano mkubwa uwanja wa Kowuoro karibu na mtaa wa Elgon. Mnamo Jumamosi, viongozi hao walitembelea kaburi la Raila, Kangó ka Jaramogi eneobunge la Bondo kisha kuweka maua kwenye kaburi hilo pamoja na la babake marahemu Jaramogi Oginga Odinga.

from Taifa Leo https://ift.tt/lxZSzFw
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post