
KIONGOZI wa Wiper Kalonzo Musyoka amezua mjadala kuhusu msimamo wake wa kisiasa baada ya kuonyesha dalili ya kuwa atashiriki handisheki na Rais William Ruto upinzani ukishindwa uchaguzi wa 2027.
Bw Musyoka amesisitiza kuwa siasa za ushindani kati ya Rais Ruto na vinara wa upinzani inastahili kuzingatia masuala yanayohusisha maslahi ya nchi badala ya uhasama wa kisiasa.
“Ukitushinda, tunaweza kutathmini ukiwa na tabia nzuri. Tukikushinda, tutaangalia masuala haya yote. Tuangaliane kwa sababu tuna nchi na Mungu haheshimu binadamu licha ya hadhi yake,” akasema Bw Musyoka.
Bw Musyoka alikuwa akizungumza jana katika Kaunti ya Siaya ambayo ni ngome ya kisiasa ya marehemu kigogo wa siasa za upinzani Raila Odinga.
Hatua ya kinara huyo wa Wiper kumsifu Rais Ruto imeibua mjadala kuhusu mahali ambapo uaminifu wake wa kisiasa upo. Siku tatu zilizopita alimsifu Rais kwa kujenga barabara inayoelekewa kwake Tseikuru.
“Bw Ruto kwa sababu ya kuogopa sisi ameweka bidii barabara ifike Tseikuru na namwambia awekee bidii imechelewa kwa sababu barabara hiyo ingekuwa imefika Maua. Bw Ruto anatumiwa na Mungu kwa njia spesheli. Kuweka hiyo bidii si Ruto ni Mungu. Kufikia Agosti mwaka tukikuja nyumbani itakuwa imekaribia sana,” akasema Bw Musyoka wakati wa Ukumbusho wa miaka 20 tangu mauti ya mamake.
“Sasa tuna chuo cha kitaifa cha kiufundi baada ya kuongea na Ruto. Tunakubali kuwa hii inafaa kuwa chuo cha kitaifa cha kiufundi,” akaongeza.
Kauli ya Bw Musyoka imekuja wakati ambapo kuna kutoaminiana ndani ya upinzani huku Rais Ruto akitumia kauli za kiongozi huyo wa Wiper kumkejeli na kusema kuwa ni kati ya viongozi wanayemtambua kazi yake.
Aidha Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki miezi ya nyuma amekuwa akimsifu Bw Musyoka na kumrejelea kama kiongozi muungana ambaye anastahili kuungana na serikali ili kuwafanyia Wakenya kazi.
Jana Bw Musyoka pia aliitaka serikali kuelekeza nguvu kwa wapinzani watakaokuwa kwenye debe badala ya kumlenga Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.
from Taifa Leo https://ift.tt/1MFof0d
via IFTTT
Tags
TRENDING NEWS